Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

Ezekieli 2 - Swahili Revised Union Version - SRUVDC


Maono ya gombo

1 Akaniambia, Mwanadamu, simama kwa miguu yako, nami nitasema nawe.

2 Naye aliposema nami, roho ikaniingia, ikanisimamisha; nikamsikia yeye aliyesema nami.

3 Akaniambia, Mwanadamu, nakutuma kwa wana wa Israeli, kwa mataifa wanaoasi, walioniasi mimi; wao na baba zao wameasi juu yangu, naam, hata hivi leo.

4 Na wana hao wana nyuso zisizo na haya, na mioyo yao ni migumu. Mimi nakutuma kwa hao; nawe utawaambia, Bwana MUNGU asema hivi.

5 Nao, iwe watasikia au hawataki kusikia, (maana ndio nyumba ya kuasi hao), hata hivyo watajua ya kuwa nabii amekuwako miongoni mwao.

6 Na wewe, mwanadamu, usiwaogope hao, wala usiyaogope maneno yao, ijapokuwa miiba na michongoma inakuzunguka, nawe unakaa katikati ya nge; usiyaogope maneno yao, wala usifadhaike kwa sababu ya nyuso zao, wajapokuwa ni nyumba yenye kuasi.

7 Nawe utawaambia maneno yangu, iwe watasikia au hawataki kusikia; maana hao wanaasi sana.

8 Bali wewe, mwanadamu, sikia neno hili ninalokuambia; usiwe wewe mwenye kuasi kama nyumba ile yenye kuasi; funua kinywa chako, ule nikupacho.

9 Nami nilipotazama, mkono ulinyoshwa kunielekea; na tazama, gombo la kitabu lilikuwa ndani yake.

10 Akalikunjua mbele yangu; nalo lilikuwa limeandikwa ndani na nje; ndani yake yalikuwa yameandikwa maombolezo, na vilio, na ole!

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo