Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

2 Mambo ya Nyakati 16 - Swahili Revised Union Version - SRUVDC


Muungano na Aramu walaumiwa

1 Katika mwaka wa thelathini na sita wa kutawala kwake Asa, Baasha mfalme wa Israeli alipanda juu ya Yuda, akaujenga Rama, ili asimwache mtu yeyote kutoka wala kuingia kwa Asa mfalme wa Yuda.

2 Ndipo Asa akatoa fedha na dhahabu katika hazina za nyumba ya BWANA, na nyumba ya mfalme, akampelekea Ben-hadadi mfalme wa Shamu, aliyekaa Dameski, akasema,

3 Na pawepo agano la kushirikiana kati yangu na wewe kama lilivyokuwa kati ya baba yangu na baba yako; tazama, nimekutumia fedha na dhahabu; basi, uvunje mkataba wako na Baasha, mfalme wa Israeli, ili aache kunishambulia.

4 Naye Ben-hadadi akamsikiliza mfalme Asa, akawatuma makamanda wa majeshi yake juu ya miji ya Israeli; wakapiga Iyoni, na Dani, na Abel-maimu, na miji ya hazina yote ya Naftali.

5 Baasha aliposikia habari hiyo, akaacha kuujenga Rama, akaifunga kazi yake.

6 Ndipo mfalme Asa akawatwaa Yuda wote; nao wakayachukua mawe ya Rama, na miti yake, aliyoijengea Baasha; naye akajenga kwa vitu hivyo Geba na Mispa.

7 Wakati huo Hanani mwonaji akamwendea Asa mfalme wa Yuda, akamwambia, Kwa kuwa umemtegemea mfalme wa Shamu, wala hukumtegemea BWANA, Mungu wako, kwa hiyo limekutoka jeshi la mfalme wa Shamu mkononi mwako.

8 Je! Hao Wakushi na Walubi hawakuwa jeshi kubwa mno, wenye magari na wapanda farasi wengi sana? Lakini, kwa kuwa ulimtegemea BWANA, aliwatia mkononi mwako.

9 Kwa maana macho ya BWANA hukimbia kimbia duniani kote, ili ajionesha kuwa mwenye nguvu kwa ajili ya hao, waliokamilika moyo kuelekea kwake. Kwa hayo umetenda upumbavu; kwani tangu sasa utakuwa na vita.

10 Ndipo Asa akamkasirikia mwonaji, akamtia katika nyumba ya magandalo gerezani, maana amemghadhibikia kwa sababu ya neno hilo. Na wakati uleule Asa akatesa baadhi ya watu.


Ugonjwa na kifo cha mfalme Asa

11 Na tazama, mambo yake Asa, toka mwanzo hadi mwisho, angalia, yameandikwa katika kitabu cha wafalme wa Yuda na Israeli.

12 Katika mwaka wa thelathini na tisa wa kumiliki kwake, Asa akashikwa na ugonjwa wa miguu; ugonjwa wake ukazidi sana; lakini hakumtafuta BWANA katika ugonjwa wake, bali alitafuta msaada wa waganga.

13 Asa akalala na babaze, akafa katika mwaka wa arubaini na mmoja wa kumiliki kwake.

14 Wakamzika katika makaburi yake mwenyewe, aliyojichimbia katika mji wa Daudi, wakamlaza juu ya kitanda kilichojazwa manukato, na kila namna ya machanganyiko ya hao mafundi wa dawa; wakawasha moto mkubwa sana kwa heshima yake.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo