Yohana 14 - New Testament in Swahili (Zanzibar) Revised Edition 19211 MSIFADHAIKE mioyo yenu; mnamwamini Mungu, niaminini na mimi. 2 Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambieni; nashika njia kwenda kuwaandalia mahali. 3 Bassi nikishika njia kwenda kuwaandalia mahali, nitakuja tena, niwakaribisheni kwangu; illi nilipo mimi, nanyi mwepo. 4 Na mimi niendako, mwaijua njia. 5 Tomaso akamwambia, Bwana, hatujui uendako; twaijuaje njia? 6 Yesu akamwambia, Ndimi niliye njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba bila kwa mimi. 7 Kama mngalinijua mimi, mngalimjua na Baba; tangu sasa mnamjua, tena mmemwona. 8 Filipo akamwambia, Bwana, tuonyeshe Baba, yatutosha. 9 Yesu akamwambia, Nimekuwa pamoja nanyi siku hizi zote wala hukunijua, Filipo? Aliyeniona mimi, amemwona Baba; wasemaje wewe, Tuonyeshe Baba? 10 Huamini ya kwamba mimi ni ndani ya Baba, na Baba ndani yangu? Maneno niwaambiayo mimi, sisemi kwa shauri langu tu; lakini Baba akaae ndani yangu huzifanya kazi zake. 11 Niaminini ya kwamba mimi ni ndani ya Baba, na Baba ndani yangu; la! hamwamini hivyo, niaminini kwa sababu ya kazi zenyewe. 12 Amin, amin, nawaambieni, Aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo mimi na yeye atazifanya; atafanya na kubwa kuliko hizi, kwa kuwa nashika njia kwenda kwa Baba. 13 Na mkiomba lo lote kwa jina langu, hili nitalifanya, Baba atukuzwe ndani ya Mwana. 14 Mkiomba neno kwa jina langu, hili nitalifanya. 15 Mkinipenda mtazishika amri zangu. 16 Na mimi nitamwomba Baba, nae atawapa Mfariji mwingine, akaae nanyi hatta milele, 17 Roho ya kweli; ambae ulimwengu hauwezi kumkubali, kwa kuwa haumwoni wala haumjui: bali ninyi mnamjua; maana anakaa kwenu, nae atakuwa ndani yenu. 18 Sitawaacha ninyi yatima; naja kwenu. 19 Bado kidogo na ulimwengu haunioni tena; bali ninyi mnaniona; kwa sababu mimi ni hayi, ninyi nanyi mtakuwa hayi. 20 Katika siku ile mtajua ninyi, ya kuwa mimi ni ndani ya Baba yangu, na ninyi ndani yangu, na mimi ndani yenu. 21 Aliye na amri zangu, na kuzishika, yeye ndiye anipendae; nae anipendae atapendwa na Baba yangu, nami nitampenda, na kujidhihirisha kwake. 22 Yuda akamwambia (siye Iskariote), Bwana, imekuwaje, ya kwamba wataka kujidhihirisha kwetu, wala si kwa ulimwengu? 23 Yesu akajibu akamwambia, Mtu akinipenda, atalishika neno langu; na Baba yangu atampenda, nasi tutakuja kwake, na kufanya makao kwake. 24 Asiyenipenda, hayashiki maneno yangu; na neno mnalolisikia silo langu, bali lake Baba aliyenipeleka. 25 Haya nimewaambia, nikikaa kwenu. 26 Lakini Mfariji, Roho Mtakatifu, ambae Baba atampeleka kwa jina langu, yeye atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia. 27 Amani nawaachieni; amani yangu nawatolea; si kama ulimwengu utoavyo, mimi nawatolea. Msifadhaike moyo wenu, wala msiwe na woga. 28 Mlisikia ya kwamba mimi naliwaambia, Nakwenda zangu, tena naja kwenu. Kama mngalinipenda, mngalifurahi, kwa sababu nashika njia kwenda kwa Baba: kwa maana Baba ni mkuu kuliko mimi. 29 Na sasa nimewaambieni kabla haijawa, kusudi iwapo, mwamini. 30 Sitasema nanyi maneno mengi tena, kwa maana mkuu wa ulimwengu anakuja, wala hana kitu kwangu: 31 lakini ulimwengu ujue ya kuwa nampenda Baba; na, kama Baba alivyoniamuru, ndivyo nifanyavyo. Ondokeni, tufoke huku. |
Swahili New Testament © Bible Society of Tanzania, 1921.
Bible Society of Tanzania