Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

Ezekieli 24 - Swahili Revised Union Version - SRUVDC


Chungu kitokotacho

1 Tena, katika mwaka wa tisa, mwezi wa kumi, siku ya kumi ya mwezi, neno la BWANA likanijia, kusema,

2 Mwanadamu, liandike jina la siku hii, naam, la siku ii hii; mfalme wa Babeli ameuzingira Yerusalemu siku ii hii.

3 Ukawatungie mithali nyumba ya kuasi, ukawaambie, Bwana MUNGU asema hivi; Teleka sufuria, liteleke; ukatie maji ndani yake;

4 vikusanye vipande vyake ndani yake, naam, kila kipande chema, paja na bega; lijaze mifupa iliyochaguliwa.

5 Uwatwae wateule wa kundi la kondoo, ukafanye chungu ya mifupa chini yake; ukalitokose sana; naam, mifupa yake itokoswe ndani yake.

6 Basi Bwana MUNGU asema hivi; Ole wake mji wa damu! Hilo sufuria ambalo kutu yake i ndani yake, ambalo kutu yake haikulitoka; litoe kipande kipande; hapana kura iliyoanguka juu yake.

7 Maana damu yake imo ndani yake; aliiweka juu ya jabali lililo wazi; hakuimwaga juu ya nchi, apate kuifunika kwa mavumbi;

8 ili ipandishe ghadhabu ya kulipa kisasi, nimeiweka damu yake juu ya jabali lililo wazi, isipate kufunikwa.

9 Basi Bwana MUNGU asema hivi; Ole wake mji wa damu! Mimi nami nitaiongeza chungu.

10 Tia kuni nyingi, uchochee moto, itokose nyama sana, fanyiza mchuzi mzito, mifupa ikateketee.

11 Kisha litie juu ya makaa yake, tupu, lipate moto, na shaba yake iteketee, uchafu wake uyeyushwe, na kutu yake iteketee.

12 Amejidhoofisha kwa taabu, lakini kutu yake nyingi haikumtoka; kutu yake haitoki kwa moto.

13 Katika uchafu wako mna uasherati, kwa maana nimekusafisha, ila wewe hukusafika; hutasafishwa tena uchafu wako ukutoke, hadi nitakapokuwa nimeituliza hasira yangu kwako.

14 Mimi, BWANA, nimenena neno hili, nalo litakuwa; nami nitalifanya; sitaachilia, wala sitahurumia, wala sitajuta; kulingana na njia zako, na kulingana na matendo yako, ndivyo watakavyokuhukumu, asema Bwana MUNGU.


Kufiwa kwa Ezekieli

15 Neno la BWANA likanijia tena, kusema,

16 Mwanadamu, tazama, ninakuondolea kwa pigo moja tunu, mteule wa macho yako; walakini hutaomboleza wala kulia, wala yasichuruzike machozi yako.

17 Piga kite lakini si kwa sauti ya kusikiwa; usifanye matanga kwa ajili yake yeye aliyekufa; jipige kilemba chako, ukavae viatu vyako, wala usiifunike midomo yako, wala usile chakula cha watu.

18 Basi nilisema na watu asubuhi, na jioni mke wangu akafa; nami kesho yake asubuhi nilifanya kama nilivyoagizwa.

19 Watu hao wakaniambia, Je! Hutaki kutuambia maana ya mambo haya kwetu, hata umefanya kama vile ufanyavyo.

20 Nikawaambia, Neno la BWANA lilinijia, kusema,

21 Uwaambie nyumba ya Israeli, Bwana MUNGU asema hivi; Angalieni, nitapatia unajisi patakatifu pangu, fahari ya uwezo wenu, mahali pa kutamaniwa na macho yenu, ambapo roho zenu zinapahurumia na wana wenu na binti zenu, mliowaacha nyuma, wataanguka kwa upanga.

22 Nanyi mtafanya kama mimi nilivyofanya; hamtaifunika midomo yenu, wala kula chakula cha watu.

23 Na vilemba vyenu vitakuwa juu ya vichwa vyenu, na viatu vyenu miguuni mwenu; hamtaomboleza wala kulia; lakini mtafifia katika maovu yenu, na kusikitika kila mtu pamoja na mwenziwe.

24 Basi ndivyo Ezekieli atakavyokuwa ishara kwenu; ninyi mtatenda sawasawa na yote aliyoyatenda yeye; litakapokuja jambo hili, ndipo mtakapojua ya kuwa mimi ndimi Bwana MUNGU.

25 Nawe, mwanadamu, je! Haitakuwa hivi katika siku hiyo nitakapowaondolea nguvu zao, na furaha ya utukufu wao, na kilichotamaniwa na macho yao, ambacho walikiinulia mioyo yao, watoto wao wa kiume na watoto wao wa kike,

26 kwamba katika siku iyo hiyo yeye atakayeokoka atakuja kwako, akusikize jambo hili kwa masikio yako?

27 Siku hiyo kinywa chako kitafumbuliwa kwake aliyeokoka, nawe utasema; hutakuwa bubu tena; ndivyo utakavyokuwa ishara kwao; nao watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo