Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

2 Mambo ya Nyakati 18 - Swahili Revised Union Version - SRUVDC


Mikaya awatabiria kushindwa

1 Basi, Yehoshafati alikuwa na mali na heshima tele, tena alifanya maridhiano ya ndoa na Ahabu.

2 Hata baada ya miaka kadhaa akamshukia Ahabu huko Samaria. Ahabu akamchinjia kondoo na ng'ombe tele, yeye na watu waliokuwa pamoja naye, akamshawishi ili apande pamoja naye waende Ramoth-gileadi.

3 Ahabu, mfalme wa Israeli, akamwambia Yehoshafati, mfalme wa Yuda, Je! Utakwenda nami mpaka Ramoth-gileadi? Akamjibu, Mimi ni kama wewe, na watu wangu kama watu wako; nasi tutakuwa pamoja nawe vitani.

4 Yehoshafati akamwambia mfalme wa Israeli, lakini kwanza umwulize BWANA ushauri.

5 Ndipo mfalme wa Israeli akawakusanya manabii, watu mia nne; akawaambia, Je! Tuende Ramoth-gileadi vitani, au niache? Wakasema, Kwea; kwa kuwa Mungu atautia mkononi mwa mfalme.

6 Lakini Yehoshafati akasema, Je! Hayupo hapa nabii mwingine wa BWANA, ili tumwulize yeye?

7 Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, Yupo mtu mmoja, ambaye tungeweza kumwuliza ya BWANA; lakini namchukia; kwa sababu hanibashirii mema kamwe, ila siku zote mabaya; naye ndiye Mikaya mwana wa Imla. Yehoshafati akasema, La! Mfalme asiseme hivyo.

8 Ndipo mfalme wa Israeli akamwita kamanda mmoja, akasema, Mlete hima Mikaya mwana wa Imla.

9 Basi, mfalme wa Israeli na Yehoshafati mfalme wa Yuda walikuwa wamekaa kila mtu katika kiti chake cha enzi, wamevaa mavazi yao, wakikaa penye kiwanja cha kupuria nafaka kwenye lango la Samaria; nao manabii wote wakafanya unabii mbele yao.

10 Na Sedekia mwana wa Kenaana akajifanyia pembe za chuma, akasema, BWANA asema hivi, Kwa hizi utawasukuma Washami, hata watakapoangamia.

11 Na manabii wote wakatoa unabii huo, wakisema, Kwea Ramoth-gileadi, ukafanikiwe, kwa kuwa BWANA atautia mkononi mwa mfalme.

12 Na yule mjumbe, aliyekwenda kumwita Mikaya, akamwambia, akasema, Angalia, maneno ya manabii kwa kupatana yasema mema kwa mfalme; neno lako basi na liwe kama mojawapo lao, ukaseme mema.

13 Mikaya akasema, Kama aishivyo BWANA, neno lile atakalolinena Mungu wangu, ndilo nitakalolinena.

14 Na alipokuja kwa mfalme, mfalme akamwambia, Je! Mikaya, tuende Ramoth-gileadi vitani, au niache? Akasema, Kweeni, mkafanikiwe; nao watatiwa mikononi mwenu.

15 Mfalme akamwambia, Mara ngapi nikuapishe, usiniambie neno ila yaliyo kweli, kwa jina la BWANA?

16 Akasema, Niliwaona Waisraeli wote wametawanyika milimani, kama kondoo wasio na mchungaji; BWANA akasema, Hawa hawana bwana; na warudi kila mtu nyumbani kwake kwa amani.

17 Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, Je! Sikukuambia, hatanibashiria mema, ila mabaya?

18 Mikaya akasema, Sikieni basi neno la BWANA; Nilimwona BWANA ameketi katika kiti chake cha enzi na jeshi lote la mbinguni wamesimama mkono wake wa kulia na wa kushoto.

19 BWANA akasema, Ni nani atakayemdanganya Ahabu mfalme wa Israeli, ili akwee Ramoth-gileadi akaanguke? Basi huyu akasema hivi; na huyu hivi.

20 Akatoka pepo, akasimama mbele za BWANA, akasema, Mimi nitamdanganya. BWANA akamwambia, Jinsi gani?

21 Akasema, Nitaondoka, na kuwa pepo wa uongo vinywani mwa manabii wake wote. Akasema, Utamdanganya, na kufanikiwa pia; ondoka, ukafanye hivyo.

22 Basi sasa, angalia, BWANA ametia pepo wa uongo vinywani mwa manabii wako hawa; naye BWANA amenena mabaya juu yako.

23 Ndipo akakaribia Sedekia mwana wa Kenaana, akampiga Mikaya kofi la shavu, akasema, Alitokaje kwangu Roho ya BWANA ili aseme na wewe?

24 Mikaya akasema, Angalia utaona siku ile, utakapoingia katika chumba cha ndani ili ujifiche.

25 Mfalme wa Israeli akasema, Mchukueni Mikaya mkamrudishe kwa Amoni mkuu wa mji, na kwa Yoashi mwana wa mfalme;

26 mkaseme, Mfalme asema hivi, Mtieni huyu gerezani, mkamlishe chakula cha shida, na maji ya shida, hadi nitakaporudi kwa amani.

27 Mikaya akasema, Ukirudi kabisa kwa amani, BWANA hakusema kupitia kwangu. Akasema, Sikieni, enyi watu wote.


Kushindwa kwa Ahabu na kifo chake

28 Basi mfalme wa Israeli na Yehoshafati mfalme wa Yuda wakakwea mpaka Ramoth-gileadi.

29 Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, Nitajibadilisha, na kuingia vitani; lakini wewe uvae mavazi yako. Mfalme wa Israeli akajibadilisha; nao wakaingia vitani.

30 Basi mfalme wa Shamu alikuwa amewaamuru makamanda wa magari yake, akisema, Msipigane na mdogo wala mkuu, ila na mfalme wa Israeli peke yake.

31 Ikawa makamanda wa magari walipomwona Yehoshafati, wakasema, Mfalme wa Israeli ni huyu. Basi wakamgeukia ili wapigane naye; lakini Yehoshafati akalia, na BWANA akamsaidia; Mungu akawaondoa kwake.

32 Ikawa, makamanda wa magari walipoona ya kuwa siye mfalme wa Israeli, wakageuka nyuma wasimfuate.

33 Na mtu mmoja akavuta upinde kwa kubahatisha, akampiga mfalme wa Israeli mahali pa kuungana mavazi yake ya chuma; kwa hiyo akamwambia mwendesha gari, Geuza gari, uniondoe katika vita; kwa kuwa nimejeruhiwa sana.

34 Pigano likazidi siku ile; lakini mfalme wa Israeli akajitegemeza garini juu ya Washami hata jioni; akafa kama wakati wa kuchwa kwa jua.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo