1 Wakorintho 16 - Swahili Revised Union Version - SRUVDCMichango kwa watakatifu 1 Kuhusu ile michango kwa ajili ya watakatifu, kama vile nilivyoamuru makanisa ya Galatia, nanyi fanyeni vivyo hivyo. 2 Siku ya kwanza ya juma kila mmoja wenu na aweke akiba kwake, kwa kadiri ya kufanikiwa kwake; ili kwamba michango isifanyike hapo nitakapokuja; 3 nami nitakapofika nitawatuma kwa barua wale mtakaowachagua, wachukue hisani yenu mpaka Yerusalemu. 4 Na kama ikifaa niende na mimi, watasafiri pamoja nami. Mipango ya usafiri 5 Lakini nitakuja kwenu, nikiisha kupita kati ya Makedonia; maana napita kati ya Makedonia. 6 Labda nitakaa kwenu; naam, labda wakati wote wa baridi, mpate kunisafirisha kokote nitakakokwenda. 7 Maana sipendi kuonana nanyi sasa, katika kupita tu, kwa sababu natarajia kukaa kwenu muda kidogo, Bwana akinijalia. 8 Lakini nitakaa Efeso hadi siku ya Pentekoste; 9 kwa maana nimefunguliwa mlango mkubwa wa kufaa sana, na wako wengi wanipingao. 10 Lakini, Timotheo akija, angalieni akae kwenu pasipo hofu; maana anaifanya kazi ya Bwana vile vile kama mimi mwenyewe; 11 basi mtu yeyote asimdharau, lakini msafirisheni kwa amani, ili aje kwangu; maana ninamtazamia pamoja na ndugu zetu. 12 Lakini kuhusu Apolo, ndugu yetu, nilimsihi sana aje kwenu pamoja na hao ndugu; ambaye si mapenzi yake kwenda sasa; lakini atakuja atakapopata nafasi. Wasia wa mwisho na salamu 13 Kesheni, simameni imara katika imani, iweni na ujasiri, mkawe hodari. 14 Mambo yenu yote na yatendeke katika upendo. 15 Tena ndugu, nawasihi; (mnawajua watu wa nyumbani mwa Stefana kwamba ni malimbuko ya Akaya, nao wamejitia katika kazi ya kuwahudumia watakatifu); 16 watiini watu kama hawa, na kila mtu afanyaye kazi pamoja nao, na kujitaabisha. 17 Nami nafurahi kwa sababu ya kuja kwao Stefana na Fortunato na Akaiko; maana hawa wamenikirimia kwa wingi yale niliyopungukiwa kwenu. 18 Maana wameniburudisha roho yangu, na roho zenu pia; basi wajueni sana watu kama hao. 19 Makanisa ya Asia wawasalimu. Akila na Priska wawasalimu sana katika Bwana, pamoja na kanisa lililoko ndani ya nyumba yao. 20 Ndugu wote wawasalimu. Salimianeni kwa busu takatifu. 21 Hii ni salamu yangu Paulo kwa mkono wangu mwenyewe. 22 Mtu awaye yote asiyempenda Bwana, na awe amelaaniwa. Maranatha. 23 Neema ya Bwana Yesu na iwe pamoja nanyi. 24 Pendo langu na liwe pamoja nanyi nyote katika Kristo Yesu. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya