Mhubiri 5 - Swahili Revised Union Version - SRUVDCUchaji, unyenyekevu na kuridhika 1 Jitunze mguu wako uendapo nyumbani kwa Mungu; Maana ni heri kukaribia ili usikie, Kuliko kutoa kafara ya wapumbavu; Ambao hawajui kuwa wafanya mabaya. 2 Usiseme maneno ya ujinga kwa kinywa chako, wala moyo wako usiwe na haraka kunena mbele za Mungu; kwa maana, Mungu yuko mbinguni, na wewe upo chini, Kwa hiyo maneno yako na yawe machache. 3 Kwa maana ndoto huja kwa sababu ya shughuli nyingi; na sauti ya mpumbavu kwa njia ya wingi wa maneno. 4 Wewe ukimwekea Mungu nadhiri, usikawie kuiondoa; kwa kuwa yeye hawi radhi na wapumbavu; basi, uiondoe hiyo uliyoiweka nadhiri. 5 Ni afadhali usiweke nadhiri, Kuliko kuiweka usiiondoe. 6 Usikiache kinywa chako kuukosesha mwili wako; wala usiseme mbele ya huyo malaika ya kwamba hukukusudia; kwa nini Mungu akasirishwe na maneno yako, na kuiharibu kazi ya mikono yako? 7 Maana ndivyo ilivyo katika habari za wingi wa ndoto, na ubatili, na maneno mengi; walakini wewe umche Mungu. 8 Ujapokuwa unaona maskini kuonewa, na hukumu na haki kuondolewa kwa jeuri katika jimbo, usilistaajabie jambo hilo; kwa sababu, Aliye Juu kuliko walio juu huangalia; Tena wako walio juu kupita hao. 9 Lakini, pamoja na hayo, manufaa ya nchi kwa kila njia ni mfalme anayejibidiisha kwa ajili ya shamba. 10 Apendaye fedha hatashiba fedha, Wala apendaye wingi hatashiba nyongeza. Hayo pia ni ubatili. 11 Mali yakiongezeka, hao walao nao wanaongezeka na mwenyewe hufaidiwa nini, ila kuyatazama kwa macho yake tu? 12 Usingizi wake kibarua ni mtamu, awe amekula kidogo, au awe amekula kingi; lakini kushiba kwake tajiri hakumwachi kulala usingizi. 13 Kuna balaa mbaya sana niliyoiona chini ya jua, nayo ni hii, mali alizoziweka mwenyewe kwa kujinyima; 14 na mali hizo zimepotea kwa bahati mbaya; naye akiwa amezaa mwana, hamna kitu mkononi mwake. 15 Alivyotoka tumboni mwa mamaye, atakwenda tena tuputupu kama alivyokuja; asichume kitu chochote kwa ajili ya kazi yake, hata akichukue mkononi mwake. 16 Hiyo ndiyo balaa mbaya sana, ya kwamba kama vile alivyokuja, vivyo hivyo atakwenda zake; naye amefaidiwa nini mwenye kujitaabisha kwa ajili ya upepo? 17 Siku zake zote hula gizani, mwenye fadhaa nyingi, mwenye ugonjwa na uchungu. 18 Tazama, mimi niliyoyaona kuwa ndiyo mema na ya kufaa, ni mtu kula na kunywa, na kujiburudisha kwa mema katika kazi yake yote anayoifanya chini ya jua, siku zote za maisha yake alizopewa na Mungu; maana hilo ndilo fungu lake. 19 Tena, kwa habari za kila mwanadamu, ambaye Mungu amempa mali na ukwasi, akamwezesha kula katika hizo, na kuipokea sehemu yake, na kuifurahia amali yake; hiyo ndiyo karama ya Mungu. 20 Kwa kuwa mtu hatazikumbuka mno siku za maisha yake; kwa sababu Mungu humtakabali katika furaha ya moyo wake. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya