Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni

- Matangazo -

1 Mambo ya Nyakati 14 - Swahili Revised Union Version - SRUVDC


Daudi ajiimarisha katika Yerusalemu

1 Naye Hiramu, mfalme wa Tiro, akatuma wajumbe kwa Daudi, akampelekea na mierezi, na waashi, na maseremala, ili wamjengee nyumba.

2 Daudi akajua ya kwamba BWANA amemweka imara ili atawale Israeli, na kwamba milki yake imetukuka zaidi kwa ajili ya watu wake Israeli.

3 Tena Daudi akazidi kuoa wake huko Yerusalemu; akazidi kuzaa wana na binti.

4 Na haya ndiyo majina ya watoto aliozaliwa huko Yerusalemu; Shamua, na Shobabu, na Nathani, na Sulemani;

5 na Ibhari, na Elishua, na Elpeleti;

6 na Noga, na Nefegi, na Yafia;

7 na Elishama, na Eliada, na Elifeleti.


Kushindwa kwa Wafilisti

8 Wafilisti waliposikia ya kwamba Daudi ametiwa mafuta ili awe mfalme wa Israeli wote, Wafilisti wote wakapanda kumtafuta Daudi; naye Daudi akasikia, akatoka nje kupigana nao.

9 Basi hao Wafilisti walikuwa wamekuja na kujitawanya katika bonde la Warefai.

10 Daudi akamwuliza Mungu, akisema, Je! Nipande juu ya Wafilisti! Utawatia mikononi mwangu? Naye BWANA akamwambia, Panda; kwa kuwa nitawatia mikononi mwako.

11 Basi wakapanda mpaka Baal-perasimu, Daudi naye akawapiga huko; Daudi akasema, BWANA amewafurikia adui zangu kwa mkono wangu, kama mafuriko ya maji. Basi wakapaita mahali pale jina lake Baal-perasimu.

12 Nao wakaiacha miungu yao huko; naye Daudi akaamuru, ikateketezwa kwa moto.

13 Lakini hao Wafilisti wakajitawanya tena mara ya pili bondeni.

14 Na Daudi akamwuliza Mungu tena; naye Mungu akamwambia, Hutapanda kuwafuata; zunguka mbali nao, na kuwajia ukielekea miforsadi.

15 Kisha itakuwa utakapoisikia sauti ya kwenda katika vilele vya miforsadi, ndipo utakapokwenda nje vitani; kwa maana ndipo Mungu ametoka mbele yako, awapige jeshi la Wafilisti.

16 Daudi akafanya kama vile Mungu alivyomwamuru; wakawapiga jeshi la Wafilisti toka Geba mpaka Gezeri.

17 Sifa za Daudi zikafika nchi zote; naye BWANA akawaletea mataifa yote hofu yake.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.

Bible Society of Kenya
Tufuate:



Matangazo