Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

2 Mambo ya Nyakati 14 - Swahili Revised Union Version - SRUVDC


Asa atawala

1 Basi Abiya akalala na baba zake, wakamzika mjini mwa Daudi, akatawala Asa mwanawe mahali pake; katika siku zake nchi ikastarehe miaka kumi.

2 Basi, Asa akafanya yaliyo mema, yaliyo ya adili, machoni pa BWANA, Mungu wake;

3 maana aliziondoa madhabahu za kigeni, na mahali pa juu, akazivunja nguzo, akayakatakata maashera;

4 akawaamuru Yuda wamtafute BWANA, Mungu wa baba zao, na kuzitenda torati na amri.

5 Tena akaondoa kutoka miji yote ya Yuda mahali pa juu na sanamu za jua; ufalme ukastarehe mbele yake.

6 Akajenga miji yenye maboma katika Yuda; kwa kuwa nchi ilikuwa imestarehe, wala hakuwa na vita miaka ile; kwa sababu BWANA alimpa amani.

7 Naye akawaambia Yuda, Na tuijenge miji hii, na kuizungushia maboma, na minara, na malango, na makomeo; nchi bado ingali ipo mbele yetu, kwa kuwa tumemtafuta BWANA, Mungu wetu; naam, tumemtafuta, naye amemstarehesha pande zote. Basi wakajenga, wakafanikiwa.

8 Naye Asa alikuwa na jeshi waliochukua ngao na mikuki, katika Yuda elfu mia tatu; na katika Benyamini wenye kuchukua vigao na kupinda upinde, elfu mia mbili na themanini; hao wote walikuwa mashujaa.


Uvamizi wa Kushi wazimwa

9 Kisha, Zera Mkushi alikuja kuwashambulia akiwa na jeshi la watu milioni moja na magari mia tatu akaja Maresha.

10 Asa akatoka kukutana naye, wakapanga vita Maresha bondeni mwa Sefatha.

11 Naye Asa akamlilia BWANA, Mungu wake, akasema, BWANA, hapana kuliko wewe aliye wa kusaidia, kati yake yeye aliye hodari, na yeye asiye na nguvu; utusaidie, Ee BWANA, Mungu wetu; kwa kuwa sisi twakutegemea wewe, na kwa jina lako tumekuja juu ya jamii kubwa hii. Ee BWANA, wewe ndiwe Mungu wetu, asikushinde mwanadamu.

12 Basi, BWANA akawapiga Wakushi mbele ya Asa, na mbele ya Yuda; na Wakushi wakakimbia.

13 Asa na watu waliokuwa pamoja naye wakawafuata mpaka Gerari; wakawaua Wakushi wengi sana asipone hata mmoja; kwa sababu waliangamizwa mbele za BWANA, na mbele ya jeshi lake; na hao wakachukua mateka wengi sana.

14 Wakaipiga miji yote kandokando ya Gerari; maana hofu ya BWANA ikawajia; nao wakaiteka nyara miji yote, kwa maana zilikuwamo ndani yake nyara nyingi mno.

15 Wakazipiga pia hema za ng'ombe, wakachukua kondoo wengi na ngamia, wakarudi Yerusalemu.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo