Waamuzi 19 - Swahili Revised Union Version - SRUVDCSuria wa Mlawi 1 Ikawa katika siku hizo, kulipokuwa hakuna mfalme katika Israeli, alikuwapo Mlawi mmoja aliyekuwa akikaa kama mgeni upande wa mbele wa nchi ya vilima vilima ya Efraimu, aliyejitwalia suria katika Bethlehemu-yuda. 2 Kisha huyo suria wake akamkasirikia, akamwacha kwenda nyumbani kwa baba yake huko Bethlehemu-yuda, akakaa huko muda wa miezi minne. 3 Kisha mumewe akaondoka akamfuata, aseme naye kwa upendo, ili apate kumrudisha tena, naye alikuwa na mtumishi wake pamoja naye na punda kadhaa; huyo mwanamke akamkaribisha katika nyumba ya baba yake; naye baba yake alipomwona akafurahi kuonana naye. 4 Kisha mkwewe, babaye huyo mwanamke, akamzuia; akakaa naye siku tatu; basi wakala na kunywa na kulala huko. 5 Kisha ilikuwa siku ya nne, wakaamka asubuhi na mapema, naye akaondoka ili aende zake; baba yake huyo mwanamke akamwambia mkwewe, Tunza moyo wako, ule chakula kidogo, kisha baadaye mtakwenda zenu. 6 Basi wakaketi, wakala na kunywa wote wawili pamoja; kisha baba yake mwanamke akamwambia huyo mtu, Uwe radhi, tafadhali, ukae usiku kucha, na moyo wako na ufurahi. 7 Yule mtu akainuka ili aondoke; lakini mkwewe akamsihi sana, naye akalala huko tena. 8 Basi akaamka asubuhi na mapema siku ya tano ili aende zake; na baba yake mwanamke akasema, Tunza moyo wako, tafadhali, ukae hadi jua litue; nao wakala chakula wote wawili. 9 Kisha hapo mtu huyo alipoinuka ili aende zake, yeye na suria wake, na mtumishi wake, huyo mkwewe, baba yake mwanamke, akamwambia, Tazama mchana wakaribia jioni, tafadhali kaa usiku kucha; tazama mchana wakaribia mwisho wake, lala hapa, ili moyo wako ufurahi; hata kesho uende zako asubuhi na mapema, ili upate kwenda kwenu. 10 Lakini huyo mtu hakukubali kukaa usiku huo, ila akainuka, akaenda zake, akafika mkabala wa Yebusi (huo ndio Yerusalemu); nao walikuwako pamoja naye punda kadhaa waliotandikwa; suria wake naye alikuwa pamoja naye. 11 Basi hapo walipokuwa karibu na Yebusi, mchana ulikuwa umeendelea mno; yule mtumishi akamwambia bwana wake, Haya, tafadhali, tuende kando na kuingia mji huu wa Wayebusi, tulale humu. 12 Bwana wake akamwambia, Hatutageuka sisi kuingia mji wa wageni, ambao si wa wana wa Israeli; lakini tutapita mpaka Gibea. 13 Kisha akamwambia mtumishi wake, Haya, tuifikie miji hii mmojawapo nasi tutalala katika Gibea au katika Rama. 14 Basi wakashika njia na kuendelea; jua likawachwea walipokuwa karibu na Gibea, ambao ni mji wa Benyamini. 15 Wakageuka huko, wapate kuingia na kulala katika Gibea; akaingia ndani, akaketi katika eneo la mji lililokuwa wazi; kwa kuwa hapakuwa na mtu yeyote aliyewakaribisha nyumbani kwake kulala. 16 Kisha, tazama, akatokea mwanamume mzee, akitoka kazini kwake shambani, wakati wa jioni; mtu huyo alikuwa ni wa ile nchi ya vilima vilima ya Efraimu, naye alikuwa anakaa katika Gibea kama mgeni lakini wenyeji wa mahali hapo walikuwa Wabenyamini. 17 Naye alipotazama, akamwona huyo mtu msafiri katika eneo la mji lililokuwa wazi; huyo mzee akamwuliza, Unaenda wapi na umetoka wapi? 18 Akamwambia, Sisi tunapita hapa kutoka Bethlehemu-yuda, tunaenda huko upande wa mbali wa nchi ya vilima vilima ya Efraimu; ndiko nilikotoka nami nilikwenda Bethlehemu-yuda; nami sasa naiendea nyumba ya BWANA, wala hakuna mtu anikaribishaye nyumbani mwake. 19 Walakini nyasi tunazo, na chakula cha hawa punda wetu; mkate pia tunao na divai kwa mimi na huyu kijakazi wako, na kwa huyu kijana aliye pamoja nasi watumishi wako; hapana uhitaji wa kitu chochote. 20 Kisha huyo mzee alisema, Amani Na iwe kwako; nitayakidhi mahitaji yenu yote; bora msikeshe nje. 21 Basi akamkaribisha ndani ya nyumba yake, akawapa punda chakula; nao wakaosha miguu, wakala na kunywa. Hatia ya Gibea 22 Hapo walipokuwa wakifurahisha mioyo yao, tazama, watu wa mji huo, watu mabaradhuli wakaizingira hiyo nyumba pande zote, wakagonga mlango; wakasema na huyo mwenye nyumba, huyo mzee, na kumwambia, Mlete nje mtu yule aliyefika nyumbani kwako, ili tupate kumjua. 23 Naye mwenye nyumba akawatokea hapo nje, na kuwaambia, La, sivyo, ndugu zangu nawasihi msifanye uovu jinsi hii; kwa kuwa mtu huyu ameingia ndani ya nyumba yangu, msifanye upumbavu huu. 24 Tazama, binti yangu yupo hapa, ni mwanamwali, na suria wake huyo mtu; nitawaleta hapa nje sasa nanyi watwezeni, na kuwatenda hayo myaonayo kuwa ni mema; lakini mtu huyu msimtende jambo la upumbavu namna hii. 25 Lakini hao watu hawakumsikia; basi mtu huyo akamshika suria wake, na kumleta nje kwao; nao wakamjua, na kumtenda uovu usiku kucha hadi asubuhi kisha kulipoanza kupambazuka wakamuacha aende zake. 26 Ndipo huyo mwanamke akaja alfajiri, akaanguka chini mlangoni pa nyumba ya mtu yule alimokuwamo bwana wake, hata kulipokucha. 27 Bwana wake akaondoka asubuhi, akaifungua milango ya nyumba, akatoka nje ili aende zake, na tazama, huyo mwanamke suria wake alikuwa ameanguka pale mlangoni pa nyumba, na mikono yake ilikuwa iko pale kizingitini. 28 Akamwambia, Haya inuka, twende zetu; lakini hakumjibu; ndipo akamwinua akamweka juu ya punda; mtu huyo akaondoka, akaenda kwake nyumbani. 29 Naye alipoingia nyumbani mwake, akatwaa kisu, kisha akamshika huyo suria wake, akampasua kiungo kwa kiungo, vipande kumi na viwili akampeleka katika mipaka yote ya Israeli. 30 Basi ikawa, wote waliolishuhudia jambo hilo wakasema, Jambo kama hili halijatendeka wala kuonekana tangu siku hiyo wana wa Israeli walipokwea kutoka katika nchi ya Misri hadi leo; haya, lifikirini, fanyeni shauri, na mliseme. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya