Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni

- Matangazo -

Matendo 28 - Swahili Revised Union Version - SRUVDC


Paulo akiwa katika kisiwa cha Malta

1 Tulipokwisha kuokoka, ndipo tulipojua ya kuwa kisiwa kile chaitwa Melita.

2 Wenyeji wakatufanyia fadhili zisizokuwa za kawaida. Kwa maana waliwasha moto, wakatukaribisha sote, kwa sababu ya mvua iliyonyesha na kwa sababu ya baridi.

3 Paulo alipokuwa amekusanya mzigo wa kuni, na kuuweka motoni, nyoka akatoka kwa ajili ya ule moto akamzongazonga mkononi.

4 Wenyeji walipomwona yule nyoka akilewalewa mkononi, wakaambiana, Hakosi mtu huyu ni mwuaji; ambaye ijapokuwa ameokoka katika bahari haki haimwachi kuishi.

5 Lakini yeye akamtukusia motoni asipate madhara.

6 Wao wakadhani ya kuwa atavimba au kuanguka chini kwa kufa ghafla; na wakiisha kumwangalia sana, na kuona kwamba halimpati dhara lolote, wakageuka, wakasema kwamba yeye ni mungu.

7 Karibu na mahali pale palikuwa na mashamba ya mkuu wa kisiwa, jina lake Publio; mtu huyu akatukaribisha kwa moyo wa urafiki, akatufanya wageni wake kwa muda wa siku tatu.

8 Ikawa babake Publio alikuwa akiugua homa na kuhara damu. Paulo akaingia kwake, akaomba, akaweka mikono yake juu yake, na kumponya.

9 Yalipokwisha kutendeka hayo wengine waliokuwa na magonjwa katika kisiwa wakaja wakaponywa;

10 nao wakatuheshimu kwa heshima nyingi; basi tulipoabiri wakatupakilia vitu vile tulivyokuwa na haja navyo.


Paulo afika Rumi

11 Baada ya miezi mitatu tukasafiri katika merikebu ya Aleksandria iliyokuwa imekaa pale kisiwani wakati wa baridi; na alama yake ni Ndugu Pacha.

12 Tukafika Sirakusa, tukakaa siku tatu.

13 Kutoka huko tukazunguka tukafikia Regio; baada ya siku moja upepo wa kusi ukavuma, na siku ya pili tukawasili Puteoli.

14 Huko tukakuta ndugu, wakatusihi tukae nao siku saba; na hivi ndivyo tulifika Rumi.

15 Na kutoka huko ndugu, waliposikia habari zetu, wakaja kutulaki mpaka Soko la Apio na Mikahawa Mitatu. Paulo alipowaona alimshukuru Mungu, akachangamka.

16 Tulipoingia Rumi Paulo alipewa ruhusa kukaa kwake mwenyewe pamoja na askari aliyemlinda.


Paulo nawakuu wa Wayahudi wakiwa Rumi

17 Ikawa baada ya siku tatu akawaita wakuu wa Wayahudi wakutane, na walipokutanika akawaambia, Ndugu zangu, ningawa sikufanya neno kinyume cha watu wetu wala neno lililopingamana na desturi za baba zetu, nilitiwa katika mikono ya Warumi, nikiwa nimefungwa, tokea Yerusalemu.

18 Na hao walipokwisha kunihoji walitaka kunifungua, kwa maana hapakuwa na sababu yoyote kwangu ya kuuawa.

19 Lakini Wayahudi walipotoa hoja juu ya shauri hili nilishurutishwa kutaka rufani kwa Kaisari. Si kwamba nilikuwa na neno la kuwashitaki watu wa taifa langu.

20 Basi kwa ajili ya hayo, nimewaita mje kunitazama na kusema nami; kwa maana nimefungwa kwa mnyororo huu kwa ajili ya tumaini la Israeli.

21 Wale wakamwambia, Sisi hatukupata nyaraka zenye habari zako kutoka Yudea, wala hapana ndugu hata mmoja aliyefika hapa na kutupasha habari, au kunena neno baya juu yako.

22 Lakini tunataka kusikia kwako uonavyo wewe; kwa maana kuhusu madhehebu hiyo imejulikana kwetu kwamba inanenwa vibaya kila mahali.


Paulo ahubiri Rumi

23 Wakiisha kupanga naye siku, wakamjia katika nyumba aliyokaa, watu wengi sana, akawaeleza kwa taratibu na kuushuhudia ufalme wa Mungu, akiwaonya mambo yake Yesu, kwa maneno ya Sheria ya Musa na ya manabii, tangu asubuhi hadi jioni.

24 Wengine waliamini yale yaliyonenwa, wengine hawakuyaamini.

25 Na walipokuwa hawapatani wao kwa wao, wakaenda zao, Paulo alipokwisha kusema neno hili moja, ya kwamba, Roho Mtakatifu alinena vema na baba zetu, kwa kinywa cha nabii Isaya,

26 akisema, Nenda kwa watu hawa, ukawaambie, Kusikia, mtasikia wala hamtafahamu; Na kuona, mtaona wala hamtatambua;

27 Kwa maana mioyo ya watu hawa imepumbaa, Na masikio yao ni mazito ya kusikia, Na macho yao wameyafumba; Wasije wakaona kwa macho yao, Na kusikia kwa masikio yao, Na kufahamu kwa mioyo yao, Na kubadili nia zao, nikawaponya.

28 Basi ijulikane kwenu ya kwamba wokovu huu wa Mungu umepelekwa kwa Mataifa, nao watasikia! [

29 Alipokwisha kusema hayo, Wayahudi wakaenda zao, wakiulizana mengi wao kwa wao.]

30 Akakaa muda wa miaka miwili kamili katika nyumba yake aliyokuwa ameipanga, akawakaribisha watu wote waliokuwa wakimwendea,

31 akihubiri habari za ufalme wa Mungu, na kuyafundisha mambo ya Bwana Yesu Kristo, kwa ujasiri mwingi, asikatazwe na mtu.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo