Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

Kumbukumbu la Torati 34 - Swahili Revised Union Version - SRUVDC


Kifo cha Musa na kuzikwa kwake katika Moabu

1 Musa akapanda kutoka uwanda wa Moabu mpaka mlima Nebo, hata kilele cha Pisga kukabili Yeriko. BWANA akamwonesha nchi yote ya Gileadi hata Dani;

2 na Naftali yote, na nchi ya Efraimu na Manase, na nchi yote ya Yuda, mpaka bahari ya magharibi;

3 na Negebu, na uwanja wa bonde la Yeriko, mji wa mitende, hata mpaka Soari.

4 BWANA akamwambia, Hii ndiyo nchi niliyowaapia Abrahamu, na Isaka, na Yakobo, nikisema, Nitawapa wazao wako. Basi nimekuonesha kwa macho yako, lakini hutavuka huko.

5 Basi Musa, mtumishi wa BWANA, akafa huko, katika nchi ya Moabu, kwa neno la BWANA.

6 Akamzika bondeni, katika nchi ya Moabu, kukabili Beth-peori; lakini hapana mtu ajuaye kaburi lake hata leo.

7 Musa alikuwa mtu wa miaka mia moja na ishirini alipokufa; jicho lake halikupofuka, wala nguvu za mwili wake hazikupunguka.

8 Wana wa Israeli wakamwombolezea Musa katika uwanda wa Moabu siku thelathini; basi siku za maombolezo ya matanga ya Musa zikaisha.

9 Na Yoshua, mwana wa Nuni, alikuwa amejaa roho ya hekima; maana Musa alikuwa amemwekea mikono yake juu yake; wana wa Israeli wakamsikiliza, wakafanya kama BWANA alivyomwamuru Musa.

10 Wala hajainuka tena katika Israeli nabii kama Musa, ambaye BWANA alimjua uso kwa uso;

11 katika ishara zote na maajabu yote, ambayo BWANA alimtuma kuyatenda katika nchi ya Misri, kwa Farao, na kwa watumishi wake wote, na kwa nchi yake yote;

12 na katika ule mkono wa nguvu wote, tena katika ule utisho mkuu wote, alioutenda Musa machoni pa Israeli wote.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo