Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni

- Matangazo -

Kutoka 38 - Swahili Revised Union Version - SRUVDC


Kutengeneza madhabahu ya sadaka za kuchomwa

1 Kisha akafanya hiyo madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, ya mti wa mshita urefu wake ulikuwa dhiraa tano, na upana wake ulikuwa dhiraa tano, ilikuwa mraba; na kwenda juu kwake kulikuwa dhiraa tatu.

2 Naye akazifanya pembe zake katika ncha zake nne; hizo pembe zilikuwa za kitu kimoja nayo; naye akaifunika shaba.

3 Kisha akafanya vyombo vyote vya madhabahu, yaani sufuria zake, na majembe yake, na mabakuli yake, na uma zake, na meko yake; vyombo vyake vyote akavifanya vya shaba.

4 Naye akaifanyia madhabahu wavu wa shaba, akautia chini ya ukingo kuizunguka pande zote, ukawa katikati ya hiyo madhabahu.

5 Naye akasubu vikuku vinne kwa kutiwa katika pembe nne za huo wavu wa shaba, viwe mahali pa kutia ile miti ya kuichukulia.

6 Naye akaifanya hiyo miti kwa mti wa mshita na kuifunika shaba.

7 Naye akaitia ile miti katika vile vikuku vilivyokuwa katika mbavu za hiyo madhabahu, ili kuichukua; akaifanya yenye mvungu ndani, kwa zile mbao.

8 Kisha akafanya hilo birika la shaba, na kitako chake cha shaba; shaba hiyo ilikuwa ni ya vioo vya wanawake wenye kutumika, waliokuwa wakitumika mlangoni mwa hema ya kukutania.


Kutengeneza behewa la sanduku la Agano

9 Naye akafanya ua; upande wa kusini kwa kuelekea kusini, chandarua cha ua kilikuwa cha nguo ya kitani nzuri ya kusokotwa, kiasi cha dhiraa mia moja;

10 nguzo zake zilikuwa ishirini, na vitako vyake vilikuwa ishirini, vilikuwa vya shaba; kulabu za nguzo na vitanzi vyake vilikuwa vya fedha.

11 Upande wa kaskazini ulikuwa ni dhiraa mia moja vivyo hivyo, nguzo zake ishirini na vitako vyake ishirini, vilikuwa ni vya shaba; kulabu za nguzo na vitanzi vyake vilikuwa vya fedha.

12 Upande wa magharibi mlikuwa na chandarua ya dhiraa hamsini, nguzo zake zilikuwa ni kumi, na vitako vyake kumi; kulabu za hizo nguzo na vitanzi vyake vilikuwa vya fedha.

13 Upande wa mashariki kuelekea mashariki dhiraa hamsini.

14 Chandarua ya upande mmoja wa lango ilikuwa dhiraa kumi na tano urefu wake; na nguzo zake tatu, na vitako vyake vitatu;

15 ni vivyo hivyo upande wa pili; upande huu na huu langoni mwa ua mlikuwa na chandarua ya dhiraa kumi na tano urefu wake; nguzo zake zilikuwa ni tatu, na vitako vyake vitatu.

16 Vyandarua vya nguo zote za ule ua vilivyouzunguka pande zote vilikuwa ni vya kitani nzuri iliyosokotwa.

17 Na vitako vya zile nguzo vilikuwa vya shaba; kulabu za hizo nguzo na vitanzi vyake vilikuwa vya fedha; na vichwa vya zile nguzo vilikuwa ni vya fedha; na nguzo zote za huo ua ziliungwa kwa vitanzi vya fedha.

18 Na hilo pazia la lango la ua, lilikuwa ni kazi ya mwenye kutia taraza, lilikuwa la nyuzi za rangi ya buluu, zambarau na nyekundu, na kitani nzuri ya kusokotwa; lilikuwa na urefu wa dhiraa ishirini, na kutukuka kwake katika huo upana wake kulikuwa dhiraa tano, kupatana na ile chandarua ya ua.

19 Na nguzo zake zilikuwa nne, na vitako vyake vinne, vilikuwa vya shaba; kulabu zake zilikuwa za fedha, na vichwa vyake na vitanzi vyake vilikuwa vya fedha.

20 Na vigingi vyote vya maskani, na vya ua ulioizunguka pande zote vilikuwa vya shaba.


Vyombo vya hema ya kukutania

21 Jumla ya vile vyombo vilivyofanywa kwa ajili ya hiyo maskani, hiyo maskani ya ushuhuda ni hii, kama vilivyohesabiwa, kama maagizo ya Musa yalivyokuwa, kwa ajili ya utumishi wa Walawi kwa mkono wa Ithamari, mwana wa Haruni, kuhani.

22 Na Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, wa kabila la Yuda, akafanya yote BWANA aliyomwagiza Musa.

23 Na pamoja naye alikuwa na Oholiabu, mwana wa Ahisamaki, wa kabila la Dani, aliyekuwa fundi wa kuchora nakshi, mfanyaji wa kazi mwerevu, naye alikuwa mwenye kutia taraza za nyuzi za rangi ya samawati, na za rangi ya zambarau, na nyekundu, na kitani nzuri.

24 Dhahabu yote iliyotumiwa kwa ajili ya hiyo kazi, katika kazi hiyo yote ya mahali patakatifu, hiyo dhahabu ya matoleo, ilikuwa ni talanta ishirini na tisa, na shekeli mia saba na thelathini, kwa kadiri ya shekeli ya mahali patakatifu.

25 Na fedha ya hao waliohesabiwa, watu wa huo mkutano ilikuwa talanta mia moja, na shekeli elfu moja na mia saba na sabini na tano kwa kadiri ya shekeli ya mahali patakatifu;

26 kichwa beka, maana, nusu shekeli, kwa kadiri ya shekeli ya mahali patakatifu, kwa ajili ya kila mtu aliyepita kwa wale waliohesabiwa, aliyekuwa wa umri wa miaka ishirini au zaidi, kwa ajili ya wanaume elfu mia sita na tatu mia tano na hamsini (603,550).

27 Na hizo talanta mia moja za fedha zilikuwa kwa kutengenezea vile vitako vya mahali patakatifu na vitako vya hilo pazia; vitako mia moja kwa hizo talanta mia moja, talanta moja kitako kimoja.

28 Na kwa hizo shekeli elfu moja na mia saba, na sabini na tano, akafanya vifungo vya hizo nguzo, na kuvifunika fedha vile vichwa vyake, na kufanya vitanzi vyake.

29 Na hiyo shaba iliyoletwa ilikuwa ni talanta sabini, na shekeli elfu mbili na mia nne.

30 Naye akafanya ya hiyo shaba vitako kwa ajili ya lango la hema ya kukutania, na hiyo madhabahu ya shaba, na ule wavu wa shaba kwa ajili yake na vyombo vyote vya hiyo madhabahu,

31 na vitako vya ua kuuzunguka pande zote, na vitako vya lango la huo ua, na vigingi vyote vya maskani, na vigingi vyote vya huo ua uliozunguka pande zote.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo