Kumbukumbu la Torati 1 - Swahili Revised Union Version - SRUVDCKumbukumbu ya yaliyotokea Horebu 1 Haya ndiyo maneno Musa aliyowaambia Israeli wote ng'ambo ya Yordani nyikani, katika Araba lililoelekea Sufu, kati ya Parani, na Tofeli, na Labani, na Hazerothi, na Dizahabu. 2 Ni mwendo wa siku kumi na moja kutoka Horebu kwa njia ya mlima wa Seiri mpaka Kadesh-barnea. 3 Ikawa mwaka wa arubaini, mwezi wa kumi na moja, siku ya kwanza ya mwezi, Musa akawaambia wana wa Israeli kama yote aliyopewa na BWANA ya kuwaamuru; 4 alipokwisha kumpiga Sihoni mfalme wa Waamori, aliyekuwa akikaa Heshboni, na Ogu mfalme wa Bashani, aliyekuwa akikaa Ashtarothi iliyo katika Edrei; 5 ni ng'ambo ya Yordani katika nchi ya Moabu, alipoanza Musa kufunua torati hii, akisema, 6 BWANA, Mungu wetu, alituambia huko Horebu, akasema, Mmekaa katika mlima huu vya kutosha; 7 geukeni mshike safari yenu mwende nchi ya milima ya Waamori, na mahali pote palipo karibu ya hapo, katika hiyo Araba, na nchi ya vilima vilima, na huko Shefela, na Negebu, na pwani pwani, nchi ya Wakanaani, na Lebanoni, mpaka mto huo mkubwa, mto wa Frati. 8 Angalieni, nimewawekea nchi mbele yenu, ingieni mkaimiliki nchi BWANA aliyowaapia baba zenu, Abrahamu, na Isaka, na Yakobo, kwamba atawapa na uzao wao baada yao. Viongozi wa makabila wateuliwa 9 Nami wakati ule niliwaambia, nikasema, Mimi siwezi kuwachukua peke yangu. 10 BWANA, Mungu wenu, amewafanya kuwa wengi, nanyi, angalieni, mmekuwa leo mfano wa nyota za mbinguni kwa wingi. 11 BWANA, Mungu wa baba zenu, na awafanye kuwa wengi mara elfu kuliko mlivyo, na kuwabariki, kama alivyowaahidi. 12 Nitachukuaje peke yangu mimi mwenyewe udhia wenu, na mzigo wenu, na ugomvi wenu? 13 Jitwalieni watu wenye akili na fahamu, watu wanaojulikana, kwa kadiri ya makabila yenu, nami nitawafanya wawe vichwa juu yenu. 14 Nanyi mkanijibu, mkaniambia, Jambo ulilolisema ni jema la kufanya. 15 Basi nikatwaa vichwa vya makabila yenu wenye akili, waliojulikana, nikawafanya wawe vichwa juu yenu, makamanda wa maelfu, na makamanda wa mamia, na makamanda wa hamsini hamsini, na makamanda wa kumi kumi, na wenye amri, kwa kadiri ya makabila yenu. 16 Nikawaagiza wakati ule waamuzi wenu, nikawaambia, Sikilizeni ninyi maneno kati ya ndugu zenu, mkaamue kwa haki kati ya mtu na nduguye, na mgeni aliye pamoja naye. 17 Msitazame nafsi za watu katika hukumu; muwasikize wadogo na wakubwa sawasawa; msiche uso wa mtu yeyote; kwa kuwa hukumu ni ya Mungu; na lile neno liwashindalo mniletee mimi, nami nitalisikiza. 18 Nikawaamuru wakati huo mambo yote yaliyowapasa ninyi kuyafanya. Waisraeli wakataa kuingia katika nchi 19 Tukasafiri kutoka Horebu, tukapita katikati ya jangwa lile kubwa la kutisha mliloliona, njia ile ya kuiendea nchi ya vilima vya Waamori, kama BWANA, Mungu wetu, alivyotuamuru, tukafika Kadesh-barnea. 20 Nami nikawaambia, Mmefika nchi ya vilima ya Waamori, anayotupa sisi BWANA, Mungu wetu. 21 Tazama, BWANA, Mungu wako, ameiweka nchi mbele yako; haya panda, itamalaki, kama BWANA, Mungu wa baba zako, alivyokuambia; usiogope wala usifadhaike. 22 Nanyi mkanikaribia kila mmoja wenu, mkasema, Na tutume watu mbele yetu, ili watupelelezee nchi na kutuletea habari za njia itupasayo kuipandia, na za miji tutakayoifikia. 23 Neno hili likanipendeza sana; nikatwaa watu kumi na wawili, mtu mmoja wa kila kabila. 24 Nao wakageuka, wakapanda mlimani wakafika katika bonde la Eshkoli, wakalipeleleza. 25 Wakachuma baadhi ya matunda ya nchi ile mikononi mwao, wakatuletea huku chini, wakatuletea habari tena, wakasema, Nchi hii anayotupa BWANA, Mungu wetu, ni nchi njema. 26 Lakini hamkukubali kukwea huko, mliasi neno la BWANA, Mungu wenu; 27 mkanung'unika hemani mwenu, mkasema, Ni kwa sababu BWANA ametuchukia, ndipo akatutoa katika nchi ya Misri, apate kututia katika mikono ya Waamori, ili kutuangamiza. 28 Twakwea kwenda wapi? Ndugu zetu wameiyeyusha mioyo yetu, wakituambia, Wale watu ni wengi, ni warefu kuliko sisi; miji nayo ni mikubwa, imejengewa kuta hata mbinguni; na zaidi ya hayo huko tumewaona Waanaki. 29 Ndipo nikawaambia msiwaogope. 30 BWANA, Mungu wenu, anayetangulia mbele yenu, ndiye atakayewapigania, kwa mfano wa yote aliyowafanyia huko Misri mbele ya macho yenu; 31 na huko jangwani, ulipoona alivyokuchukua BWANA, Mungu wako, kama mtu amchukuavyo mwanawe, njia yote mliyoiendea, hata mkafika mahali hapa. 32 Lakini katika jambo hili hamkumwamini BWANA, Mungu wenu, 33 aliyewatangulia njiani, usiku kwa moto, kuwaonesha njia mtakayoiendea, na mchana kwa hilo wingu, ili apate kuwatafutia mahali pa kusimamisha hema zenu. Adhabu kwa ajili ya uasi wa Israeli 34 BWANA akaisikia sauti ya maneno yenu, akaghadhibika, akaapa, akasema, 35 Hakika yangu hapana mmoja miongoni mwa watu hawa wa kizazi hiki kibaya atakayeiona nchi hiyo nzuri, niliyowaapia baba zenu kuwapa, 36 isipokuwa Kalebu mwana wa Yefune, huyo ataiona; nami nitampa yeye na watoto wake nchi hiyo aliyoikanyaga; kwa kuwa amemfuata BWANA kwa kila neno. 37 Na BWANA alinikasirikia mimi kwa ajili yenu, akasema, Wala wewe hutaingia humo; 38 Yoshua mwana wa Nuni asimamaye mbele yako ndiye atakayeingia; mtie moyo; kwa kuwa yeye atawarithisha Israeli. 39 Tena, wadogo wenu, mliosema watakuwa mateka, na wana wenu, wasiokuwa leo na maarifa ya mabaya wala mema, ndio watakaoingia, nao ndio nitakaowapa, nao wataimiliki. 40 Na ninyi basi geukeni, mshike safari yenu, mwende jangwani kwa njia ya Bahari ya Shamu. 41 Ndipo mkanijibu, mkaniambia, Sisi tumefanya dhambi juu ya BWANA, tutakwea kupigana kwa mfano wa yote tuliyoamriwa na BWANA. Mkajihami kila mtu silaha zake za vita, mkafanya wepesi kukwea mlimani. 42 BWANA akaniambia, Waambie, Msiende, wala msipigane; kwani mimi siko kati yenu; msije mkapigwa mbele ya adui zenu. 43 Hata ingawa niliwaambia, hamkunisikiza, bali mliasi amri ya Bwana, makajiamini na kulewa mlimani. 44 Na Waamori waliokuwa wakikaa katika mlima huo, waliwatokea juu yenu, wakawafukuza, kama wafukuzwao na nyuki, wakawapigia Seiri mpaka Horma. 45 Mkarudi mkalia mbele za BWANA; BWANA asiisikize sauti yenu, wala hakuelekeza masikio yake kwenu. Maisha ya jangwani 46 Ndipo mkakaa Kadeshi siku nyingi, kwa kadiri ya hizo siku mlizokaa. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya