Hesabu 31 - Swahili Revised Union Version - SRUVDCVita juu ya Midiani 1 Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia, 2 Walipizie kisasi wana wa Israeli juu ya Wamidiani; kisha baadaye utakusanywa uwe pamoja na watu wako. 3 Basi Musa akanena na watu, na kuwaambia, Wavikeni silaha watu miongoni mwenu waende vitani, ili waende kupigana na Midiani, wapate kumlipizia kisasi BWANA, juu ya Midiani. 4 Katika kila kabila mtatoa watu elfu moja, katika kabila zote za Israeli, nanyi mtawatuma waende vitani. 5 Basi walitolewa katika maelfu ya Israeli, elfu moja ya kila kabila, wanaume elfu kumi na mbili walioandaliwa kwa vita. 6 Basi Musa akawatuma watu elfu wa kila kabila waende vitani, wao na Finehasi mwana wa Eleazari kuhani, waende vitani, na vile vyombo vya mahali patakatifu, na hizo tarumbeta za kupiga sauti za kugutusha mkononi mwake. 7 Nao wakapigana na Midiani kama BWANA alivyomwagiza Musa; nao wakawaua kila mwanamume. 8 Nao wafalme wa Midiani wakawaua pamoja na watu wengine waliouawa; Evi, na Rekemu, na Suri, na Huri, na Reba, hao wafalme watano wa Midiani; Balaamu mwana wa Beori naye wakamwua kwa upanga. 9 Wana wa Israeli wakawachukua mateka wanawake wa Midiani na watoto wao; na ng'ombe zao wote, na kondoo zao wote, na mali zao zote, wakachukua nyara. 10 Na miji yao yote, kila mahali walipokuwa wakikaa, na kambi yao yote wakayateketeza kwa moto. 11 Nao wakatwaa hizo nyara zote, na mateka yote, ya wanadamu na ya wanyama. 12 Nao wakawaleta mateka ya wanadamu, na mateka ya wanyama, na hizo nyara, na kuyaweka mbele ya Musa, na mbele ya Eleazari kuhani, na mbele ya mkutano wa wana wa Israeli, hapo kambini katika nchi tambarare za Moabu, zilizo karibu na Yordani hapo Yeriko. Kurejea toka Vitani 13 Basi Musa, na Eleazari kuhani, na wakuu wote wa huo mkutano, wakatoka nje kwenda kuwalaki nje ya kambi. 14 Musa akawakasirikia majemadari wa jeshi, na hao makamanda wa maelfu, na makamanda wa mamia, hao waliorudi kutoka kupigana vita. 15 Musa akawauliza, Je! Mmewaponya wanawake wote hai? 16 Tazama, hawa ndio waliowakosesha wana wa Israeli, kwa shauri la Balaamu, wamfanyie BWANA dhambi katika hilo jambo la Peori, na kwa hiyo pigo lilikuwa katika mkutano wa BWANA. 17 Basi kwa ajili hiyo mwueni kila mwanamume katika hao watoto, na kila mwanamke aliyemjua mwanamume kwa kulala pamoja naye. 18 Lakini hao wasichana wote ambao hawakumjua mwanamume kwa kulala pamoja naye, mtawaweka hai kwa ajili yenu. 19 Nanyi fanyeni matuo yenu nje ya kambi muda wa siku saba; mtu yeyote aliyemwua mtu, na yeyote aliyemgusa mtu aliyeuawa, jitakaseni nafsi zenu siku ya tatu, na siku ya saba, ninyi na mateka yenu. 20 Na kuhusu kila nguo, na kila kitu kilichofanywa cha ngozi, na kazi yote ya singa za mbuzi, na vyombo vyote vilivyofanywa vya mti, mtajitakasa wenyewe; 21 Kisha Eleazari kuhani akawaambia wanaume wa vita wote waliokwenda vitani, Hii ndiyo amri ya sheria BWANA aliyomwagiza Musa; 22 lakini dhahabu, na fedha, na shaba, na chuma, na bati, na risasi, 23 kila kitu kiwezacho kuuhimili moto, mtakipitisha katika moto, nacho kitakuwa safi, pamoja na haya kitatakaswa kwa hayo maji ya utakaso; na kila kitu kisichouhimili moto mtakipitisha katika hayo maji. 24 Nanyi mtazifua nguo zenu siku ya saba, nanyi mtakuwa safi, kisha baadaye mtaingia kambini. Mgawanyo wa mateka na nyara 25 Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia, 26 Fanya jumla ya hayo mateka ya wanadamu, na ya wanyama pia, wewe, na Eleazari kuhani, na wakuu wa nyumba za baba za mkutano; 27 ukagawanye nyara katika mafungu mawili; kati ya wanajeshi waliotoka nje kupigana vita na hio jumuiya nzima; 28 kisha uwatoze hao watu wa vita waliotoka kwenda vitani sehemu kwa ajili ya BWANA; mmoja katika mia tano, katika wanadamu, na katika ng'ombe, na katika punda, na katika kondoo; 29 twaa katika nusu yao, ukampe Eleazari kuhani, kuwa sadaka ya kuinuliwa kwa BWANA. 30 Na katika hiyo nusu ya wana wa Israeli utatwaa mmoja atakayetolewa katika kila hamsini, katika wanadamu, na katika ng'ombe, na katika punda, na katika kondoo, maana, katika wanyama wote, ukawape Walawi, hao wenye wajibu wa kuhudumu maskani ya BWANA. 31 Musa na Eleazari kuhani wakafanya kama BWANA alivyomwagiza Musa. 32 Basi masazo ya hizo nyara walizotwaa watu wa vita, zilikuwa ni kondoo elfu mia sita na sabini na tano, 33 na ng'ombe elfu sabini na mbili, 34 na punda elfu sitini na moja, 35 tena wanadamu jumla yao ilikuwa elfu thelathini na mbili, katika hao wanawake ambao hawakumjua mwanamume kwa kulala pamoja naye. 36 Na hiyo nusu ambayo ilikuwa ni sehemu ya hao waliotoka kwenda vitani, idadi yake ilikuwa kondoo elfu mia tatu na thelathini na saba na mia tano; 37 na kodi ya BWANA katika hao kondoo ilikuwa kondoo mia sita na sabini na watano. 38 Tena, ng'ombe walikuwa elfu thelathini na sita; na katika hao kodi ya BWANA ilikuwa ng'ombe sabini na wawili. 39 Na punda walikuwa elfu thelathini na mia tano, katika hao kodi ya BWANA ilikuwa punda sitini na mmoja. 40 Na wanadamu walikuwa watu elfu kumi na sita; katika hao sehemu ya BWANA ilikuwa ni watu thelathini na wawili. 41 Basi Musa akampa Eleazari kuhani hiyo sehemu, iliyokuwa sadaka ya kuinuliwa kwa BWANA, kama BWANA alivyomwagiza Musa. 42 Tena katika hiyo nusu iliyokuwa ya wana wa Israeli, ambayo Musa aliitenga na watu waliokwenda vitani, 43 (basi hiyo nusu ya mkutano ilikuwa ni kondoo elfu mia tatu na thelathini na saba na mia tano, 44 na ng'ombe elfu thelathini na sita, 45 na punda elfu thelathini, na mia tano, 46 na wanadamu elfu kumi na sita;) 47 na katika hiyo nusu iliyokuwa ya wana wa Israeli, Musa akatwaa mmoja aliyetolewa katika kila hamsini, wa binadamu na wa wanyama, akawapa Walawi, wenye wajibu wa kuhudumu katika maskani ya BWANA; kama BWANA alivyomwagiza Musa. 48 Na majemadari waliokuwa juu ya maelfu ya hilo jeshi, na viongozi wa maelfu, na viongozi wa mamia, wakamkaribia Musa; 49 wakamwambia Musa wakisema, Sisi watumishi wako tumefanya jumla ya hesabu ya watu wa vita walio chini ya mikono yetu, na hapana hata mmoja aliyetupungukia. 50 Nasi tumeleta matoleo ya BWANA, aliyopata kila mtu, ya vyombo vya dhahabu, na mitali, na timbi, na pete za mhuri, na vipini, na vikuku, ili kuzifanyia upatanisho nafsi zetu mbele ya BWANA. 51 Musa na Eleazari kuhani wakapokea kwao hiyo dhahabu, maana, vile vyombo vyote vilivyofanyizwa. 52 Na dhahabu yote ya sadaka ya kuinuliwa waliyosongeza kwa BWANA, ya makamanda wa maelfu, na makamanda wa mamia, ilikuwa shekeli elfu kumi na sita, mia saba na hamsini. 53 (Kwa kuwa wanajeshi walikuwa wamechukua nyara kila mtu zake binafsi.) 54 Basi Musa na Eleazari kuhani wakapokea hiyo dhahabu mikononi mwa hao makamanda wa maelfu na wa mamia, na kuileta ndani ya hema ya kukutania, ili iwe ukumbusho kwa ajili ya wana wa Israeli mbele za BWANA. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya