Kumbukumbu la Torati 5 - Swahili Revised Union Version - SRUVDCAmri kumi 1 Musa akawaita Israeli wote, akawaambia, Enyi Israeli, zisikieni amri na hukumu nisemazo masikioni mwenu leo, mpate kujifunza na kuzizingatia. 2 BWANA, Mungu wetu, alifanya agano nasi katika Horebu. 3 BWANA hakufanya agano hili na baba zetu, bali na sisi, yaani, sisi sote tuliopo hapa, tu hai. 4 BWANA alisema nanyi uso kwa uso mlimani, kutoka kati ya moto; 5 (nami wakati ule nikiwa nimesimama kati ya BWANA na ninyi, ili kuwaonesha neno la BWANA; maana, mliogopa kwa sababu ya ule moto, wala hamkupanda mlimani); naye akasema, 6 Mimi ni BWANA, Mungu wako, niliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa. 7 Usiwe na miungu mingine ila mimi. 8 Usijifanyie sanamu ya kuchonga, mfano wa kitu chochote kilicho juu mbinguni, au kilicho chini duniani, au kilicho majini chini ya nchi. 9 Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi BWANA, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu, nawapatiliza wana uovu wa baba zao; hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao, 10 nami nawarehemu maelfu wanipendao, na kuzishika amri zangu. 11 Usilitaje bure Jina la BWANA, Mungu wako; maana BWANA hatamhesabia kuwa hana hatia, mtu alitajaye jina lake bure. 12 Ishike siku ya Sabato uitakase, kama BWANA, Mungu wako, alivyokuamuru. 13 Siku sita fanya kazi, utende mambo yako yote; 14 lakini siku ya saba ni Sabato ya BWANA, Mungu wako; siku hiyo usifanye kazi yoyote, wewe, wala mwanao, wala binti yako, wala mtumwa wako, wala mjakazi wako, wala ng'ombe wako, wala punda wako, wala mnyama wako yeyote, wala mgeni aliye ndani ya malango yako, ili mtumwa wako na mjakazi wako wapumzike vile vile kama wewe. 15 Nawe utakumbuka ya kuwa wewe ulikuwa mtumwa katika nchi ya Misri, na ya kuwa BWANA, Mungu wako, alikutoa huko kwa mkono wenye nguvu, na mkono ulionyoshwa; kwa sababu hiyo BWANA, Mungu wako, alikuamuru uishike sabato. 16 Waheshimu baba yako na mama yako; kama BWANA, Mungu wako, alivyokuamuru, siku zako zipate kuzidi, nawe upate kufanikiwa katika nchi upewayo na BWANA, Mungu wako. 17 Usiue. 18 Wala usizini. 19 Wala usiibe. 20 Wala usimshuhudie jirani yako uongo. 21 Wala usimtamani mke wa jirani yako; wala usiitamani nyumba ya jirani yako, wala shamba lake, wala mtumwa wake, wala mjakazi wake, wala ng'ombe wake, wala punda wake, wala kitu chochote alicho nacho jirani yako. Musa mwakilishi wa mapenzi ya Mungu 22 Haya ndiyo maneno ambayo BWANA aliwaambia mkutano wenu wote mlimani kwa sauti kuu toka kati ya moto, na wingu, na giza kuu; wala hakuongeza neno. Akayaandika juu ya mbao mbili za mawe, akanipa. 23 Ikawa, mlipoisikia sauti ile toka kati ya giza, na wakati uo huo mlima ule ulikuwa ukiwaka moto, basi, mlinikaribia, naam, wakuu wote wa makabila yenu, na wazee wenu, 24 mkasema, Tazama, BWANA, Mungu wetu, ametuonesha utukufu wake, na ukuu wake, nasi tunasikia sauti yake toka kati ya moto; mmeona leo ya kuwa Mungu husema na mwanadamu, naye akaishi. 25 Sasa basi, mbona tufe? Maana moto huu mkubwa utatuteketeza; tukiisikia tena sauti ya BWANA, Mungu wetu, tutakufa. 26 Maana katika watu wote ni nani aliyeisikia sauti ya Mungu aliye hai, akisema toka kati ya moto, kama vile sisi, asife? 27 Nenda karibu wewe, ukasikie yote atakayoyasema BWANA, Mungu wetu; ukatuambie yote atakayokuambia BWANA, Mungu wetu; nasi tutayasikia na kuyatenda. 28 Naye BWANA akasikia sauti ya maneno yenu mliyoniambia; BWANA akaniambia, Nimesikia sauti ya maneno ya watu hawa waliyokuambia; wamesema vema yote waliyosema. 29 Laiti wangekuwa na moyo kama huu ndani yao sikuzote, wa kunicha, na kushika amri zangu zote sikuzote, wapate kufanikiwa wao na watoto wao milele! 30 Enda uwaambie, Rudini hemani mwenu. 31 Lakini wewe, simama hapa karibu nami, nami nitasema nawe sheria zote, na amri na hukumu, utakazowafunza, wapate kuzifanya katika nchi niwapayo kuimiliki. 32 Tunzeni basi, mtende kama mlivyoamriwa na BWANA, Mungu wenu; msikengeuke kwa mkono wa kulia wala wa kushoto. 33 Endeni njia yote aliyowaagiza BWANA, Mungu wenu, mpate kuwa hai, na kufanikiwa, mkafanye siku zenu kuwa nyingi katika nchi mtakayoimiliki. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya