Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

2 Mambo ya Nyakati 3 - Swahili Revised Union Version - SRUVDC


Sulemani ajenga hekalu

1 Ndipo Sulemani akaanza kuijenga nyumba ya BWANA huko Yerusalemu, juu ya mlima Moria, pale BWANA alipomtokea Daudi babaye alipotengeza mahali pale alipoagiza Daudi, katika kiwanja cha kupuria cha Arauna Myebusi.

2 Akaanza kujenga siku ya pili ya mwezi wa pili katika mwaka wa nne wa kutawala kwake.

3 Basi hivi ndivyo vipimo vya majengo ya nyumba ya Mungu alivyoviweka Sulemani. Urefu wake ulikuwa dhiraa sitini na upana wake dhiraa ishirini.

4 Na ukumbi uliokuwa mbele yake, urefu wake ulikuwa sawa na upana wa nyumba ulikuwa dhiraa ishirini, na kimo chake mia moja na ishirini; akaufunikiza ndani kwa dhahabu safi.

5 Nayo nyumba kubwa ilizungushiwa miti ya miberoshi, aliyoifunikiza kwa dhahabu safi, juu yake akaichora mitende na minyororo.

6 Akaipamba nyumba kwa vito iwe na uzuri; nayo dhahabu ilikuwa dhahabu ya Parvaimu.

7 Tena, akaifunikiza kwa dhahabu nyumba, na boriti, na vizingiti, na kuta zake, na milango yake; akachora makerubi kutani.

8 Akaifanya nyumba ya patakatifu pa patakatifu; urefu wake sawa na upana wa nyumba, ulikuwa dhiraa ishirini, na upana wake dhiraa ishirini; akaifunikiza kwa dhahabu safi, ya talanta mia sita.

9 Na uzani wa misumari ulikuwa shekeli hamsini za dhahabu. Alivifunika vyumba vyake ghorofani kwa dhahabu.

10 Na ndani ya nyumba ya patakatifu pa patakatifu akatengeneza makerubi mawili ya kuchonga; wakayafunika kwa dhahabu.

11 Na mabawa ya makerubi hayo urefu wake ulikuwa mikono ishirini; bawa moja mikono mitano, likiufikia ukuta wa nyumba; na bawa la pili mikono mitano, likishikana na bawa la kerubi la pili.

12 Na bawa la kerubi la pili lilikuwa mikono mitano, likiufikia ukuta wa nyumba; na bawa la pili mikono mitano, likishikana na bawa la kerubi la kwanza.

13 Yakaenea mabawa ya makerubi hayo dhiraa ishirini; yakasimama juu ya miguu yao, na nyuso zao ziliielekea nyumba.

14 Akalifanya pazia la samawati na urujuani na nyekundu, na kitani safi, akaitengeneza makerubi.

15 Tena akafanya mbele ya nyumba nguzo mbili za mikono thelathini na tano kwenda juu kwake, na mataji yaliyokuwa juu yake moja moja ilikuwa mikono mitano.

16 Akafanya minyororo ndani ya chumba cha ndani, akaiweka juu ya vichwa vya nguzo; akafanya makomamanga mia moja, akayaweka juu ya hiyo minyororo.

17 Akazisimamisha nguzo hizo mbele ya hekalu, moja upande wa kulia, na ya pili upande wa kushoto; akaliita jina la ile ya kulia Yakini, na jina la ile ya kushoto Boazi.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo