2 Mambo ya Nyakati 19 - Swahili Revised Union Version - SRUVDC1 Yehoshafati mfalme wa Yuda akarudi Yerusalemu nyumbani kwake kwa amani. 2 Yehu mwana wa Hanani mwonaji akatoka kwenda kumlaki, akamwambia mfalme Yehoshafati, Je! Imekupasa kuwasaidia waovu, na kuwapenda wamchukiao BWANA? Kwa ajili ya hayo ghadhabu itokayo kwa BWANA i juu yako. 3 Walakini, yameonekana kiasi cha mema ndani yako, kwa kuwa umeyaondoa Maashera katika nchi, na moyo wako umeukaza kumtafuta Mungu. Matengenezo aliyoyafanya Yehoshafati 4 Na Yehoshafati akakaa Yerusalemu; akatoka tena kwenda kati ya watu toka Beer-sheba mpaka milima ya Efraimu, akawarudisha kwa BWANA, Mungu wa baba zao. 5 Akateua waamuzi katika nchi, katikati ya miji yote yenye maboma ya Yuda, mji kwa mji; 6 akawaambia hao waamuzi, Angalieni myafanyayo; kwa kuwa hammfanyii mwanadamu hukumu, ila BWANA; naye yupo pamoja nanyi katika neno la hukumu. 7 Basi sasa hofu ya BWANA na iwe juu yenu; aiweni waangalifu katika jambo mtendalo, kwa maana kwa BWANA, Mungu wetu hakuna upotoshaji wala kupendelea nafsi za watu au kupokea rushwa. 8 Tena katika Yerusalemu Yehoshafati akateua baadhi ya Walawi na makuhani, na wakuu wa jamaa za Waisraeli wawe waamuzi kwa hukumu za BWANA na kesi kati yao. Nao wakarudi Yerusalemu. 9 Akawaagiza, akasema, Ndivyo mtakavyotenda kwa hofu ya BWANA, kwa uaminifu, na kwa moyo wote. 10 Na kila mara watakapowaletea shitaka toka ndugu zenu wakaao mijini mwao, kuhusu uuaji, uvunjaji wa sheria na amri, kanuni au maagizo, mtawaonya, wasiingie hatiani mbele za BWANA, mkajiliwa na ghadhabu ninyi na ndugu zenu; fanyeni haya wala hamtakuwa na hatia. 11 Tena angalieni, Amaria, kuhani mkuu, yuko juu yenu kwa maneno yote ya BWANA; naye Zebadia, mwana wa Ishmaeli, jemadari wa nyumba ya Yuda, kwa mambo yote ya mfalme; Walawi nao watakuwa wasimamizi mbele yenu. Jitieni nguvu, mtende, naye BWANA awe pamoja nao walio wema. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya