Kitabu hiki si kilichoandikwa kwa uvuvio wa Mungu, na si sehemu ya kanoni ya Kikristo wala Tanaki ya Kiyahudi. Kinaonyeshwa kwa madhumuni ya kihistoria na ya utafiti tu. Tazama maelezo kamili Tobiti 8 - Swahili Revised Union Version - SRUVDCTobia atimua jini 1 Walipokwisha kula wakamwingiza Tobia kwake. 2 Naye alipokuwa akienda, akayakumbuka maneno ya Rafaeli, akayatwaa majivu ya ubani, akavitia juu yake moyo na ini vya samaki, akafukiza moshi. 3 Yule jini alipoisikia harufu, akakimbia hata kukimbilia pande za juu za Misri; huko ndiko malaika alikomfunga. 4 Na wakiisha kuwamo chumbani wote wawili. Tobia akaondoka kitandani, akasema, Ndugu yangu, ondoka, ili pamoja tumwombe Mungu atuhurumie. 5 Ndipo Tobia alipoanza kusema, Ee Mungu wa baba zetu, umehimidiwa; na jina lako takatifu tukufu limehimidiwa milele; mbingu nazo zikuhimidi, pamoja na viumbe vyako vyote. 6 Ndiwe uliyemuumba Adamu, ukampa mkewe Hawa, ili awe msaidizi na tegemeo; na kwao umetoka uzao wote wa wanadamu. Nawe ukasema, Si vema mwanamume akae peke yake; na tumfanyizie msaidizi wa kufanana naye. 7 Na sasa, Ee BWANA, simtwai huyu ndugu yangu kwa ajili ya tamaa, bali katika kweli. Uamuru nirehemiwe, hata niwahi kuona uzee pamoja naye. 8 Sara akasema pamoja naye, Amin. 9 Basi usiku ule wakalala usingizi wote wawili. Ragueli akaondoka mapema, akaenda akachimba kaburi; 10 akasema, Huenda huyu naye atakufa. 11 Ragueli akarudi nyumbani, akamwambia mkewe Edna, 12 Tuma mjakazi mmoja, amtazame kama yu hai. La! Amekufa, na tumzike; wala asijue mtu yeyote. 13 Basi yule mjakazi akaufungua mlango, akaingia; akawakuta wote wawili wamelala. 14 Akatoka akawaambia ya kwamba yu hai. 15 Mara Ragueli akamhimidi Mungu, akasema, Ee Mungu, umehimidiwa kwa sifa zote zilizo safi takatifu; kwa hiyo watakatifu wakuhimidi, pamoja na viumbe vyako vyote, na malaika wako wote; na wateule wako wote wakuhimidi milele. 16 Wewe umehimidiwa kwa kuwa umenifurahisha; wala yale niliyoyahofu hayakunipata; bali umetutendea sawasawa na rehema zako nyingi. 17 Wewe umehimidiwa kwa kuwa umewarehemu wawili hawa, walio watoto pekee wa wazazi wao. Ee BWANA, uwajalie rehema, ili waimalize maisha yao katika afya, pamoja na furaha na rehema. 18 Kisha Ragueli akawaamuru watumishi wake walifukie kaburi. Karamu ya harusi 19 Akaifanya karamu ya arusi yao siku kumi na nne. 20 Na kabla ya kuisha siku za karamu ya arusi, Ragueli akamwapisha Tobia asiondoke hata siku zile kumi na nne za karamu ya arusi zitimie. 21 Baadaye aitwae nusu ya mali zake zote, aende salama kwa baba yake; akasema, Na iliyobaki utapewa nitakapokufa mimi na mke wangu. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya