2 Mambo ya Nyakati 23 - Swahili Revised Union Version - SRUVDC1 Katika mwaka wa saba Yehoyada alijasiri, akawatwaa makamanda wa mamia, Azaria mwana wa Yerohamu, na Ishmaeli mwana wa Yehohanani, na Azaria mwana wa Obedi, na Maaseya mwana wa Adaya, na Elishafati mwana wa Zikri, akapatana nao. 2 Wakazunguka katikati ya Yuda, wakawakusanya Walawi kutoka katika miji yote ya Yuda, na wakuu wa nyumba za mababa wa Israeli, wakaja Yerusalemu. 3 Na kusanyiko lote wakafanya agano na mfalme nyumbani mwa Mungu. Akawaambia, Angalieni, mwana wa mfalme atatawala, kama BWANA alivyonena juu ya wana wa Daudi. 4 Hili ndilo neno mtakalolifanya; theluthi moja yenu, ninyi makuhani na Walawi mwingiao zamu siku ya sabato, mtalinda milangoni; 5 na theluthi nyumbani pa mfalme; na theluthi langoni pa msingi; na watu wote watakuwapo nyuani mwa nyumba ya BWANA. 6 Wala asiingie mtu nyumbani mwa BWANA, ila makuhani, na Walawi watumikao; hao wataingia, kwa kuwa ni watakatifu; ila watu wengine wote watafuata amri za BWANA. 7 Nao Walawi watamzunguka mfalme pande zote, kila mtu mwenye silaha zake mkononi; naye awaye yote aingiaye nyumbani na auawe; nanyi mfuatane na mfalme, aingiapo na atokapo. Yoashi atawazwa kuwa Mfalme 8 Basi Walawi na Yuda wote wakafanya kama alivyowaamuru Yehoyada kuhani; wakawatwaa kila mtu watu wake, hao watakaoingia siku ya sabato, na wale watakaotoka siku ya sabato; kwa maana Yehoyada kuhani hakuwaruhusu waondoke. 9 Naye Yehoyada kuhani akawapa makamanda wa mamia mikuki, na ngao, na vigao, vilivyokuwa vya mfalme Daudi, vilivyokuwamo nyumbani mwa Mungu. 10 Akawasimamisha watu wote, kila mtu akiwa na silaha yake mkononi, toka pembe ya kulia ya nyumba mpaka pembe ya kushoto, upande wa madhabahu na nyumba, kumzunguka mfalme pande zote. 11 Ndipo wakamleta nje mwana wa mfalme, wakamvika taji, na kumpa ule ushuhuda, wakamtawaza kuwa mfalme; Yehoyada na wanawe wakamtia mafuta, wakasema, Mfalme na aishi. Athalia auawa 12 Na Athalia alipoisikia sauti ya watu, na ya walinzi, na ya hao waliomsifu mfalme, akaingia kwa watu nyumbani mwa BWANA; 13 akatazama, na angalia, mfalme amesimama karibu na nguzo yake mlangoni, nao makamanda na wenye parapanda karibu na mfalme; wakafurahi watu wote wa nchi, wakapiga parapanda; waimbaji pia wakipiga vinanda, wakaongoza nyimbo za kusifu. Ndipo Athalia akararua mavazi yake, akasema, Uhaini! Uhaini! 14 Yehoyada kuhani akawaleta nje makamanda wa mamia, waliowekwa kuongoza jeshi, akawaambia, Mtoeni nje kati ya safu; na yeyote amfuataye, na auawe kwa upanga; kwani kuhani amesema, Msimwue katika nyumba ya BWANA. 15 Basi wakampisha njia; akaenda kwa kuingia pa mlango wa farasi nyumbani mwa mfalme; nao wakamwua huko. 16 Kisha, Yehoyada akafanya agano, yeye na watu wote, na mfalme, kwamba watakuwa watu wa BWANA. 17 Na watu wote wakaiendea nyumba ya Baali, wakaibomoa; wakavunjavunja madhabahu zake na sanamu zake, wakamwua Matani kuhani wa Baali mbele ya madhabahu. 18 Yehoyada akauamuru usimamizi wa nyumba ya BWANA chini ya mkono wa makuhani Walawi, aliowagawa Daudi nyumbani mwa BWANA, ili wazisongeze sadaka za kuteketezwa za BWANA, kama ilivyoandikwa katika Torati ya Musa, kwa kufurahi na kuimba, kama alivyoamuru Daudi. 19 Akawaweka walinzi malangoni pa nyumba ya BWANA, asiingie aliye najisi kwa namna yoyote. 20 Akawatwaa makamanda wa mamia, na watu wakubwa, na hao watawalao watu, na watu wote wa nchi, akamteremsha mfalme kutoka nyumba ya BWANA; wakalipitia lango la juu waende nyumbani kwa mfalme, wakamketisha mfalme katika kiti cha ufalme. 21 Basi wakafurahi watu wote wa nchi, na mji ukatulia baada ya Athalia kuuawa kwa upanga. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya