2 Mambo ya Nyakati 28 - Swahili Revised Union Version - SRUVDCUtawala wa Ahazi 1 Ahazi alikuwa na umri wa miaka ishirini alipoanza kutawala; akatawala katika Yerusalemu miaka kumi na sita; wala hakufanya yaliyo ya adili machoni pa BWANA, kama Daudi babaye; 2 bali akaziendea njia za wafalme wa Israeli, alitengeneza sanamu za mabaali za kusubu. 3 Tena akafukiza uvumba katika bonde la mwana wa Hinomu, akawateketeza wanawe motoni, sawasawa na machukizo ya mataifa, aliowafukuza BWANA mbele ya wana wa Israeli. 4 Akatoa dhabihu na kufukiza uvumba katika mahali pa juu, na vilimani, na chini ya kila mti wenye majani mabichi. Shamu na Israeli waishinda Yuda 5 Kwa hiyo BWANA, Mungu wake, akamtia mkononi mwa mfalme wa Shamu; wakampiga, wakachukua wa watu wake wafungwa wengi sana, wakawaleta Dameski. Tena akatiwa mkononi mwa mfalme wa Israeli, aliyempiga mapigo makuu. 6 Peka mwana wa Remalia akawaua katika Yuda siku moja watu elfu mia moja na ishirini, mashujaa wote; kwa sababu walikuwa wamemwacha BWANA, Mungu wa baba zao. 7 Naye Zikri, mtu hodari wa Efraimu, akawaua Maaseya mwana wa mfalme, na Azrikamu mkuu wa nyumba, na Elkana, aliyekuwa wa pili wake mfalme. Obedi aingilia kati 8 Waisraeli wakachukua mateka ndugu zao wafungwa elfu mia mbili wakiwemo wanawake, watoto wa kiume na kike, pia wakachukua kwao nyara nyingi, wakazileta nyara Samaria. 9 Lakini kulikuwako huko nabii wa BWANA, jina lake aliitwa Odedi; akatoka kuwalaki jeshi waliokuja Samaria, akawaambia, Angalieni, kwa kuwa BWANA, Mungu wa baba zenu, aliwakasirikia Yuda, yeye amewatia mikononi mwenu, nanyi mmewaua kwa ghadhabu iliyofikia mbinguni. 10 Na sasa mnanuia kuwatawala wana wa Yuda na Yerusalemu na kuwafanya wawe watumwa na wajakazi wenu; lakini ninyi nanyi je! Hamna hatia zenu wenyewe juu ya BWANA, Mungu wenu? 11 Haya, nisikieni mimi basi, mwarudishe wafungwa, mliowachukua mateka wa ndugu zenu; kwa maana ghadhabu ya BWANA iliyo kali iko juu yenu. 12 Ndipo wakaondoka juu ya hao waliotoka vitani baadhi ya wakuu wa wana wa Efraimu, Azaria, mwana wa Yohanani, na Berekia mwana wa Meshilemothi, na Yehizkia mwana wa Shalumu, na Amasa mwana wa Hadlai, 13 wakawaambia, Hamtawaleta wafungwa humo; kwa sababu mnayanuia yatakayotutia hatiani mbele za BWANA, kuongeza dhambi zetu, na hatia yetu; maana hatia yetu ni kubwa, na ghadhabu kali ipo juu ya Israeli. 14 Basi watu wenye silaha wakawaachilia wafungwa na nyara mbele ya wakuu na kusanyiko lote. 15 Wakaondoka wale watu waliotajwa majina yao, wakawatwaa wafungwa, wakawavika kwa zile nyara wale wote waliokuwa uchi, wakawapa mavazi na viatu, wakawalisha, wakawanywesha, wakawatia mafuta, wakawapandisha waliokuwa dhaifu miongoni mwao juu ya punda wakawaleta Yeriko, mji wa mitende, kwa ndugu zao; kisha wakarudi Samaria. Ashuru Yakataa Kuisaidia Yuda 16 Wakati ule mfalme Ahazi akatuma wajumbe kwa mfalme wa Ashuru ili amsaidie. 17 Kwa kuwa Waedomi walikuwa wamekuja tena, na kuwapiga Yuda, na kuwachukua wafungwa. 18 Wafilisti pia walikuwa wameishambulia na kuitwaa miji ya Shemeshi, Ayaloni, Gederothi, soko, pamoja na vijiji vyake, Timna pamoja na vijiji vyake na Gimzo pia na vijiji vyake, miji yake; wakakaa humo. 19 Kwa maana BWANA aliinamisha Yuda kwa ajili ya Ahazi mfalme wa Israeli; kwa kuwa yeye aliwafanyia Yuda aibu, na kumwasi BWANA mno. 20 Na Tiglath-pileseri mfalme wa Ashuru akamjia, akamfadhaisha, asimtie nguvu kwa lolote. 21 Kwa maana Ahazi alitwaa sehemu katika nyumba ya BWANA, na katika nyumba ya mfalme, na ya wakuu, akampa mfalme wa Ashuru; asisaidiwe na jambo hilo. Ukaidi na kifo cha Ahazi 22 Na wakati alipofadhaishwa, akazidi kumwasi BWANA, huyo mfalme Ahazi. 23 Maana aliitolea dhabihu miungu ya Dameski iliyompiga, akasema, Kwa sababu miungu ya wafalme wa Shamu imewasaidia wao, mimi nitaitolea dhabihu, ili inisaidie mimi. Lakini ndiyo iliyomwangamiza yeye na Israeli wote. 24 Tena Ahazi akakusanya vyombo vyote vya nyumba ya Mungu, akavikata vipande vipande vyombo vya nyumba ya Mungu, akaifunga milango ya nyumba ya BWANA; akajijengea madhabahu katika kila pembe ya Yerusalemu. 25 Na katika kila mji wa Yuda akafanya mahali pa juu pa kuifukizia miungu mingine uvumba, akamkasirisha BWANA, Mungu wa babaze. 26 Basi mambo yake yote yaliyosalia, na njia zake zote, za kwanza hadi za mwisho, tazama, yameandikwa katika Kitabu cha Wafalme wa Yuda na Israeli. 27 Ahazi akalala na babaze, wakamzika mjini, yaani, Yerusalemu; maana hawakumleta makaburini mwa wafalme wa Israeli; na Hezekia mwanawe akatawala mahali pake. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya