Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni

- Matangazo -

Isaya 38 - Swahili Revised Union Version - SRUVDC


Kuugua kwa Hezekia

1 Siku hizo Hezekia aliugua, akawa karibu kufa; na Isaya nabii, mwana wa Amozi, akaenda kwa mfalme, akamwambia, BWANA asema hivi, Tengeneza mambo ya nyumba yako; maana utakufa, wala hutapona.

2 Basi Hezekia akajigeuza, akaelekeza uso wake ukutani, akamwomba BWANA,

3 akasema, Ee BWANA, kumbuka haya, nakusihi, kwamba nimekwenda mbele zako katika kweli na kwa moyo mkamilifu, na kutenda yaliyo mema machoni pako. Hezekia akalia kwa uchungu.

4 Ikawa, neno la BWANA likamjia Isaya, kusema,

5 Nenda ukamwambie Hezekia, BWANA, Mungu wa Daudi, baba yako, asema hivi, Mimi nimeyasikia maombi yako, nimeyaona machozi yako; tazama, nitaziongeza siku zako, kiasi cha miaka kumi na mitano.

6 Nami nitakuokoa wewe, na mji huu, kutoka kwa mkono wa mfalme wa Ashuru, nami nitaulinda mji huu.

7 Jambo hili liwe ishara kwako, itokayo kwa BWANA, ya kuwa BWANA atalitimiza jambo hili alilolisema;

8 Tazama, nitakirudisha nyuma kivuli madaraja kumi, ambayo kilishuka juu ya duara ya Ahazi kwa sababu ya jua. Basi jua likarudi madaraja kumi katika hiyo duara, ambayo limekwisha kushuka.

9 Haya ndiyo maandiko ya Hezekia, mfalme wa Yuda, alipokuwa mgonjwa, naye akapona ugonjwa wake.

10 Nilisema, Katika usitawi wa siku zangu nitakwenda kuingia malango ya kuzimu; Nimenyimwa mabaki ya miaka yangu.

11 Nilisema, Sitamwona BWANA, yeye BWANA, katika nchi ya walio hai; Sitamwona mwanadamu tena pamoja na hao wakaao duniani.

12 Makao yangu yameondolewa kabisa, yamechukuliwa kama hema ya mchungaji; Nimekunja maisha yangu kama mfumaji; atanikatilia mbali na kitanda cha mfumi; Tangu mchana hata usiku wanimaliza.

13 Nilijituliza hata asubuhi; kama simba, anaivunja mifupa yangu yote; Tangu mchana hata usiku wanimaliza.

14 Kama mbayuwayu au korongo ndivyo nilivyolia; Niliomboleza kama hua; macho yangu yamedhoofu kwa kutazama juu; Ee BWANA, nimeonewa, na uwe mdhamini wangu.

15 Niseme nini? Yeye amenena nami, na yeye mwenyewe ametenda hayo; Nitakwenda polepole miaka yangu yote, kwa sababu ya uchungu wa nafsi yangu.

16 Ee Bwana, kwa mambo hayo watu huishi; Na uhai wa roho yangu u katika hayo yote; Kwa hiyo uniponye na kunihuisha.

17 Tazama; nilikuwa na uchungu mwingi kwa ajili ya amani yangu; Lakini kwa kunipenda umeniokoa kutoka kwa shimo la uharibifu; Kwa maana umezitupa dhambi zangu zote nyuma yako.

18 Kwa kuwa kuzimu hakuwezi kukusifu; mauti haiwezi kukuadhimisha; Wale washukao shimoni hawawezi kuutumainia uaminifu wako.

19 Aliye hai, naam, aliye hai, ndiye atakayekusifu, kama mimi leo; Baba atawajulisha watoto uaminifu wako.

20 BWANA yu tayari kunipa wokovu. Basi, kwa vinubi tutaziimba nyimbo zangu, Siku zote za maisha yetu nyumbani mwa BWANA.

21 Maana Isaya amesema, Na watwae mkate wa tini, wakauweke juu ya jipu, naye atapona.

22 Tena Hezekia alikuwa amesema, Iko ishara gani ya kunionesha ya kuwa nitapanda niingie nyumbani mwa BWANA?

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo