Hesabu 33 - Swahili Revised Union Version - SRUVDCVituo vya safari ya Waisraeli wakitoka Misri 1 Hivi ndivyo vituo vya wana wa Israeli, hapo walipotoka nchi ya Misri kwa vikosi chini ya uongozi wa Musa na Haruni. 2 Musa akaandika jinsi walivyotoka katika vituo, kituo baada ya kituo kwa kufuata amri ya BWANA; na hivi ndivyo vituo: 3 Wakasafiri kutoka Ramesesi mwezi wa kwanza, siku ya kumi na tano ya mwezi wa kwanza; siku ya pili baada ya Pasaka, wana wa Israeli wakatoka kwa uhodari mkubwa mbele ya macho ya Wamisri wote, 4 hapo Wamisri walipokuwa wanazika wazaliwa wa kwanza wao wote, BWANA aliokuwa amewapiga kati yao; BWANA akafanya hukumu juu ya miungu yao nayo. 5 Wana wa Israeli wakasafiri kutoka Ramesesi, wakapiga kambi katika Sukothi. 6 Kisha wakasafiri kutoka Sukothi, wakapiga kambi Ethamu, palipo katika mwisho wa nyika. 7 Wakasafiri kutoka Ethamu, na kurudi nyuma hata Pi-hahirothi palipokabili Baal-sefoni; wakapiga kambi mbele ya Migdoli. 8 Wakasafiri kutoka hapo mbele ya Hahirothi, wakapita katikati ya bahari na kuingia jangwani; kisha wakaenda safari ya siku tatu katika nyika ya Ethamu, wakapiga kambi Mara. 9 Wakasafiri kutoka Mara, wakafika Elimu; huko Elimu palikuwa na chemchemi za maji kumi na mbili, na mitende sabini; nao wakapiga kambi Elimu. 10 Wakasafiri kutoka Elimu wakapiga kambi karibu na Bahari ya Shamu. 11 Wakasafiri kutoka Bahari ya Shamu, wakapiga kambi katika nyika ya Sini. 12 Wakasafiri kutoka nyika ya Sini, wakapiga kambi Dofka. 13 Wakasafiri kutoka Dofka, wakapiga kambi Alushi. 14 Wakasafiri kutoka Alushi, wakapiga kambi Refidimu, ambapo hapakuwa na maji ya watu kunywa. 15 Wakasafiri kutoka Refidimu, wakapiga kambi katika nyika ya Sinai. 16 Wakasafiri kutoka nyika ya Sinai, wakapiga kambi Kibroth-hataava. 17 Wakasafiri kutoka Kibroth-hataava, wakapiga kambi Haserothi. 18 Wakasafiri kutoka Haserothi, wakapiga kambi Rithma. 19 Wakasafiri kutoka Rithma, wakapiga kambi Rimon-peresi. 20 Wakasafiri kutoka Rimon-peresi, wakapiga kambi Libna. 21 Wakasafiri kutoka Libna, wakapiga kambi Risa. 22 Wakasafiri kutoka Risa, wakapiga kambi Keheletha. 23 Wakasafiri kutoka Keheletha, wakapiga kambi katika mlima wa Sheferi 24 Wakasafiri kutoka huo mlima wa Sheferi, wakapiga kambi Harada. 25 Wakasafiri kutoka Harada, wakapiga kambi Makelothi. 26 Wakasafiri kutoka Makelothi, wakapiga kambi Tahathi. 27 Wakasafiri kutoka Tahathi wakapiga kambi Tera. 28 Wakasafiri kutoka Tera, wakapiga kambi Mithka. 29 Wakasafiri kutoka Mithka, wakapiga kambi Hashmona. 30 Wakasafiri kutoka Hashmona, wakapiga kambi Moserothi. 31 Wakasafiri kutoka Moserothi, wakapiga kambi Bene-yaakani. 32 Wakasafiri kutoka Bene-yaakani, wakapiga kambi Hor-hagidgadi. 33 Wakasafiri kutoka Hor-hagidgadi, wakapiga kambi Yotbatha. 34 Wakasafiri kutoka Yotbatha, wakapiga kambi Abrona. 35 Wakasafiri kutoka Abrona, wakapiga kambi Esion-geberi. 36 Wakasafiri kutoka Esion-geberi, wakapiga kambi katika nyika ya Sini (ni Kadeshi). 37 Wakasafiri kutoka Kadeshi wakapiga kambi katika mlima wa Hori, katika mpaka wa nchi ya Edomu, 38 Haruni akakwea mlima wa Hori, kwa amri ya BWANA, akafa hapo, katika mwaka wa arubaini baada ya wana wa Israeli kutoka katika nchi ya Misri, mwezi wa tano, siku ya kwanza ya mwezi. 39 Naye Haruni alikuwa mtu wa umri wa miaka mia moja ishirini na mitatu hapo alipokufa katika mlima wa Hori. 40 Ndipo Mkanaani, mfalme wa Aradi, aliyekaa pande za Negebu katika nchi ya Kanaani akasikia habari za kuja kwao wana wa Israeli. 41 Nao wakasafiri kutoka mlima wa Hori, wakapiga kambi Salmona. 42 Wakasafiri kutoka Salmona, wakapiga kambi Punoni. 43 Wakasafiri kutoka Punoni, wakapiga kambi Obothi. 44 Wakasafiri kutoka Obothi, wakapiga kambi Lye-abarimu, katika mpaka wa Moabu. 45 Wakasafiri kutoka Iye-abarimu, wakapiga kambi Dibon-gadi. 46 Wakasafiri kutoka Dibon-gadi, wakapiga kambi Almon-diblathaimu. 47 Wakasafiri kutoka Almon-diblathaimu, wakapiga kambi katika milima ya Abarimu, kukabili Nebo. 48 Wakasafiri kutoka hiyo milima ya Abarimu, wakapiga kambi katika nchi tambarare za Moabu, karibu na mto wa Yordani, hapo Yeriko. 49 Wakapiga kambi karibu na Yordani, tangu Beth-yeshimothi hata kufikia Abel-shitimu katika nchi tambarare za Moabu. Maagizo ya kuishinda Kanaani 50 Kisha BWANA akanena na Musa hapo katika nchi tambarare za Moabu, karibu na Yordani, hapo Yeriko, na kumwambia, 51 Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Mtakapovuka mto wa Yordani na kuingia nchi ya Kanaani, 52 ndipo mtakapowafukuza wenyeji wote wa hiyo nchi mbele yenu, nanyi mtayaharibu mawe yao yote yenye kuchorwa sanamu, na kuziharibu sanamu zao zote za kusubu, kuvunjavunja mahali pao pote palipoinuka; 53 nanyi mtaishika hiyo nchi kuimiliki na kuishi humo; kwa kuwa mimi nimewapa ninyi hiyo nchi ili mwimiliki. 54 Nanyi mtairithi nchi kwa kufanya kura, kama jamaa zenu zilivyo; hao walio wengi mtawapa urithi zaidi, na hao waliopunguka utawapa kama kupunguka kwao; mahali popote kura itakapomwangukia mtu yeyote, mahali hapo ni pake; mtarithi kama makabila ya baba zenu yalivyo. 55 Lakini kama hamtaki kuwafukuza wenyeji wa nchi watoke mbele yenu; ndipo hao ambao mtawabakiza watakuwa kama sindano machoni mwenu, na kama miiba ubavuni mwenu, nao watawasumbua katika hiyo nchi ambayo mwakaa. 56 Kisha itakuwa, kama nilivyoazimia kuwatenda wao, ndivyo nitakavyowatenda ninyi. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya