Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

Kutoka 19 - Swahili Revised Union Version - SRUVDC


Wana wa Israeli waufikia mlima wa Sinai

1 Mwezi wa tatu baada ya Waisraeli kutoka katika nchi ya Misri, siku iyo hiyo wakafika katika jangwa la Sinai.

2 Nao walipokuwa wameondoka Refidimu na kufika jangwa la Sinai, wakatua katika lile jangwa; Israeli wakapiga kambi huko wakiukabili mlima.

3 Musa akapanda kwa Mungu, na BWANA akamwita kutoka mlimani ule, akisema, Utawaambia nyumba ya Yakobo, na kuwaarifu wana wa Israeli, maneno haya;

4 Mmeona jinsi nilivyowatendea Wamisri, na jinsi nilivyowachukua ninyi juu ya mbawa za tai, nikawaleta ninyi kwangu mimi.

5 Sasa basi ikiwa mtaitii sauti yangu kweli kweli, na kulishika agano langu, hapo ndipo mtakapokuwa tunu kwangu kuliko makabila yote ya watu; maana dunia yote pia ni mali yangu,

6 nanyi mtakuwa kwangu ufalme wa makuhani, na taifa takatifu. Hayo ndiyo maneno utakayowaambia wana wa Israeli.

7 Musa akaenda akawaita wazee wa watu, akawafunulia maneno hayo yote, BWANA aliyokuwa amemwagiza.

8 Watu wote wakaitika pamoja wakisema, Hayo yote aliyoyasema BWANA tutayatenda. Naye Musa akamwambia BWANA maneno ya hao watu.


Watu watakaswa

9 BWANA akamwambia Musa, Tazama, mimi naja kwako katika wingu zito ili watu hawa wasikie nitakaposema nawe, nao wapate kukuamini nawe hata milele. Musa akamwambia BWANA hayo maneno ya watu.

10 BWANA akamwambia Musa, Nenda kwa watu hawa, ukawatakase leo na kesho, wakazifue nguo zao,

11 wawe tayari kwa siku ya tatu; maana siku ya tatu BWANA atashuka katika mlima wa Sinai machoni pa watu hawa wote.

12 Nawe utawawekea mipaka watu hawa pande zote, ukisema, Jihadharini, msipande mlima huu, wala msiuguse, hata pambizo zake; kila mtu atakayeugusa mlima huu, bila shaka atauawa.

13 Mkono wa mtu yeyote usimguse mtu huyo, ila hakika yake atapigwa kwa mawe, au kupigwa kwa mkuki; awe ni mnyama au awe ni mwanadamu, hataishi. Hapo parapanda itakapotoa sauti kwa kufululiza ndipo watakapoukaribia mlima.

14 Musa akateremka mlimani akawaendea watu akawatakasa, nao wakafua nguo zao.

15 Akawaambia watu; Muwe tayari siku ya tatu; msimkaribie mwanamke.

16 Ikawa siku ya tatu, wakati wa asubuhi, palikuwa na ngurumo na umeme, na wingu zito juu ya mlima, na sauti ya baragumu iliyolia sana. Watu wote waliokuwa kituoni wakatetemeka.

17 Musa akawatoa hao watu katika kituo, akawaleta ili waonane na Mungu; wakasimama pande za chini za kile kilima.

18 Mlima wa Sinai wote pia ukatoa moshi, kwa sababu BWANA alishuka katika moto; na ule moshi wake ukapanda juu kama moshi wa tanuri, mlima wote ukatetemeka sana.

19 Na hapo sauti ya baragumu ilipozidi kulia sana, Musa akanena, naye Mungu akamwitikia kwa sauti.

20 BWANA akaushukia mlima, juu ya kilele cha mlima; BWANA akamwita Musa aende hata kilele cha mlima; Musa akapanda juu.

21 Ndipo BWANA akamwambia Musa, Shuka chini, uwaonye watu wasije wakafanya njia kuja kwa BWANA kutazama, kisha wengi miongoni mwao wakaangamia.

22 Makuhani nao, wamkaribiao BWANA, na wajitakase, BWANA asije akawakasirikia.

23 Musa akamwambia BWANA, Watu hawa hawawezi kuukaribia mlima wa Sinai; kwa kuwa wewe ulituusia, ukisema, Wekeni mipaka kandokando ya mlima, na kuutenga.

24 BWANA akamwambia, Nenda, ushuke wewe; nawe utakwea, wewe, na Haruni pamoja nawe; lakini wale makuhani na watu wasipenye kumkaribia BWANA, asije yeye akawafurikia juu yao.

25 Basi Musa akawateremkia hao watu na kuwaambia hayo.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo