Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

2 Mambo ya Nyakati 11 - Swahili Revised Union Version - SRUVDC


Yuda na Benyamini wajiimarisha

1 Hata Rehoboamu alipofika Yerusalemu, akakusanya nyumba ya Yuda na Benyamini, watu wateule elfu mia moja na themanini waliokuwa hodari, watu wa vita, ili wapigane juu ya Israeli, ili wamrudishie Rehoboamu huo ufalme.

2 Lakini neno la BWANA likamjia Shemaya mtu wa Mungu, kusema,

3 Mwambie Rehoboamu mwana wa Sulemani, mfalme wa Yuda, uwaambie na Israeli wote waliomo Yuda na Benyamini, ukisema,

4 BWANA asema hivi, Hamtapanda wala kupigana na ndugu zenu; rudini kila mtu nyumbani kwake; kwa kuwa jambo hili limetoka kwangu. Basi wakayatii maneno ya BWANA wakarudi wasiende kupigana na Yeroboamu.

5 Naye Rehoboamu akakaa Yerusalemu, akajenga miji yenye ngome katika Yuda.

6 Akajenga Bethlehemu, Etamu, Tekoa,

7 Beth-suri, Soko, Adulamu,

8 Gathi, Maresha, Zifu,

9 Adoraimu, Lakishi, Azeka,

10 Sora, Aiyaloni, na Hebroni, iliyoko katika Yuda na Benyamini, miji yenye maboma.

11 Akazifanya imara hizo ngome, akaweka majemadari humo, na akiba ya vyakula, na mafuta, na mvinyo.

12 Na ndani ya miji yote mmoja mmoja aliweka ngao na mikuki, akaifanya kuwa na nguvu nyingi mno. Yuda na Benyamini ikawa milki yake.


Makuhani na Walawi aamuunga Rehoboamu mkono

13 Makuhani na Walawi waliokuwa katika Israeli yote wakamwendea, kutoka maeneo yao yote.

14 Walawi wakaacha malisho yao, na milki yao, wakaja Yuda na Yerusalemu; kwa sababu Yeroboamu na wanawe waliwakataza, ili wasimfanyie BWANA ukuhani;

15 naye akajiwekea makuhani wa mahali pa juu, na wa wale majini, na wa zile ndama alizozitengeneza.

16 Na kutoka katika kabila zote za Israeli, wakaandamwa na hao waliojikaza nia kumtafuta BWANA, Mungu wa Israeli, wakaja Yerusalemu, ili wamtolee dhabihu BWANA, Mungu wa baba zao.

17 Hivyo wakaufanya imara kwa miaka mitatu ufalme wa Yuda, na kumtia nguvu Rehoboamu mwana wa Sulemani; kwa maana muda wa miaka mitatu wakaiendea njia ya Daudi na Sulemani.


Ndoa za Rehoboamu

18 Rehoboamu akaoa mke, Mahalathi binti Yerimothi mwana wa Daudi, na wa Abihaili binti Eliabu, mwana wa Yese;

19 akamzalia wana, Yeushi, na Shemaria, na Zahamu.

20 Kisha baada yake akamwoa Maaka, binti Absalomu; na yeye akamzalia Abiya, na Atai, na Ziza, na Shelomithi.

21 Rehoboamu akampenda Maaka binti Absalomu kuliko wakeze wote na masuria yake; (maana alioa wake kumi na wanane, na masuria sitini, akazaa watoto wa kiume ishirini na wanane na mabinti sitini).

22 Rehoboamu akamteua Abiya, mwana wa Maaka, kuwa mkuu, mtawala kati ya nduguze, kwa kuwa aliazimia kumtawaza awe mfalme.

23 Akafanya kwa akili, akawatawanya wanawe wote kati ya nchi zote za Yuda na Benyamini, katika kila mji wenye boma; akawapa vyakula tele. Akawatafutia wake wengi.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo