Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni

- Matangazo -

Kitabu hiki si kilichoandikwa kwa uvuvio wa Mungu, na si sehemu ya kanoni ya Kikristo wala Tanaki ya Kiyahudi. Kinaonyeshwa kwa madhumuni ya kihistoria na ya utafiti tu. Tazama maelezo kamili

Tobiti 12 - Swahili Revised Union Version - SRUVDC


Malaika wa Rafaeli

1 Halafu yake Tobiti akamwita mwanawe Tobia, akamwambia, Mwanangu, angalia mtu huyu aliyefuatana nawe alipwe mshahara wake, na lazima uongeze.

2 Akamwambia, Baba, si hasara kwangu kumpa nusu ya zile mali nilizozileta.

3 Kwa maana amenirudisha kwako salama; akamponya mke wangu; akaniletea ile fedha; akakuponya na wewe pia.

4 Mzee akasema, Ni haki.

5 Basi akamwita malaika, akamwambia, Afadhali sana wewe utwae nusu ya yote mliyoleta.


Rafaeli atoa maonyo

6 Ndipo alipochukua wote wawili kwa faragha, akawaambia, Mhimidini Mungu, na kumshukuru, na kumwadhimisha; na kumpa shukrani mbele ya wote walio hai kwa mambo yote aliyowatendeeni. Ni vema kumhimidi Mungu na kulikuza jina lake; na kuyatangaza kwa heshima matendo ya Mungu. Basi msilegee katika kumshukuru.

7 Ni vema kuisetiri siri ya mfalme, bali kuyafunua kwa utukufu matendo ya Mungu. Mtende yaliyo mema, na mabaya hayatawapata.

8 Bora ni kusali pamoja na kufunga na kutoa sadaka za haki. Kidogo pamoja na haki ni bora kuliko wingi pasipo na haki. Yafaa kutoa sadaka kuliko kuweka akiba ya dhahabu.

9 Sadaka huokoa na mauti, nazo zitasafishia mbali dhambi zote. Watoao sadaka na kutenda haki watajaa uzima,

10 bali watendao dhambi ni adui za uhai wao wenyewe.


Kujitambulisha kwa Rafaeli

11 Hakika sitawaficheni neno. Nimesema, Ni vema kuisetiri siri ya mfalme, bali kuyafunua kwa utukufu matendo ya Mungu.

12 Basi hapo mliposali, wewe na mkweo Sara mimi niliupeleka ukumbusho wa sala zenu mbele zake Aliye Mtakatifu; na hapo ulipowazika wafu, nilikuwapo pamoja nawe vile vile.

13 Na hapo usipokawia kuondoka na kuacha chakula chako, ili uende kumzika yule mfu, tendo lako jema halikufichwa kwangu; lakini nilikuwapo pamoja nawe.

14 Na sasa Mungu amenituma ili niwaponye, wewe na mkweo Sara.

15 Mimi ndimi Rafaeli, mmojawapo wa malaika watakatifu saba, wapelekao sala za watakatifu, na kuingia mbele za utukufu wake Aliye Mtakatifu.

16 Mara wakafadhaika wote wawili, wakaanguka kifudifudi; kwa maana waliogopa.

17 Akawaambia, Msiogope, amani kwenu, mhimidini Mungu milele.

18 Maana sikuja kwa hisani yangu, bali nilikuja kwa mapenzi ya Mungu wetu. Kwa hiyo mhimidini Yeye milele.

19 Siku hizi zote nilionekana nanyi, lakini sikula wala sikunywa, ila ninyi mliona njozi.

20 Sasa mshukuruni Mungu; kwa kuwa mimi ninapaa kwake aliyenituma; nanyi andikeni katika kitabu mambo yote yaliyotendeka. Nao walipoondoka hawakumwona tena.

21 Wakayakiri matendo makuu ya ajabu ya Mungu, na jinsi Malaika wa BWANA alivyowatokea.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo