1 Mambo ya Nyakati 29 - Swahili Revised Union Version - SRUVDCMatoleo kwa ujenzi wa hekalu 1 Kisha mfalme Daudi akawaambia kusanyiko lote, Sulemani mwanangu, ambaye Mungu amemchagua peke yake, angali ni mchanga bado na hana uzoefu, nayo kazi hii ni kubwa; kwani nyumba hii ya enzi si kwa mwanadamu, ila kwa BWANA, Mungu. 2 Basi kwa uwezo wangu wote nimeiwekea akiba nyumba ya Mungu wangu, dhahabu kwa vitu vya dhahabu, na fedha kwa vitu vya fedha, na shaba kwa vitu vya shaba, na chuma kwa vitu vya chuma, na miti kwa vitu vya miti; vito vya shohamu, na vya kujazia, vito vya njumu, na vya rangi mbalimbali, na mawe ya thamani ya kila namna, na marumaru tele. 3 Nami tena kwa kuwa nimeiwekea nyumba ya Mungu wangu shauku yangu, nami ninayo hazina yangu mwenyewe ya dhahabu na fedha, ninaitoa kwa ajili ya nyumba ya Mungu wangu, zaidi ya hiyo akiba niliyoiwekea tayari nyumba takatifu; 4 yaani, talanta elfu tatu za dhahabu, za dhahabu ya Ofiri, na talanta elfu saba za fedha iliyosafika, ya kuzifunikiza kuta za nyumba; 5 ya dhahabu, kwa vitu vya dhahabu, na ya fedha kwa vitu vya fedha, na kwa kazi za kila namna zitakazofanywa kwa mikono ya mafundi. Ni nani basi ajitoaye kwa moyo ili ajiweke wakfu leo kwa BWANA? 6 Ndipo wakuu wa koo za mababa, na wakuu wa makabila ya Israeli, na makamanda wa maelfu na wa mamia, pamoja na wasimamizi wa kazi ya mfalme, wakajitoa kwa hiari yao; 7 nao wakatoa, kwa ajili ya utumishi wa nyumba ya Mungu, dhahabu talanta elfu tano, na darkoni elfu kumi, na fedha talanta elfu kumi, na shaba talanta elfu kumi na nane, na chuma talanta elfu mia moja. 8 Na wale walioonekana kuwa na vito vya thamani wakavitoa vitiwe katika hazina ya nyumba ya BWANA, chini ya mkono wa Yehieli, Mgershoni. 9 Ndipo hao watu wakafurahi, kwa sababu wametoa kwa hiari yao wenyewe, kwa moyo wao wote, kwa hiari yao wenyewe, wamemtolea BWANA; mfalme Daudi naye akafurahi sana. Daudi amshukuru Mungu 10 Kwa hiyo Daudi akamhimidi BWANA, mbele ya mkutano wote; naye Daudi akasema, Uhimidiwe, Ee BWANA, Mungu wa Israeli baba yetu, milele na milele. 11 Ee BWANA, ukuu ni wako, na uweza, na utukufu, na ushindi, na enzi; maana vitu vyote vilivyo mbinguni na duniani ni vyako; ufalme ni wako, Ee BWANA, nawe umetukuzwa, u mkuu juu ya vitu vyote. 12 Utajiri na heshima hutoka kwako wewe, nawe watawala juu ya vyote; na mkononi mwako mna uweza na nguvu; tena mkononi mwako mna kuwatukuza na kuwawezesha wote. 13 Basi sasa, Mungu wetu, tunakushukuru na kulisifu jina lako tukufu. 14 Lakini mimi ni nani, na watu wangu ni nani, hata tuweze kutoa kwa hiari hivi? Kwani vitu vyote vyatoka kwako na katika vitu vyako mwenyewe tumekutolea. 15 Kwani sisi tu wageni na wapitaji mbele zako, kama walivyokuwa baba zetu wote; siku zetu duniani ni kama kivuli, na hakuna tumaini la kuishi. 16 Ee BWANA, Mungu wetu, akiba hii yote tuliyoiweka, ili tukujengee nyumba kwa ajili ya jina lako takatifu, yote inatoka mkononi mwako, na yote ni yako wewe. 17 Nami ninajua, Mungu wangu, ya kuwa wewe wajaribu moyo, nawe wapendezwa na unyofu. Nami katika unyofu wa moyo wangu nimeyatoa haya yote kwa hiari yangu mwenyewe; nami sasa nimeona kwa furaha watu wako, waliopo hapa, wakikutolea kwa hiari yao. 18 Ee BWANA, Mungu wa Abrahamu, na wa Isaka, na wa Israeli, baba zetu, ulidumishe jambo hili milele katika fikira za mawazo ya mioyo ya watu wako, ukaiongoze mioyo yao kwako; 19 naye Sulemani mwanangu, umjalie ili kwa moyo wote, azishike amri zako, na shuhuda zako, na maagizo yako, akayatende hayo yote na kuijenga nyumba hii ya enzi, niliyoiwekea akiba. 20 Ndipo Daudi akawaambia kusanyiko lote, Haya, mhimidini BWANA, Mungu wenu. Basi kusanyiko lote wakamhimidi BWANA, Mungu wa baba zao, wakainamisha vichwa vyao, wakamsujudia BWANA, na mfalme naye. Sulemani atawazwa kuwa mfalme 21 Siku ya pili yake, wakamtolea BWANA dhabihu, wakamchinjia BWANA sadaka ya kuteketezwa, yaani, ng'ombe elfu moja, na kondoo dume elfu moja, na wana-kondoo elfu moja, pamoja na sadaka zao za vinywaji, na dhabihu nyingi kwa ajili ya Israeli wote; 22 wakala na kunywa mbele za BWANA siku ile, kwa furaha kuu. Wakamtawaza Sulemani, mwana wa Daudi, mara ya pili, wakamtia mafuta mbele za BWANA, awe mkuu, na Sadoki awe kuhani. 23 Ndipo Sulemani akaketi katika kiti cha enzi cha BWANA, awe mfalme badala ya Daudi babaye, akafanikiwa; nao Israeli wote wakamtii. 24 Nao wakuu wote, na mashujaa, na wana wote wa mfalme Daudi nao, wakaahidi kuwa watiifu kwa mfalme Sulemani. 25 Naye BWANA akamtukuza Sulemani mno machoni pa Israeli wote, akampa fahari ya kifalme ya kumpita mfalme awaye yote aliyekuwa kabla yake katika Israeli. Muhtasari wa utawala wa Daudi 26 Basi Daudi, mwana wa Yese, akawa mfalme juu ya Israeli wote. 27 Na wakati aliotawala juu ya Israeli, ulikuwa miaka arubaini; miaka saba alitawala Hebroni, na miaka thelathini na mitatu akatawala Yerusalemu. 28 Akafa akiwa mzee sana, mwenye maisha marefu, mali na heshima; naye Sulemani mwanawe akatawala badala yake. 29 Basi habari za mfalme Daudi, mwanzo hadi mwisho, angalia, zimeandikwa katika kumbukumbu za Samweli, mwonaji, na katika kumbukumbu za Nathani, nabii, na katika kumbukumbu za Gadi, mwonaji; 30 zikisimulia kuhusu kutawala kwake kote na nguvu zake, na mambo yote yaliyompata yeye, na Israeli, na falme zote za nchi. |
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Bible Society of Kenya