Yohana 5 - New Testament in Swahili (Zanzibar) Revised Edition 19211 BAADA ya haya palikuwa na siku kuu ya Wayahudi; Yesu akapanda kwenda Yerusalemi. 2 Na huko Yerusalemi penye mlango wa kondoo pana birika, iitwayo kwa Kiehrania Bethesda, nayo ina matao matano. 3 Ndani ya hayo jamii kubwa ya wagonjwa walikuwa wamelala, vipofu, viwete, na waliopooza, wakingoja maji yachemke. 4 Kwa maana kuna wakati malaika hushuka akaiingia ile birika, akayatibua maji: bassi yeye aliyeingia kwanza baada ya maji kutibuliwa, akaponea ugonjwa wote uliokuwa umempata. 5 Na huko palikuwa na mtu, amekuwa hawezi muda wa miaka thelathini na minane. 6 Yesu alipomwona huyu amelala, akijua ya kuwa amekuwa hali hii siku nyingi, akamwambia, Wataka kuwa nizima? 7 Yule mgonjwa akamjibu, Bwana, sina mtu wa kunitia birikani, maji yanapotibuliwa; bali wakati ninapokuja mimi, mtu mwingine hushuka mbele yangu. 8 Yesu akamwambia, Simama, jitwike kitanda chako, ukaende. 9 Marra yule mtu akawa mzima, akajitwika kitanda chake, akaenda. Bassi ilikuwa sabato siku ile. 10 Kwa sababu hiyo Wayahudi wakamwambia yule aliyeponywa, Leo ni sabato, si halali kwako kujitwika kitanda chako. 11 Akawajibu, Yeye aliyenifanya kuwa mzima, ndiye aliyeniambia, Jitwike kitanda chako, ukaende. 12 Bassi wakamwuliza, Yule mtu aliyekuambia, Jitwike kitanda chako ukaende, ni nani? 13 Lakini yule aliyeponywa, hakujua ni nani; maana Yesu amejitenga, kwa sababu palikuwa na watu wengi mahali pale. 14 Baada ya haya Yesu akamkuta ndani ya hekalu, akamwambia, Angalia, umekuwa mzima: usitencle dhambi tena, jambo lililo baya zaidi lisije likakupata. 15 Yule mtu akaenda zake, akawapasha Wayahudi khabari ya kwamba Yesu ndiye aliyemfanya kuwa mzima. 16 Kwa sababu hiyo Wayahudi wakaanza kumwudhi Yesu, wakitaka kumwua, kwa kuwa alitenda haya siku ya sabato. 17 Yesu akawajibu, Baba yangu anatenda kazi hatta sasa, nami ninatenda kazi. 18 Bassi kwa sababu hii Wayahudi wakazidi kutaka kumwua, kwa kuwa hakuivunja sabato tu, bali pamoja na haya alimwita Mungu Baba yake, akijifanya sawa na Mungu. 19 Bassi Yesu akajibu, akawaambia, Amin, amin, nawaambieni, Mwana hawezi kutenda neno kwa nafsi yake, illa lile amwonalo Baba analitenda; kwa maana yote atendayo yeye, hayo na Mwana ayatenda vilevile. 20 Maana Baba ampenda Mwana, amwonyesha yote ayatendayo mwenyewe; na kazi kubwa zaidi kuliko hizi atamwonyesha illi ninyi mpate kustaajabu. 21 Maana kama Baba awafufuavyo wafu na kuwahuisha, vivyo hivyo na Mwana awahuisha awatakao. 22 Maana Baba hamhukumu mtu aliye yote, bali amempa Mwana hukumu yote; 23 illi wote wamheshimu Mwana kama wanavyomheshimu Baba. Asiyemheshimu Mwana, hamheshimu Baba aliyempeleka. 24 Amin, amin, nawaambieni, Alisikiae neno langu na kumwamini yeye aliyenipeleka ana uzima wa milele, wala hafiki hukumuni, bali amepita toka mauti hatta uzima. 25 Amin, amin, nawaambieni, Saa inakuja, na sasa ipo, wafu watakapoisikia sauti ya Mwana wa Mungu, na wale waisikiao watakuwa hayi. 26 Maana kama vile Baba alivyo na uzima nafsini mwake, vivyo hivyo alimpa na Mwana kuwa na uzima nafsini mwake; 27 akampa mamlaka ya kufanya hukumu kwa sababu yu Mwana wa Adamu. 28 Msistaajabie haya: kwa maana saa inakuja, ambayo watu wote waliomo makaburini watakapoisikia sauti yake, nao watatoka: 29 wale waliofanya mema kwa ufufuo wa uzima, na wale waliofanya manyonge kwa ufufuo wa hukumu. 30 Mimi siwezi kufanya neno kwa nafsi yangu: kama nisikiavyo ndivyo nihukumuvyo, na hukumu yangu ina haki: kwa sababu siyatafuti mapenzi yangu mwenyewe, bali mapenzi yake Baba aliyenipeleka. 31 Mimi nikijishuhudia nafsi yangu, ushuhuda wangu si kweli. 32 Yuko mwingine anaenishuhudia; nami najua ya kuwa ushuhuda wake anaonishuhudia ni kweli. 33 Ninyi mlituma watu kwa Yohana, akaishuhudia kweli. 34 Lakini mimi sipokei ushuhuda kwa wana Adamu; walakini ninasema haya illi ninyi mpate kuokoka. 35 Yeye alikuwa taa iwakayo na kuangaza, na ninyi mlipenda kuishangilia nuru yake kitambo. 36 Lakini ushuhuda nilio nao ni mkubwa kuliko ule wa Yohana: kwa kuwa zile kazi nilizopewa na Baba nizimalize, kazi hizo zenyeye ninazozitenda zinanishuhudia kwamba Baba amenituma. 37 Nae Baba aliyenipeleka amenishuhudia. Sauti yake hamkuisikia wakati wo wote, wala sura yake hamkuiona. 38 Na neno lake hamnalo likikaa ndani yenu, kwa kuwa ninyi hamwamini yeye alivetumwa nae. 39 Mwayachunguza maandiko, kwa sababu mnadhani kwamba ninyi mna uzima wa milele ndani yake: na hayo ndiyo yanayonishuhudia: 40 wala hamtaki kuja kwangu, mpate kuwa na uzima. 41 Sipokei utukufu kwa wana Adamu. 42 Walakini nimewajua ninyi ya kuwa hamna upendo wa Mungu ndani yenu. 43 Mimi nimekuja kwa jina la Baba yangu, nanyi hamnipokei: mwingine akija kwa jina lake mwenyewe mtampokea huyo. 44 Mwawezaje kuamini ninyi mnaopokezanya utukufu ninyi kwa ninyi, na utukufu ule utokao kwa Mungu aliye wa pekee hamwutafuti? 45 Msidhani kwamba mimi nitawashitaki kwa Baba: yuko anaewashitaki, yaani Musa, mnaemtumaini ninyi. 46 Kwa maana kama mngalimwamini Musa, mngeniamini mimi; maana yeye aliandika khahari zangu. 47 Illakini msipoyaamini maandiko yake, mtayaaminije maneno yangu? |
Swahili New Testament © Bible Society of Tanzania, 1921.
Bible Society of Tanzania