Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni

- Matangazo -

Kitabu hiki si kilichoandikwa kwa uvuvio wa Mungu, na si sehemu ya kanoni ya Kikristo wala Tanaki ya Kiyahudi. Kinaonyeshwa kwa madhumuni ya kihistoria na ya utafiti tu. Tazama maelezo kamili

Tobiti 11 - Swahili Revised Union Version - SRUVDC


MACHO YANAONA Kuwasili Nyumbani

1 Wakaendelea mpaka walipoukaribia Ninawi.

2 Hapo Rafaeli alimwambia Tobia, Ndugu yangu, waijua hali uliyomwacha baba yako.

3 Basi sasa tumtangulie mkeo, ili tukaitengeneze nyumba.

4 Nawe uichukue mkononi mwako nyongo ya samaki. Basi wakashika njia mbele, na yule mbwa akafuatana nao.

5 Naye Ana alikuwa amekaa kuyaelekeza macho yake njiani hali akimtazamia mwanawe.

6 Akamwona mbwa akija mbio; akamwambia mumewe, Lo-o-o! Mwanao anakuja, na yule mtu aliyefuatana naye.


Tobiti Aponywa na Kuona Tena

7 Rafaeli akamwambia Tobia, Najua ya kuwa baba yako atafumbua macho yake.

8 Basi umtie mara nyongo machoni; na imchomapo atajifikicha; na vyamba vyeupe vitaambuka; atakuona kwa macho.

9 Lakini Ana alimkimbilia, akamwangukia mwanawe shingoni, akamwambia, Mwanangu! Nimekuona; tangu sasa ni radhi nife. Wakalia wote wawili.

10 Tobiti naye akaondoka kwenda mlangoni, akajikwaa; lakini mwanawe akamkimbilia, akamshika baba yake;

11 akamtia nyongo machoni, akasema, Jipe moyo, baba yangu.

12 Yeye macho yake yalipoanza kuwasha aliyafikicha; navyo vyamba vyeupe vikaambuka katika pembe za macho yake,

13 akamwona mwanawe, akamwangukia shingoni.

14 Akalia, akasema, Ee Mungu, umehimidiwa; na jina lako limehimidiwa milele; na watukuzwe malaika zako watakatifu wote.

15 Kwa maana umenirudi, ukanihurumia; lo-o-o! Namwona mwanangu Tobia. Naye mwanawe aliingia ndani, huku anafurahi, akamwambia baba yake habari za yale mambo makuu yaliyomtukia huko Umedi.

16 Ndipo Tobiti alipotoka mara kwenda kumlaki mkwewe penye lango la Ninawi, akifurahi na kumhimidi Mungu; na wale waliomwona akienda wakastaajabu, kwa sababu amepewa kuona tena.

17 Naye Tobiti akashukuru mbele yao, kwa sababu Mungu amemrehemu, na alipomkaribia mkwewe Sara, alimbariki, akasema, Binti yangu, karibu kwetu. Amehimidiwa Mungu aliyekuleta kwetu, na baba yako na mama yako wamebarikiwa. Ikawa furaha kuu kwa ndugu zake zote waliokuwako Ninawi.

18 Akaja Akiakaro, pamoja na Nasba mwana wa nduguye; akafanywa karamu ya arusi yake Tobia siku saba kwa furaha kuu.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo