Hesabu 29 - Swahili Revised Union Version - SRUVDCSadaka za sikukuu ya mabaragumu 1 Tena mwezi wa saba, siku ya kwanza ya mwezi, mtakuwa na kusanyiko takatifu; hamtafanya kazi yoyote ya utumishi; ni siku ya kupiga tarumbeta kwenu. 2 Nanyi mtasongeza sadaka ya kuteketezwa kuwa harufu ya kupendeza kwa BWANA; ng'ombe dume mchanga mmoja, na kondoo dume mmoja, na wana-kondoo dume saba wa mwaka mmoja wote wasiwe na dosari; 3 pamoja na sadaka yake ya unga, unga laini uliochanganywa na mafuta, sehemu ya tatu ya kumi ya ng'ombe, sehemu ya mbili ya kumi kwa kondoo dume, 4 na sehemu ya moja ya kumi kwa kila mwana-kondoo katika wale wana-kondoo saba; 5 na mbuzi dume mmoja kuwa sadaka ya dhambi, ili kufanya upatanisho kwa ajili yenu; 6 zaidi ya hiyo sadaka ya kuteketezwa ya kuandama mwezi, na sadaka yake ya unga, na hiyo sadaka ya kuteketezwa ya sikuzote, na sadaka yake ya unga, na sadaka zake za vinywaji, kama ilivyo amri yake, kuwa harufu ya kupendeza, ni sadaka iliyosongezwa kwa BWANA kwa moto. Sadaka za siku ya upatanisho 7 Tena siku ya kumi ya huo mwezi wa saba mtakuwa na kusanyiko takatifu; nanyi mtajinyima nafsi zenu, msifanye kazi yoyote ya utumishi 8 lakini mtamsogezea BWANA sadaka ya kuteketezwa, kuwa harufu ya kupendeza; ng'ombe dume mchanga mmoja, na kondoo dume mmoja, na wana-kondoo dume saba wa mwaka mmoja; watakuwa wakamilifu kwenu; 9 pamoja na sadaka zake za unga, unga laini uliochanganywa na mafuta, sehemu ya tatu ya kumi kwa huyo ng'ombe, na sehemu ya mbili ya kumi kwa huyo kondoo, 10 na sehemu ya moja ya kumi kwa kila mwana-kondoo katika wale wana-kondoo saba; 11 na mbuzi dume mmoja kuwa sadaka ya dhambi; zaidi ya hiyo sadaka ya dhambi ya upatanisho, na hiyo sadaka ya kuteketezwa ya sikuzote, na sadaka yake ya unga, na sadaka zake za vinywaji. Sadaka za siku kuu ya vibanda 12 Tena siku ya kumi na tano ya mwezi wa saba mtakuwa na kusanyiko takatifu; hamtafanya kazi yoyote kwenye nafsi zenu, nanyi mtamfanyia BWANA sikukuu muda wa siku saba; 13 nanyi mtasongeza sadaka ya kuteketezwa, sadaka isongezwayo kwa moto, harufu ya kupendeza kwa BWANA; ng'ombe dume wachanga kumi na watatu na kondoo dume wawili, na wana-kondoo dume wa mwaka mmoja kumi na wanne; wote watakuwa wakamilifu; 14 pamoja na sadaka zake za unga, unga laini uliochanganywa na mafuta, sehemu ya tatu ya kumi kwa kila ng'ombe katika wale kumi na watatu na sehemu ya mbili ya kumi kwa kila kondoo katika hao kondoo dume wawili; 15 na sehemu ya moja ya kumi kwa kila mwana-kondoo katika wale wana-kondoo kumi na wanne; 16 na mbuzi dume mmoja kuwa sadaka ya dhambi zaidi ya hiyo sadaka ya kuteketezwa ya sikuzote, na sadaka yake ya unga, na sadaka yake ya kinywaji. 17 Tena siku ya pili mtasongeza ng'ombe dume wachanga kumi na wawili, na kondoo dume wawili, na wana-kondoo dume wa mwaka mmoja kumi na wanne wakamilifu; 18 pamoja na sadaka yake ya unga, na sadaka zake za vinywaji kwa hao ng'ombe, na kwa hao kondoo, na kwa wale wana-kondoo kama idadi yao ilivyo, kulingana na amri hiyo; 19 na mbuzi dume mmoja kuwa sadaka ya dhambi; zaidi ya hiyo sadaka ya kuteketezwa ya sikuzote, na sadaka yake ya unga, na sadaka zake za vinywaji. 20 Tena siku ya tatu mtasongeza ng'ombe dume kumi na mmoja, na kondoo dume wawili, na wana-kondoo dume wa mwaka mmoja wasio na dosari kumi na wanne; 21 pamoja na sadaka yake ya unga, na sadaka zake za vinywaji, kwa hao ng'ombe, na kwa hao kondoo, na kwa wale wana-kondoo kama idadi yao ilivyo kulingana na amri; 22 na mbuzi dume mmoja kuwa sadaka ya dhambi; zaidi ya hiyo sadaka ya kuteketezwa ya sikuzote, na sadaka yake ya unga, na sadaka yake ya kinywaji. 23 Tena siku ya nne mtasongeza ng'ombe dume kumi, na kondoo dume wawili, na wana-kondoo dume wa mwaka mmoja wasio na dosari kumi na wanne; 24 na sadaka yake ya unga, na sadaka zake za vinywaji kwa hao ng'ombe, na kwa hao kondoo, na kwa wale wana-kondoo, kama idadi yao ilivyo, kulingana na amri; 25 na mbuzi dume mmoja kuwa sadaka ya dhambi, zaidi ya hiyo sadaka ya kuteketezwa ya sikuzote, na sadaka yake ya unga, na sadaka yake ya kinywaji. 26 Tena siku ya tano mtasongeza ng'ombe dume tisa, na kondoo dume wawili, na wana-kondoo dume wa mwaka mmoja wasio na dosari kumi na wanne; 27 pamoja na sadaka yake ya unga, na sadaka zake za vinywaji, kwa hao ng'ombe, na kwa hao kondoo, na kwa wale wana-kondoo, kama idadi yao ilivyo, kulingana na amri; 28 na mbuzi dume mmoja kuwa sadaka ya dhambi; zaidi ya hiyo sadaka ya kuteketezwa ya siku zote, na hiyo sadaka yake ya unga na sadaka yake ya kinywaji. 29 Tena siku ya sita mtasongeza ng'ombe dume wanane, na kondoo dume wawili, na wana-kondoo dume wa mwaka mmoja wasio na dosari kumi na wanne; 30 pamoja na sadaka yake ya unga, na sadaka zake za vinywaji, kwa hao ng'ombe, na kwa hao kondoo, na kwa wale wana-kondoo, kama idadi yao ilivyo, kulingana na amri; 31 na mbuzi dume mmoja kuwa sadaka ya dhambi; zaidi ya hiyo sadaka ya kuteketezwa ya siku zote, na hiyo sadaka yake ya unga na sadaka yake ya kinywaji. 32 Tena siku ya saba mtasongeza ng'ombe dume saba, na kondoo dume wawili, na wana-kondoo dume wa mwaka mmoja wasio na dosari kumi na wanne; 33 pamoja na sadaka yake ya unga, na sadaka zake za vinywaji, kwa hao ng'ombe, na kwa hao kondoo, na kwa wale wana-kondoo, kama idadi yao ilivyo, kulingana na amri; 34 na mbuzi dume mmoja kuwa sadaka ya dhambi; zaidi ya hiyo sadaka ya kuteketezwa ya siku zote, na hiyo sadaka yake ya unga na sadaka yake ya kinywaji. 35 Tena siku ya nane mtakuwa na kusanyiko la makini sana; hamtafanya kazi yoyote kwenye nafsi zenu; 36 lakini mtasongeza sadaka ya kuteketezwa, sadaka ya kusongezwa kwa moto, harufu ya kupendeza kwa BWANA; ng'ombe dume mmoja, na kondoo dume mmoja, na wana-kondoo dume wa mwaka mmoja wasio na dosari saba; 37 pamoja na sadaka yake ya unga, na sadaka zake za vinywaji, kwa huyo ng'ombe, na kwa huyo kondoo dume, na kwa wale wana-kondoo, kama idadi yao ilivyo, kulingana na amri; 38 na mbuzi dume mmoja kuwa sadaka ya dhambi; zaidi ya hiyo sadaka ya kuteketezwa ya siku zote, na hiyo sadaka yake ya unga na sadaka yake ya kinywaji. 39 Sadaka hizo mtamsogezea BWANA katika sikukuu zenu zilizoamriwa, zaidi ya nadhiri zenu, na sadaka zenu za hiari, kuwa sadaka zenu za kuteketezwa, na sadaka zenu za unga, na sadaka zenu za vinywaji, na sadaka zenu za amani. 40 Naye Musa akawaambia wana wa Israeli vile vile kama hayo yote BWANA alivyomwagiza Musa. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya