Mhubiri 6 - Swahili Revised Union Version - SRUVDCKukatishwa tamaa 1 Kuna baa nililoliona mimi chini ya jua, nalo linawalemea wanadamu kwa uzito; 2 mtu aliyepewa na Mungu mali, ukwasi, na heshima, hata asipungukiwe na kitu chochote kwa nafsi yake, katika yote anayoyatamani lakini Mungu hamwezeshi kula katika hizo; bali mgeni hula. Hayo ndiyo ubatili hasa, nayo ni ugonjwa mbaya. 3 Mtu akizaa watoto mia moja, akaishi miaka mingi, hata siku za maisha yake zikiwa nyingi, lakini nafsi yake haikushiba mema; tena ikiwa, zaidi ya hayo, amekosa maziko; mimi nasema, Heri mimba iliyoharibika kuliko huyo; 4 yaani, hiyo huja katika ubatili, na huenda gizani, nalo jina lake limefunikwa giza; 5 tena, haikuliona jua wala kulifahamu; basi, hii imepata kustarehe kuliko yule; 6 naam, ajapoishi miaka elfu mara mbili, asijiburudishe kwa mema; je! Wote hawaendi mahali pamoja? 7 Juhudi zote za binadamu ni kwa kinywa chake, Lakini hamu yake haitosheleki. 8 Kwa maana mwenye hekima hupata faida gani kuliko mpumbavu? Au maskini ana nini kuliko yeye ajuaye kwenda mbele ya walio hai? 9 Heri kuona kwa macho, Kuliko kutangatanga kwa tamaa. Hayo nayo ni ubatili, na kufukuza upepo. 10 Na awe kitu chochote, aliitwa jina lake zamani za kale, naye amejulikana kuwa ndiye mwanadamu; wala hawezi kabisa kushindana na yeye aliye na uwezo kuliko yeye mwenyewe. 11 Basi, kwa kuwa kuna mambo mengi yaongezayo ubatili, mwanadamu hufaidiwa nini? 12 Kwa maana ni nani ajuaye yaliyo mema ya mwanadamu katika maisha yake, siku zote za maisha yake ya ubatili, anayoishi kama kivuli? Kwa maana ni nani awezaye kumweleza mwanadamu mambo yatakayofuata baada yake chini ya jua? |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya