Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

Waamuzi 12 - Swahili Revised Union Version - SRUVDC


Makabila yazozana

1 Kisha watu wa Efraimu walikusanyika na kuvuka hadi Zafoni; wakamwambia Yeftha, Kwa nini ulivuka kwenda kupigana na wana wa Amoni, nawe hukutuita sisi kwenda pamoja nawe? Tutaichoma nyumba yako juu yako.

2 Yeftha akawaambia, Mimi na watu wangu tulikuwa na mzozo mkali na wana wa Amoni; nami hapo nilipowaita ninyi, hamkuniokoa na mikono yao.

3 Nami nilipoona ya kuwa ninyi hamniokoi, niliuhatarisha uhai wangu, na kuvuka ili nipigane na wana wa Amoni, BWANA naye akawatia mkononi mwangu; basi kwa nini ninyi kunijia hivi leo kutaka kupigana nami?

4 Ndipo Yeftha akawakutanisha watu wote wa Gileadi, na kupigana na Efraimu; na hao watu wa Gileadi wakawapiga Efraimu, kwa sababu walisema, Ninyi Wagileadi ni watoro mliotoroka Efraimu, na kukaa kati ya Efraimu na Manase.

5 Nao Wagileadi wakavitwaa vivuko vya Yordani kinyume cha hao Waefraimu; kisha kila mmoja wa watoro walitoroka Efraimu aliposema “Niache nivuke”, hao watu wa Gileadi walimuuliza, “Je! Wewe ni Mwefraimu?” Alijibu, la;

6 ndipo walipomwambia, Haya, tamka sasa neno hili, Shibolethi; naye akasema, Sibolethi; kwa maana hakuweza kufanya midomo yake kutamka neno hilo sawasawa; ndipo wakamshika, na kumwua hapo penye vivuko vya Yordani; basi wakaanguka watu elfu arubaini na mbili wa Efraimu wakati huo.

7 Huyo Yeftha akawa mwamuzi wa Israeli muda wa miaka sita. Ndipo akafa Yeftha, Mgileadi, akazikwa katika miji ya Gileadi mmojawapo.


Ibzani, Eloni na Abdoni

8 Baada ya Yeftha, Ibzani wa Bethlehemu akawa mwamuzi wa Israeli.

9 Alikuwa na watoto thelathini wa kiume; na binti thelathini aliwaoza nje ya ukoo wake, kisha akaleta wanawake thelathini kutoka mahali pengine kwa ajili ya hao wanawe. Akawa mwamuzi wa Israeli muda wa miaka saba.

10 Huyo Ibzani akafa, akazikwa huko Bethlehemu.

11 Baada ya Ibzani, Eloni, Mzabuloni, akawa mwamuzi wa Israeli akawaamua Israeli muda wa miaka kumi.

12 Huyo Eloni, Mzabuloni, akafa, akazikwa katika Aiyaloni katika nchi ya Zabuloni.

13 Baada ya Eloni, Abdoni mwana wa Hileli, Mpirathoni, akawa mwamuzi wa Israeli.

14 Naye alikuwa na wana arubaini, na wajukuu thelathini, waliokuwa wakipanda wanapunda sabini; akawa mwamuzi wa Israeli muda wa miaka minane.

15 Huyo Abdoni mwana wa Hileli, Mpirathoni, akafa, akazikwa huko Pirathoni katika nchi ya Efraimu, katika nchi ya vilima ya Waamaleki.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo