Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni
- Matangazo -

1 Petro 1 - Swahili Revised Union Version - SRUVDC


Salamu

1 Petro, mtume wa Yesu Kristo, kwa wateule wa Utawanyiko, wakaao hali ya ugeni katika Ponto, na Galatia, na Kapadokia, na Asia, na Bithinia;

2 kama vile Mungu Baba alivyotangulia kuwajua katika kutakaswa na Roho, hata mkapata kutii na kunyunyiziwa damu ya Yesu Kristo. Neema na amani na ziongezwe kwenu.


Tumaini hai

3 Ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa rehema zake nyingi alituzaa mara ya pili ili tupate tumaini lenye uzima kwa kufufuka kwake Yesu Kristo katika wafu;

4 tupate na urithi usioharibika, usio na uchafu, usionyauka, uliotunzwa mbinguni kwa ajili yenu.

5 Nanyi mnalindwa na nguvu za Mungu kwa njia ya imani ili mpate wokovu ulio tayari kufunuliwa wakati wa mwisho.

6 Mnafurahi sana wakati huo, ijapokuwa sasa kwa muda mfupi, ikiwa ni lazima, mmehuzunishwa kwa majaribu ya namna mbalimbali;

7 ili kwamba kujaribiwa kwa imani yenu, ambayo ina thamani kuu kuliko dhahabu ipoteayo, ijapokuwa hiyo hujaribiwa kwa moto, kuonekane kuwa kwenye sifa na utukufu na heshima, katika kufunuliwa kwake Yesu Kristo.

8 Naye mwampenda, ijapokuwa hamkumwona; ambaye ijapokuwa hamumwoni sasa, mnamwamini; na kufurahi sana, kwa furaha isiyoneneka, yenye utukufu,

9 katika kuupokea mwisho wa imani yenu, yaani, wokovu wa roho zenu.

10 Kuhusu wokovu huo, manabii ambao walitabiri habari za neema itakayowafikia ninyi, walichunguza sana.

11 Wakatafuta ni wakati upi, na wakati wa namna gani ulioonywa na Roho wa Kristo aliyekuwa ndani yao, ambaye alitangulia kuyashuhudia mateso yatakayompata Kristo, na utukufu utakaokuwako baada ya hayo.

12 Wakafunuliwa ya kuwa si kwa ajili yao wenyewe, bali kwa ajili yenu walihudumu katika mambo hayo, ambayo sasa yamehubiriwa kwenu na wale waliowahubiria ninyi Injili kwa Roho Mtakatifu aliyetumwa kutoka mbinguni. Mambo hayo malaika wanatamani kuyaona.


Wito wa kuishi maisha ya utakatifu

13 Kwa hiyo iweni tayari, na makini; mkiitumainia kwa utimilifu ile neema mtakayoletewa katika ufunuo wake Yesu Kristo.

14 Kama watoto wa kutii msijifananishe na tamaa zenu za kwanza za ujinga wenu;

15 bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote;

16 kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu.

17 Na ikiwa mnamwita Baba, yeye ahukumuye kila mtu pasipo upendeleo, kwa kadiri ya kazi yake, nendeni kwa hofu katika wakati wenu wa kukaa hapa kama wageni.

18 Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu;

19 bali kwa damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na dosari wala waa, yaani, ya Kristo.

20 Naye amejulikana kweli tangu zamani, kabla haijawekwa misingi ya dunia; lakini alifunuliwa siku hizi za mwisho kwa ajili yenu;

21 na kupitia kwake mmekuwa wenye kumwamini Mungu, aliyemfufua katika wafu akampa utukufu; hata imani yenu na tumaini lenu liwe kwa Mungu.

22 Mkiisha kujitakasa roho zenu kwa kuitii kweli, hata kuufikia upendano wa ndugu usio na unafiki, basi jitahidini kupendana kwa moyo safi.

23 Kwa kuwa mmezaliwa mara ya pili; si kwa mbegu iharibikayo, bali kwa ile isiyoharibika; kwa neno la Mungu lenye uzima, linalodumu hata milele.

24 Maana, Mwili wote ni kama majani, Na fahari yake yote ni kama ua la majani. Majani hukauka na ua lake huanguka;

25 Bali Neno la Bwana hudumu hata milele. Na neno hilo ni neno lile jema lililohubiriwa kwenu.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo