2 Mambo ya Nyakati 21 - Swahili Revised Union Version - SRUVDCYehoramu atawala 1 Yehoshafati akalala na babaze, akazikwa pamoja na babaze katika mji wa Daudi; Yehoramu mwanawe akatawala mahali pake. 2 Naye alikuwa na ndugu, wana wa Yehoshafati, Azaria, Yehieli, Zekaria, Azaria, Mikaeli, na Shefatia; hao wote walikuwa wana wa Yehoshafati mfalme wa Yuda. 3 Baba yao akawapa zawadi kubwa, za fedha, za dhahabu, na za tunu, pamoja na miji yenye maboma katika Yuda; lakini ufalme akampa Yehoramu, kwa sababu alikuwa mzaliwa wa kwanza. 4 Basi Yehoramu alipoinuliwa juu ya ufalme wa babaye, na kujiimarisha, akawaua nduguze wote kwa upanga, na baadhi ya wakuu wa Israeli pia. 5 Yehoramu alikuwa na umri wa miaka thelathini na miwili alipoanza kutawala, akatawala miaka minane huko Yerusalemu. 6 Akaiendea njia ya wafalme wa Israeli, kama walivyofanya nyumba ya Ahabu; kwa kuwa alikuwa amemwoa binti Ahabu; akafanya maovu machoni pa BWANA. 7 Walakini BWANA hakupenda kuiharibu nyumba ya Daudi, kwa sababu ya agano alilolifanya na Daudi, na kama alivyomwahidi kuwa atampa taa, yeye na wazao wake siku zote. Uasi wa Edomu 8 Wakati wa enzi zake Edomu wakaasi utawala wa Yuda, wakajifanyia mfalme. 9 Ndipo Yehoramu akavuka na makamanda wake, na magari yake yote pamoja naye; akaondoka usiku, akawapiga Waedomi waliomzunguka yeye na hao makamanda wa magari. 10 Hivyo Edomu wakaasi utawala wa Yuda hata leo; wakati huo uo nao Libna wakaasi utawala wake: kwa sababu alikuwa amemwacha BWANA, Mungu wa baba zake. Barua ya Eliya 11 Tena ndiye aliyetengeneza mahali pa juu katika milima ya Yuda, na kuongoza wakazi wa Yerusalemu kukosa uaminifu na kufanya Yuda ipotoke. 12 Barua kutoka nabii Eliya ilimjia, ikisema, BWANA, Mungu wa Daudi baba yako, asema hivi, Kwa kuwa hukuziendea njia za Yehoshafati baba yako, wala njia za Asa mfalme wa Yuda; 13 lakini umeiendea njia ya wafalme wa Israeli, ukawaongoza Yuda na wakazi wa Yerusalemu kwenye kukosa uaminifu, kama walivyofanya nyumba ya Ahabu; tena umewaua ndugu zako wa nyumba ya baba yako, waliokuwa wema kuliko wewe; 14 tazama, BWANA atawapiga pigo kubwa watu wako, na watoto wako, na wake zako, na mali yako yote; 15 nawe utakuwa na ugonjwa mkuu kwa maradhi ya matumbo, yatakapotokea matumbo yako kwa sababu ya ugonjwa huo siku kwa siku. 16 BWANA akawaamsha roho Wafilisti, na Waarabu walioelekeana na Wakushi juu ya Yehoramu, 17 nao wakakwea juu ya Yuda, wakaipenya, wakaichukua mali yote iliyoonekama nyumbani mwa mfalme, na wanawe pia, na wakeze; asibakizwe mtoto hata mmoja, ila Ahazia, aliyekuwa mdogo miongoni mwa wanawe. Ugonjwa na kifo cha Yehoramu 18 Na baada ya hayo yote BWANA akampiga matumbo kwa ugonjwa usioponyeka. 19 Ikawa baada ya siku, kufika mwisho wa mwaka wa pili, matumbo yake yakatokea kwa sababu ya ugonjwa wake, akafa akiwa kwenye maumivu makali. Wala watu wake hawakuwasha moto kuombolezea kifo chake kama walivyowafanyia baba zake. 20 Alikuwa na umri wa miaka thelathini na miwili alipoanza kutawala, akatawala huko Yerusalemu miaka minane; akafariki bila kutamaniwa; wakamzika mjini mwa Daudi, ila si katika makaburi ya wafalme. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya