2 Mambo ya Nyakati 1 - Swahili Revised Union Version - SRUVDCSulemani aomba hekima 1 Basi Sulemani, mwana wa Daudi, alijiimarisha katika ufalme wake, naye BWANA, Mungu wake, alikuwa pamoja naye, akamtukuza mno. 2 Sulemani akawaita Israeli wote, na makamanda wa maelfu, na wa mamia, na waamuzi, na kila kiongozi wa Israeli, na wakuu wa familia. 3 Basi Sulemani akaenda mahali pa juu pa Gibeoni, na kusanyiko lote naye; kwani ndipo lilipokuwako hema la kukutania la Mungu, alilolifanya Musa mtumishi wa BWANA jangwani. 4 Lakini sanduku la Mungu, Daudi alikuwa amelipandisha kutoka Kiriath-yearimu mpaka mahali Daudi alipolitengenezea; maana amelitandia hema katika Yerusalemu. 5 Tena madhabahu ya shaba, aliyoifanya Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, ilikuwako huko mbele ya maskani ya BWANA; Sulemani na kusanyiko wakaiendea. 6 Sulemani akaipandia huko madhabahu ya shaba mbele za BWANA, iliyokuwako hemani pa kukutania, akatoa sadaka elfu moja za kuteketezwa juu yake. 7 Usiku ule Mungu akamtokea Sulemani, akamwambia, Omba utakalo nikupe. 8 Sulemani akamwambia Mungu, Umemfanyia baba yangu Daudi fadhili kuu, nawe umenimilikisha mimi badala yake. 9 Basi sasa, Ee BWANA Mungu, na limyakinie baba yangu Daudi neno lako; maana umenitawaza niwe mfalme juu ya watu wengi kama mavumbi ya nchi. 10 Basi sasa nipe hekima na maarifa, nijue kutoka na kuingia mbele ya watu hawa; kwa kuwa ni nani awezaye kuwatawala watu wako hawa walio wengi? 11 Naye Mungu akamwambia Sulemani, Kwa sababu neno hili lilikuwamo moyoni mwako, wala hukujitakia mali, wala utajiri, wala utukufu, wala maisha ya wakuchukiao, wala hukujitakia maisha ya siku nyingi; bali umejitakia hekima na maarifa, upate kuwatawala watu wangu, niliokutawaza juu yao; 12 basi hekima na maarifa umepewa; nami nitakupa mali, na utajiri, na utukufu, kupita walivyokuwa navyo wafalme wote waliokuwa kabla yako, wala baada yako hapatakuwa na mtu atakayekuwa navyo. 13 Basi Sulemani akatoka mahali pa juu pa Gibeoni, toka mbele ya Hema la kukutania, akaja mpaka Yerusalemu; akatawala Israeli. Shughuli za jeshi na biashara za mfalme Sulemani 14 Sulemani akakusanya magari na wapandao farasi; naye alikuwa na magari elfu moja na mia nne, na wapandao farasi elfu kumi na mbili, aliowaweka katika miji ya magari, na pamoja na mfalme huko Yerusalemu. 15 Mfalme akafanya fedha na dhahabu kuwa kama mawe humo Yerusalemu, na mierezi akaifanya kuwa kama mikuyu iliyomo Shefela, kwa kuwa mingi. 16 Nao farasi, aliokuwa nao Sulemani wakaletwa toka Misri; wakapewa wafanya biashara wake mfalme kwa makundi; kila kundi na thamani yake. 17 Nao walipandisha na kununua gari kutoka Misri kwa shekeli mia sita za fedha; na farasi kwa mia moja na hamsini, vivyo hivyo wakawauzia wafalme wote Wahiti na wafalme wa Shamu. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya