Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni

- Matangazo -

Yohana 21 - New Testament in Swahili (Zanzibar) Revised Edition 1921

1 BAADA ya haya Yesu alijionyesha tena kwa wanafunzi wake, penye bahari ya Tiberia; nae alijionyesha hivi.

2 Simon Petro, na Tomaso aitwae Didumo, na Nathanael wa Kana wa Galilaya, na wana wa Zebedayo, na watu wengine wawili katika wanafunzi wake, walikuwa mahali pamoja.

3 Simon Petro akawaambia, Ninakwenda kuvua samaki. Wakamwambia, Na sisi tutakwenda pamoja nawe. Wakatoka, wakapanda chomboni; na usiku ule hawakupata kitu.

4 Hatta assubuhi kulipokucha, Yesu akasimama ufukoni, walakini wanafunzi hawakujua ya kuwa ni Yesu.

5 Bassi Yesu akawaambia, Wanangu, mna kitoweo? Wakamjibu, Hapana.

6 Akawaambia, Litupeni jarife upande wa kuume wa chombo, nanyi mtapata. Bassi wakatupa, wala hawakuweza kulivuta tena kwa sababu ya wingi wa samaki.

7 Bassi mwanafunzi yule ambae Yesu alimpenda akamwambia Petro, Ndiye Bwana. Bassi Simon Petro, aliposikia ya kwamba ni Bwana, akajifunga vazi lake (maana alikuwa uchi), akajitupa baharini.

8 Wanafunzi wengine wakaja katika mashua (maana hawakuwa mbali ya inchi kavu, illa yapata dhiraa miateen) wakilikokota jarife lenye samaki.

9 Bassi waliposhuka pwani, wakaona moto wa makaa huko, na kitoweo kimetiwa juu yake, na mkate.

10 Yesu akawaambia, Leteni hapa baadhi ya samaki mlizozivua sasa hivi.

11 Bassi Simon Petro akapanda chomboni, akalivuta jarife pwani, limejaa samaki kubwa, mia na khamsini na tatu: na ijapokuwa zilikuwa nyingi namna hii, jarife halikupasuka. Yesu akawaambia, Njoni mle.

12 Wala hapana mtu katika wale wanafunzi aliyethubutu kumwuliza, Wewe nani? wakijua ya kuwa ni Bwana.

13 Yesu akaenda akautwaa mkate, akawapa, na kitoweo vivyo hivyo.

14 Hii ndiyo marra ya tatu Yesu alionekana na wanafunzi wake baada ya kufufuka katika wafu.

15 Bassi walipokwisha kula, Yesu akamwambia Simon Petro, Simon wa Yohana, wanipenda kuliko bawa? Akamwambia, Naam, Bwana; wewe wajua ya kuwa nakupenda. Akamwambia, Lisha wana kondoo wangu.

16 Akamwambia marra ya pili, Simon wa Yohana, wanipenda? Akamwambia, Naam, Bwana; wewe wajua ya kuwa nakupenda. Akamwambia, Chunga kondoo zangu.

17 Akamwambia marra ya tatu, Simon wa Yohana, Wanipenda mimi? Petro akahuzunika kwa kuwa alimwambia marra ya tatu, Wanipenda mimi? Akamwambia, Bwana, wewe unajua yote; unajua ya kuwa nakupenda. Yesu amwambia, Lisha kondoo zangu.

18 Amin, amin, nakuambia, Ulipokuwa kijana, ulikuwa ukijifunga, ukienda ulikotaka; utakapokuwa mzee, utanyosha mikono yako, na mwingine atakufunga, atakuchukua usikotaka.

19 Akasema hili kwa kuonyesha ni mauti gani atakayomtukuza Mungu. Na akiisha kusema haya, akamwambia, Nifuate.

20 Na Petro akigeuka, akamwona mwanafunzi yule aliyependwa na Yesu akifuata; yeye ndiye aliyeegamia kifuani pake wakati wa kula chakula cha jioni na kusema, Bwana yu nani akusalitiye?

21 Petro akimwona huyu, akamwambia Yesu, Bwana, na huyu je?

22 Yesu akamwambia, Nikitaka huyu akae hatta nijapo imekukhusu nini? wewe unifuate mimi.

23 Bassi neno hili lilienea katika ndugu kwamba mwanafunzi yule hafi: walakini Yesu hakumwambia, Hafi; bali, Nikitaka akae hatta nijapo imekukhusu nini?

24 Huyu ndiye mwanafunzi ayashuhudiae haya, na aliyeandika haya; na twajua ya kuwa ushuhuda wake ni wa kweli.

25 Kuna na mengine mengi aliyoyafanya Yesu, nayo yakiandikwa moja moja, nadhani hatta ulimwengu wote usingetosha kwa vitabu vitakavyoandikwa. Amin.

Swahili New Testament © Bible Society of Tanzania, 1921.

Bible Society of Tanzania
Tufuate:



Matangazo