2 Mambo ya Nyakati 10 - Swahili Revised Union Version - SRUVDCUasi juu ya Rehoboamu 1 Rehoboamu akaenda Shekemu; maana Israeli wote walikuwa wamekuja Shekemu, ili wamfanye mfalme. 2 Ikawa Yeroboamu mwana wa Nebati aliposikia tendo hilo (maana alikuwa Misri, alikokwenda alipomkimbia mfalme Sulemani) Yeroboamu akarudi kutoka Misri. 3 Wakatuma ujumbe, wakamwita, Yeroboamu akaja na Israeli wote, wakamwambia Rehoboamu, wakasema, 4 Baba yako alilifanya zito kongwa letu; basi sasa upunguze utumwa mgumu wa baba yako, na kongwa lake zito alilotutwika, nasi tutakutumikia. 5 Akawaambia, Mnirudie baada ya siku tatu. Watu wakaenda zao. 6 Mfalme Rehoboamu akataka shauri kwa wazee, waliosimama mbele ya Sulemani baba yake, alipokuwa hai bado, akasema, Mnanipa shauri gani la kuwajibu watu hawa? 7 Wakamwambia, wakasema, Ukiwa mwema kwao watu hawa, na kuwapendeza, na kuwaambia maneno mazuri, hapo watakuwa watumishi wako siku zote. 8 Lakini akaliacha shauri lile la wazee walilompa, akataka shauri kwa wale vijana wa rika yake, waliokuwa washauri wake. 9 Akawaambia, Je! Mwanipa shauri gani la kuwajibu watu hawa, waliosema nami, wakisema, kongwa alilotutwika baba yako utufanyie liwe jepesi. 10 Na wale vijana waliokua pamoja naye wakamwambia, wakasema, Uwaambie hivi watu wale waliosema nawe, wakinena, Baba yako alilifanya kongwa letu kuwa zito, lakini wewe tufanyie jepesi; uwaambie hivi, Kidole changu cha mwisho ni kinene kuliko kiuno cha baba yangu. 11 Basi kama baba yangu aliwatwika kongwa zito, mimi nitaongeza kongwa lenu; baba yangu aliwapiga kwa mijeledi, lakini mimi nitawapiga kwa nge. 12 Basi Yeroboamu na watu wote wakamjia Rehoboamu siku ya tatu, kama mfalme alivyoamuru, akisema, Mnirudie siku ya tatu. 13 Mfalme akawajibu kwa ukali; mfalme Rehoboamu akaliacha shauri la wazee, akasema nao kwa shauri la vijana, 14 akinena, Baba yangu aliwafanyia kongwa zito, nami nitawaongezea; baba yangu aliwapiga kwa mijeledi, lakini mimi nitawapiga kwa nge. 15 Basi mfalme hakuwasikia watu wale; maana jambo hili lilitoka kwa Mungu, ili alithibitishe neno lake alilomwambia Yeroboamu mwana wa Nebati kwa mkono wa Ahiya Mshiloni. 16 Basi Israeli wote walipoona ya kuwa mfalme hawasikilizi, watu wakamjibu mfalme, wakasema, Tuna sehemu gani katika Daudi? Wala hatuna urithi katika mwana wa Yese; kila mtu aende zake hemani, enyi Israeli, sasa itunze nyumba yako mwenyewe ewe Daudi. Basi wakaenda zao Israeli wote hemani kwao. 17 Lakini kuhusu wana wa Israeli waliokaa katika miji ya Yuda, Rehoboamu alitawala juu yao. 18 Ndipo mfalme Rehoboamu akamtuma Adoramu, msimamizi wa shokoa; nao wana wa Israeli wakampiga kwa mawe hadi akafa. Mfalme Rehoboamu akafanya haraka kupanda garini mwake, ili akimbilie Yerusalemu. 19 Hivyo Israeli wakaasi juu ya nyumba ya Daudi, hata leo. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya