1 Wathesalonike 5 - Swahili Revised Union Version - SRUVDC1 Lakini, ndugu, kuhusu nyakati na majira, hamna haja niwaandikie. 2 Maana ninyi wenyewe mnajua hakika ya kuwa siku ya Bwana yaja kama vile mwizi ajavyo usiku. 3 Wakati wasemapo, Kuna amani na salama, ndipo uharibifu uwajiapo kwa ghafla, kama vile uchungu umjiavyo mwenye mimba, wala hakika hawataokolewa. 4 Bali ninyi, ndugu, hamko gizani, hata siku ile iwapate kama mwizi. 5 Kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa nuru, na wana wa mchana; sisi si wa usiku, wala wa giza. 6 Basi tusilale usingizi kama wengine, bali tukeshe, na kuwa na kiasi. 7 Maana walalao usingizi hulala usiku, pia na walewao hulewa usiku. 8 Lakini sisi tulio wa mchana, tuwe na kiasi, hali tukijivika kifuani imani na upendo, na chapeo yetu iwe tumaini la wokovu. 9 Kwa kuwa Mungu hakutuweka ili tupate hasira yake, bali ili tupate wokovu, kwa Bwana wetu Yesu Kristo; 10 ambaye alikufa kwa ajili yetu, ili tuishi pamoja naye, iwe tunakesha au tunalala. 11 Basi, farijianeni na kujengana kila mtu na mwenzake, hakika kama mnavyofanya. Mausia ya mwisho, salamu na baraka 12 Lakini, ndugu, tunataka mwatambue wale wanaojitaabisha kwa ajili yenu, na kuwasimamia ninyi katika Bwana, na kuwaonyeni; 13 mkawastahi sana katika upendo, kwa ajili ya kazi zao. Iweni na amani ninyi kwa ninyi. 14 Ndugu, tunawasihi, waonyeni wale wasiokaa kwa utaratibu; watieni moyo walio dhaifu; watieni nguvu wanyonge; vumilieni na watu wote. 15 Angalieni mtu awaye yote asimlipe mwenziwe mabaya kwa mabaya; bali siku zote lifuateni lililo jema, ninyi kwa ninyi na kwa watu wote. 16 Furahini siku zote; 17 ombeni bila kukoma; 18 shukuruni kwa kila jambo; maana hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo Yesu. 19 Msimzimishe Roho; 20 msitweze unabii; 21 jaribuni mambo yote; lishikeni lililo jema; 22 jitengeni na ubaya wa kila namna. 23 Mungu wa amani mwenyewe awatakase kabisa; nanyi nafsi zenu na roho zenu na miili yenu mhifadhiwe muwe kamili, bila lawama, wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo. 24 Yeye ni mwaminifu ambaye awaita, naye atafanya. 25 Ndugu, tuombeeni. 26 Wasalimieni ndugu wote kwa busu takatifu. 27 Nawaapisha kwa Bwana, ndugu wote wasomewe waraka huu. 28 Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na iwe pamoja nanyi. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya