Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

Matendo 20 - Swahili Revised Union Version - SRUVDC


Paulo aenda Makedonia na Ugiriki

1 Ghasia ile ilipokoma, Paulo akatuma kuwaita wanafunzi akawaonya, akaagana nao, kisha akaondoka aende zake mpaka Makedonia.

2 Naye akiisha kupita pande zile na kuwafariji kwa maneno mengi, akafika Ugiriki.

3 Alipokwisha kukaa huko miezi mitatu, na Wayahudi kumfanyia vitimvi, alipotaka kwenda Shamu kwa njia ya bahari; basi akaazimu kurejea kwa njia ya Makedonia.

4 Watu hawa wakafuatana naye, Sopatro Mberea, mwana wa Piro, na Aristarko na Sekundo, watu wa Thesalonike; na Gayo mtu wa Derbe, na Timotheo; na Tikiko na Trofimo watu wa Asia.

5 Ila watu hao wamekwisha kutangulia wakamngojea Troa.

6 Sisi tukatweka baada ya siku za mikate isiyotiwa chachu, tukatoka Filipi, tukawafikia Troa, baada ya safari ya siku tano, tukakaa huko siku saba.


Ziara ya mwisho ya Paulo huko Troa

7 Siku ya kwanza ya juma, tulipokuwa tumekutana ili kumega mkate, Paulo akawahutubia, maana aliazimia kusafiri siku iliyofuata, naye akafululiza maneno yake hadi usiku wa manane.

8 Palikuwa na taa nyingi katika ghorofa lile tulipokuwa tumekusanyika.

9 Kijana mmoja, jina lake Eutiko, alikuwa ameketi dirishani, akalemewa na usingizi sana; hata Paulo alipoendelea sana kuhubiri, akazidiwa na usingizi wake akaanguka toka ghorofa ya tatu; akainuliwa amekwisha kufa.

10 Paulo akashuka, akamwangukia, akamkumbatia, akasema, Msifanye ghasia, maana uzima wake ungalimo ndani yake.

11 Akapanda juu tena, akamega mkate, akala, akazidi kuongea nao hadi alfajiri, ndipo akaenda zake.

12 Wakamleta yule kijana, akiwa mzima, wakafarijika faraja kubwa sana.


Safari ya kutoka Troa hadi Mileto

13 Lakini sisi tukatangulia kwenda merikebuni, tukaabiri kwenda Aso, tukikusudia kumpakia Paulo huko; kwa maana ndivyo alivyoagiza, yeye mwenyewe aliazimia kwenda kwa miguu.

14 Alipotufikia huko Aso, tukampakia, kisha tukafika Mitilene.

15 Tukatweka kutoka huko, na siku ya pili tukafika mahali panapokabili Kio; siku ya tatu tukawasili Samo, tukakaa Trogilio, siku ya nne tukafika Mileto.

16 Kwa sababu Paulo alikusudia kusafiri pasipo kupitia Efeso merikebuni, asije akakawia katika Asia; kwa maana alikuwa na haraka, akitaka kuwahi Yerusalemu siku ya Pentekoste, kama ikiwezekana.


Paulo asema na viongozi wa Efeso

17 Toka Mileto Paulo akatuma watu kwenda Efeso, akawaita wazee wa kanisa.

18 Walipofika kwake, akawaambia, Ninyi wenyewe mnajua tangu siku ya kwanza nilipokanyaga hapa Asia, jinsi nilivyokuwa kwenu wakati wote,

19 nikimtumikia Bwana kwa unyenyekevu wote, na kwa machozi, na majaribu yaliyonipata kutokana na njama za Wayahudi;

20 ya kuwa sikujiepusha katika kuwatangazia neno lolote liwezalo kuwafaa bali niliwafundisha waziwazi, na nyumba kwa nyumba,

21 nikiwashuhudia Wayahudi na Wagiriki wamtubie Mungu, na kumwamini Bwana wetu Yesu Kristo.

22 Basi sasa, angalieni, nashika njia kwenda Yerusalemu nikiwa nimefungwa rohoni, nisiyajue mambo yatakayonikuta huko;

23 isipokuwa Roho Mtakatifu mji kwa mji hunishuhudia akisema, ya kwamba vifungo na dhiki vyaningoja.

24 Lakini siyahesabu maisha yangu kuwa kitu cha thamani kwangu kama kuumaliza mwendo wangu na huduma ile niliyopokea kwa Bwana Yesu, kuishuhudia Habari Njema ya neema ya Mungu.

25 Na sasa, tazameni, mimi najua ya kuwa ninyi nyote niliowahubiria ufalme wa Mungu, nikienda huku na huko, hamtaniona uso tena.

26 Kwa hiyo nawashuhudia wote siku hii ya leo, ya kuwa mimi sina hatia kwa damu ya mtu awaye yote.

27 Kwa maana sikujiepusha na kuwahubiria habari ya kusudi lote la Mungu.

28 Jitunzeni nafsi zenu, na lile kundi lote nalo, ambalo Roho Mtakatifu amewaweka ninyi kuwa waangalizi ndani yake, mpate kulilisha kanisa lake Mungu, alilolinunua kwa damu yake mwenyewe.

29 Najua mimi ya kuwa baada ya kuondoka kwangu mbwamwitu wakali wataingia kwenu, wasilihurumie kundi;

30 tena katika ninyi wenyewe watainuka watu wakisema mapotovu, wawavute hao wanafunzi wawafuatie wao.

31 Kwa hiyo kesheni, mkikumbuka ya kwamba miaka mitatu, usiku na mchana, sikuacha kumwonya kila mtu kwa machozi.

32 Basi, sasa nawaweka katika mikono ya Mungu, na kwa neno la neema yake, ambalo laweza kuwajenga na kuwapa urithi pamoja nao wote waliotakaswa.

33 Sikutamani fedha wala dhahabu, wala mavazi ya mtu.

34 Ninyi wenyewe mnajua ya kuwa mikono yangu hii imetumika kwa mahitaji yangu na ya wale waliokuwa pamoja nami.

35 Katika mambo yote nimewaonesha ya kuwa kwa kushika kazi hivi imewapasa kuwasaidia wanyonge, na kuyakumbuka maneno ya Bwana Yesu, jinsi alivyosema mwenyewe, Ni heri kutoa kuliko kupokea.

36 Alipokwisha kunena haya akapiga magoti, akaomba pamoja nao wote.

37 Wakalia sana wote, wakamwangukia Paulo shingoni, wakambusubusu,

38 wakihuzunika zaidi kwa sababu ya neno lile alilosema, ya kwamba hawatamwona uso tena. Wakamsindikiza hata merikebuni.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo