Yohana 2 - New Testament in Swahili (Zanzibar) Revised Edition 19211 NA siku ya tatu palikuwa arusi katika Kana ya Galilaya, na mama yake Yesu alikuwako. 2 Yesu nae akaitwa pamoja na wanafunzi wake arusini. 3 Hatta divai ilipowatindikia, mama yake Yesu akamwambia, Hawana divai. 4 Yesu akamwambia, Bibi, ina nini mimi nawe? Saa yangu haijawadia. 5 Mama yake akawaambia watumishi, Lo lote atakalowaambieni fanyeni. 6 Palikuwako mabalasi sita ya mawe, yamewekwa huko kwa desturi ya kutawaza kwao Wayahudi, killa moja lapata kadiri ya nzio mbili au tatu. 7 Yesu akawaambia, Jalizeni mabalasi maji. Wakayajaliza hatta juu. 8 Akawaambia, Sasa tekeni, mpelekeeni mkuu wa meza. Wakapeleka. 9 Mkuu wa meza alipoyaonja maji yaliyofanyika kuwa divai, asijue ilikotoka, (lakini watumishi walijua walioyateka maji), mkuu wa meza akamwita bwana arusi, 10 akamwambia, Killa mtu kwanza huandaa divai iliyo njema, hatta watu wakiisha kunywa sana, ndipo huleta iliyo dhaifu: wewe umeweka divai iliyo njema hatta sasa. 11 Mwanzo huu wa ishara Yesu alifanya Kana ya Galilaya, akauonyesha utukufu wake, wanafunzi wake wakamwamini. 12 Baada ya haya akashuka hatta Kapernaum, yeye na mama yake na ndugu zake na wanafunzi wake: wakakaa huko siku chache. 13 Na Pasaka ya Wayahudi ilikuwa karibu: Yesu akapanda hatta Yerusalemi. 14 Akaona hekaluni watu waliokuwa wakiuza ngʼombe na kondoo na njiwa, na wenye kuvunja fedha wameketi; 15 Akafanya mjeledi kwa kambaa akawatoa wote katika hekalu, na kondoo, na ngʼombe, akamwaga fedha yao wenye kuvunja fedha, akazipindua meza zao; 16 akawaambia wale waliokuwa wakiuza njiwa, Yaondoem haya: msiifanye nyumba ya Baba yangu kuwa nyumba ya biashara. 17 Wanafunzi wake wakakumbuka ya kuwa imeandikwa, Wivu wa nyumba yako umenila. 18 Bassi Wayahudi wakajibu wakamwambia, Ishara gani utuonyeshayo, iwapo unafanya haya? 19 Yesu akajibu, akawaambia, Livunjeni hekalu hii, nami kwa siku tatu nitaisimamisha. 20 Bassi Wayahudi wakasema, Hekalu hii ilijengwa katika muda wa miaka arubaini na sita, nawe utaisimamisha kwa siku tatu? 21 Lakini yeye alinena khabari za hekalu ya mwili wake. 22 Bassi alipofufuliwa katika wafu, wanafunzi wake wakakumbuka ya kuwa amenena neno hili, wakaliamini lile andiko na lile neno alilolinena Yesu. 23 Hatta alipokuwapo Yerusalemi wakati wa Pasaka katika siku kuu, watu wengi wakaliamini jina lake, wakiona ishara zake alizozifanya. 24 Lakini Yesu hakujiaminisha kwao, kwa kuwa yeye aliwajua wote; 25 na kwa sababu hakuwa na haja ya watu kushuhudia khabari za niwana Adamu; kwa maana yeye mwenyewe alijua yaliyomo ndani ya mwana Adamu. |
Swahili New Testament © Bible Society of Tanzania, 1921.
Bible Society of Tanzania