Isaya 62 - Swahili Revised Union Version - SRUVDCUthibitisho wa wokovu wa Sayuni 1 Kwa ajili ya Sayuni sitanyamaza, na kwa ajili ya Yerusalemu sitatulia, hata haki yake itakapotokea kama mwangaza, na wokovu wake kama taa iwakayo. 2 Na mataifa wataiona haki yako, na wafalme wote watauona utukufu wako; nawe utaitwa jina jipya, litakalotajwa na kinywa cha BWANA. 3 Nawe utakuwa taji la uzuri katika mkono wa BWANA, na kilemba cha kifalme mkononi mwa Mungu wako. 4 Hutaitwa tena Aliyeachwa, wala nchi yako haitaitwa tena, Ukiwa; bali utaitwa Hefziba; na nchi yako Beula; kwa kuwa BWANA anakufurahia, na nchi yako itaolewa. 5 Maana kama vile kijana amwoavyo mwanamwali, ndivyo wana wako watakavyokuoa wewe; na kama vile bwana arusi amfurahiavyo bibi arusi, ndivyo Mungu wako atakavyokufurahia wewe. 6 Nimeweka walinzi juu ya kuta zako, Ee Yerusalemu; hawatanyamaza mchana wala usiku; ninyi wenye kumkumbusha BWANA, msiwe na kimya; 7 wala msimwache akae kimya, mpaka atakapouimarisha Yerusalemu, na kuufanya usifike kote duniani. 8 BWANA ameapa kwa mkono wake wa kulia, na kwa mkono wa nguvu zake, Hakika sitawapa adui zako nafaka yako tena kuwa chakula chao; wala wageni hawatakunywa divai yako, uliyoifanyia kazi. 9 Lakini walioivuna, ndio watakaoila, na kumhimidi BWANA; na walioichuma, ndio watakaoinywa, ndani ya nyua za patakatifu pangu. 10 Piteni, piteni, katika malango; Itengenezeni njia ya watu; Tutieni, tutieni barabara; toeni mawe yake; Twekeni bendera kwa ajili ya makabila ya watu. 11 Tazama, BWANA ametangaza habari mpaka mwisho wa dunia, Mwambieni binti Sayuni, Tazama, wokovu wako unakuja; Tazama, thawabu yake iko pamoja naye, Na malipo yake yako mbele zake. 12 Nao watawaita, Watu watakatifu, Waliokombolewa na BWANA; Nawe utaitwa, Aliyetafutwa, Mji usioachwa. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya