1 Wathesalonike 1 - Swahili Revised Union Version - SRUVDCSalamu 1 Paulo, Silwano na Timotheo, kwa kanisa la Wathesalonike, lililo katika Mungu Baba, na katika Bwana Yesu Kristo. Neema na iwe kwenu na amani. Imani na kielelezo cha Wathesalonike 2 Twamshukuru Mungu siku zote kwa ajili yenu nyote, tukiwataja katika maombi yetu. 3 Wala hatuachi kuikumbuka kazi yenu ya imani, na taabu yenu ya upendo, na subira yenu ya tumaini lililo katika Bwana wetu Yesu Kristo, mbele za Mungu Baba yetu. 4 Kwa maana, ndugu mnaopendwa na Mungu, tunajua uteule wenu; 5 ya kwamba Injili yetu haikuwafikia katika maneno tu, bali na katika nguvu, na katika Roho Mtakatifu, na uthibitifu mwingi; kama vile mnavyojua jinsi zilivyokuwa tabia zetu kwenu, kwa ajili yenu. 6 Nanyi mkawa wafuasi wetu na wa Bwana, mkiisha kulipokea neno katika dhiki nyingi, pamoja na furaha ya Roho Mtakatifu. 7 Hata mkawa kielelezo kwa watu wote waaminio katika Makedonia, na katika Akaya. 8 Maana kutoka kwenu neno la Mungu limevuma, si katika Makedonia na Akaya tu, ila na kila mahali imani yenu mliyo nayo kwa Mungu imeenea; hata hatuna haja sisi kunena lolote. 9 Kwa kuwa wao wenyewe wanatangaza habari zetu, jinsi kulivyokuwa kuingia kwetu kwenu; na jinsi mlivyomgeukia Mungu mkaziacha sanamu, ili kumtumikia Mungu aliye hai, wa kweli; 10 na kumngojea Mwanawe kutoka mbinguni, ambaye alimfufua katika wafu, naye ni Yesu, mwenye kutuokoa kutoka kwa ghadhabu itakayokuja. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya