Kitabu hiki si kilichoandikwa kwa uvuvio wa Mungu, na si sehemu ya kanoni ya Kikristo wala Tanaki ya Kiyahudi. Kinaonyeshwa kwa madhumuni ya kihistoria na ya utafiti tu. Tazama maelezo kamili Tobiti 7 - Swahili Revised Union Version - SRUVDCKuwasili Nyumbani kwa Ragueli 1 Wakafika Ekbatana, wakawasili kwenye nyumba yake Ragueli. Naye Sara akaja kuwapokea, akawasalimu, nao wakamsalimu; kisha akawapeleka ndani ya nyumba. 2 Ragueli akamwambia mkewe Edna. Lo! Kijana huyu amefanana sana na Tobiti aliye jamaa yangu. 3 Ragueli akawauliza, Ndugu, mmetoka wapi? Wakamwambia, Sisi ni wana wa Naftali, tulio wafungwa huko Ninawi. 4 Akawaambia, Je! Mwamfahamu Tobiti, ndugu yetu? Wakasema, Naam, twamfahamu. Akawaambia, Je! Hajambo siku hizi? 5 Wakasema, Yu mzima, tena hajambo, na hapa Tobia akasema, Kweli, ndiye baba yangu. 6 Mara Ragueli akaruka, akambusu, akalia. 7 Akambariki, akamwambia, Wewe u mwana wake mtu mzuri mwema. Lakini aliposikia ya kama Tobiti yu kipofu akahuzunika, akalia, 8 kadhalika na mkewe Edna akalia, na binti yake Sara. Tobia na Sara wafunga ndoa 9 Wakawakaribisha kwa ukunjufu, wakachinja kondoo dume katika kundi, wakawaandalia wingi wa nyama. Kisha Tobia akamwambia Rafaeli, Ndugu yangu Azaria, uziseme zile habari tulizoziongea njiani, ili shauri liishe. 10 Akampasha Ragueli habari. Ragueli akamwambia Tobia, Ule, unywe, na kuchangamka, maana ni wajibu wako umwoe mtoto wangu. Lakini nitakuambia kweli. 11 Nimemwoza mtoto wangu kwa wanaume saba, na kila walipomkaribia wakafa usiku ule ule. Lakini wewe kwa sasa ujifurahishe. Tobia akamwambia, Mimi sionji kitu hapa, hata mtakapofanya agano na kuagana nami. Ragueli akamjibu, Vema, wewe umtwae tangu sasa kama ilivyo desturi, maana wewe u ndugu yake, naye yu wako. Naye Mungu mwenye rehema awafanikisheni katika mambo yote. 12 Akamwita binti yake Sara, akamshika mkono, akampa Tobia ili awe mke wake. Akasema, Tazama umtwae kama iamuruvyo Torati ya Musa, ukampeleke kwa baba yako. Akawabariki. 13 Akamwita mkewe Edna, akatwaa kitabu, akaandika hati akaitia mhuri. 14 Wakaanza kula. 15 Ragueli akamwita mkewe Edna, akamwambia, Mwenzangu, uweke tayari chumba cha pili, ukamlete ndani. 16 Akafanya kama alivyomwagiza, akamleta ndani. Akalia, akayapokea na machozi ya binti yake, akamwambia, Jipe moyo mkuu, mwanangu. BWANA wa mbingu na nchi akupe kibali badala ya hii huzuni yako. Jipe moyo mkuu, mwanangu. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya