Yohana 20 - New Testament in Swahili (Zanzibar) Revised Edition 19211 HATTA siku ya kwanza ya sabato Mariamu Magdalene akaenda kaburini alfajiri, kungali giza bado, akaliona jiwe limeondolewa kaburini. 2 Bassi akaenda mbio hatta kwa Simon Petro, na kwa mwanafunzi yule mwingine aliyependwa na Yesu, akawaambia, Wamemwondoa Bwana kaburini, wala hatujui walikomweka. 3 Bassi Petro akatoka, na mwanafunzi yule mwingine, wakashika njia kwenda kaburini. 4 Wakaenda mbio wawili pamoja: yule mwanafunzi mwingine akaenda mbio upesi kuliko Petro, akawa wa kwanza wa kufika kaburini; 5 akainama, akaviona vitambaa vimewekwa; illakini hakuingia. 6 Bassi akaja na Simon Petro, akimfuata, akaingia kaburini; akavitazama vitambaa vimewekwa, 7 na ile leso iliyokuwa kichwani pake, haikuwekwa pamoja na vitambaa, bali imekunjwa, na kuwekwa mahali pa peke yake. 8 Bassi ndipo akaingia nae mwanafunzi yule mwingine aliyekuwa wa kwanza wa kufika kaburini, akaona, akaamini. 9 Kwa maana hawajalifahamu andiko bado, kwamba imempasa kufufuka. 10 Bassi wanafunzi wale wakaenda zao nyumbani kwao. 11 Lakini Mariamu alikuwa amesimama karibu na kaburi, nje yake, analia; bassi, akilia hivi, akainama, akachungulia ndani ya kaburi; 12 akaona malaika wawili, wenye mavazi meupe, wameketi, mmoja kichwani, na mmoja miguuni, hapo ulipowekwa mwili wa Yesu. 13 Nao wakamwambia, Bibi, unalilia nini? Akawaambia, Kwa sababu wamemwondoa Bwana wangu, wala sijui walikomweka. 14 Alipokwisha kusema haya, akageuka nyuma, akamwona Yesu amesimama, asijue ya kuwa ni Yesu. 15 Yesu akamwambia, Bibi, unalilia nini? Unamtafuta nani? Yeye, akidhani ya kuwa ni mtunza bustani, akamwambia, Bwana, kama umemchukua wewe, niambie ulipomweka, nami nitamwondoa. 16 Yesu akamwambia, Mariamu. Yeye akageuka, akamwambia kwa Kiebrania, Rabboni (tafsiri yake Mwalimu). 17 Yesu akamwambia, Usiniguse; kwa maana sijapaa kwa Baba yangu. Lakini enenda kwa ndugu zangu, ukawaambie, Ninapaa kwa Baba yangu na Baba yenu, kwa Mungu wangu na Mungu wenu. 18 Mariamu Magdalene akaenda akawapasha wanafunzi khabari ya kwamba amemwona Bwana, na ya kwamba amemwambia haya. 19 Ikawa jioni katika siku ile ya kwanza ya sabato, na milango imefungwa walipokuwapo wanafunzi kwa khofu ya Wayahudi, akaja Yesu, akasimama katikati, akawaambia, Amani kwenu. 20 Akiisha kusema haya, akawaonyesha mikono yake na ubavu wake. Bassi wanafunzi wakafurahi walipomwona Bwana. 21 Bassi Yesu akawaambia marra ya pili, Amani kwenu; kama Baba alivyonipeleka, nami nawatuma ninyi. 22 Akiisha kusema haya, akawapulizia, akawaambia, Pokeeni Roho Mtakatifu. 23 Wo wote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wo wote mtakaowafungia, wamefungiwa. 24 Tomaso, mmoja wa wathenashara aitwae Didumo, hakuwako pamoja nao alipokuja Yesu. 25 Bassi wanafunzi wengine wakamwambia, Tumemwona Bwana. Akawaambia, Nisipoona mikononi mwake alama za misumari, na kutia kidole changu katika alama za misumari, na kutia mkono wangu uhavuni mwake, sitaamini kabisa. 26 Baada ya siku nane wanafunzi wake walikuwamo ndani marra ya pili, na Tomaso pamoja nao. Yesu akaja, milango imefungwa, akasimama katikati, akasema, Amani kwenu. 27 Akiisha akamwambia Tomaso, Lete hapa kidole chako, ukatazame mikono yangu; kalete mkono wako, uutie katika ubavu wangu; wala nsiwe asiyeamini, bali aaminiye. 28 Tomaso akajibu, akamwambia, Bwana wangu, na Mungu wangu. 29 Yesu amwambia, Kwa kuwa umeniona, umeamini; wa kheri wasioona wakaamini. 30 Bassi ziko ishara nyingine nyingi alizozifanya Yesu mbele ya wanafunzi wake, zisizoandikwa katika kitabu hiki; 31 lakini hizi zimeandikwa mpate kuamini kwamba Yesu ni Kristo, Mwana wa Mungu; na kwa kuamini mwe na uzima kwa jina lake. |
Swahili New Testament © Bible Society of Tanzania, 1921.
Bible Society of Tanzania