Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

Isaya 56 - Swahili Revised Union Version - SRUVDC


Agano kuwafikia watiifu wote

1 BWANA asema hivi, Shikeni hukumu, mkatende haki; kwa maana wokovu wangu uko karibu kuja, na haki yangu kufunuliwa.

2 Heri afanyaye haya, na mwanadamu ayashikaye sana; azishikaye sabato asizivunje, auzuiaye mkono wake usifanye uovu wowote.

3 Wala mgeni, aambatanaye na BWANA, asiseme hivi, Hakika yake BWANA atanitenga na watu wake; wala towashi asiseme, Mimi ni mti mkavu.

4 Kwa maana BWANA awaambia hivi matowashi, wanaozishika sabato zangu, na kuyachagua mambo yanipendezayo, na kulishika sana agano langu;

5 Nitawapa hawa nyumbani mwangu, na ndani ya kuta zangu, kumbukumbu na jina, lililo jema kuliko kuwa na watoto wa kiume na wa kike; nitawapa jina lidumulo milele, lisilokatiliwa mbali.

6 Na wageni, walioandamana na BWANA ili wamhudumu, na kulipenda jina la BWANA, kuwa watumishi wake; kila aishikaye sabato asiivunje, na kulishika sana agano langu;

7 Nitawaleta hao nao hadi katika mlima wangu mtakatifu, na kuwafurahisha katika nyumba yangu ya sala; makafara yao na dhabihu zao zitakubaliwa juu ya madhabahu zangu; kwa maana nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa yote.

8 Bwana MUNGU, akusanyaye waliofukuzwa katika Israeli asema, Pamoja na hayo nitamkusanyia na wengine, zaidi ya hao walio wake waliokusanywa.


Ufisadi wa watawala wa Israeli

9 Enyi wanyama wote wa porini njoni Mle, enyi wanyama wote wa porini.

10 Walinzi wake ni vipofu, wote pia hawana maarifa; wote ni mbwa walio bubu, hawawezi kulia; huota ndoto, hulala, hupenda usingizi.

11 Naam, mbwa hao wana uchu sana, hawashibi kamwe; na hao ni wachungaji wasioweza kufahamu neno; wote pia wamegeuka upande, wazifuate njia zao wenyewe, kila mmoja kwa faida yake, toka pande zote.

12 Husema, Njooni, nitaleta divai, Na tunywe sana kileo; Na kesho itakuwa kama leo, Sikukuu kupita kiasi.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo