Yohana 1 - New Testament in Swahili (Zanzibar) Revised Edition 19211 MWANZO alikuwako Neno, nae Neno alikuwako kwa Mungu, nae Neno alikuwa Mungu. 2 Huyu mwanzo alikuwako kwa Mungu. 3 Vyote vyalifanyika kwa huyu. Wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika. 4 Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, nao uzima ulikuwa nuru ya watu, 5 nayo nuru yangʼaa gizani, wala giza halikuiweza. 6 Palitokea mtu ametumwa kutoka kwa Mungu, jina lake Yohana. 7 Huyu alikuja kwa ushuhuda, illi aishuhudie nuru, wote wapate kuamini kwa yeye. 8 Huyu hakuwa ile nuru, illakini aishuhudie ile nuru. 9 Kulikuwako nuru halisi, imtiayo nuru killa mtu ajae katika ulimwengu. 10 Alikuwako ulimwenguni, ulimwengu umepata kuwa kwa veye, wala ulimwengu haukumtambua. 11 Alikuja kwake, nao walio wake hawakumpokea. 12 Bali wote waliompokea aliwapa mamlaka ya kufanyika watoto wa Mungu, ndio waliaminio jina lake: 13 waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu. 14 Nae Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu, tukautazama utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee akitoka kwa Baba, amejaa neema na kweli. 15 Yohana akamshuhudia, akapaaza sauti yake, akinena, Huyu ndiye niliyemnena khabari zake, kwamba, Ajae nyuma yangu amekuwa mbele yangu; kwa maana alikuwa kabla yangu. 16 Na katika ujazi wake sisi sote tulipokea, na neema juu ya neema. 17 Kwa kuwa torati ilitolewa kwa mkono wa Musa, neema na kweli zilikuwa kwa mkono wa Yesu Kristo. 18 Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wo wote, Mwana wa pekee aliye katika kifua cha Baba, huyu ndiye aliyefasiri khabari yake. 19 Na huu ndio ushuhuda wake Yohana, Wayahudi walipotuma makuhani na Walawi toka Yerusalemi wamwulize, Wewe u nani? 20 Nae aliungama wala hakukana; aliungama, Mimi siye Kristo. 21 Wakamwuliza, Nini bassi? U Eliya wewe? Akanena, Mimi siye. Wewe u nabii yule? Akajibu, La. 22 Bassi wakamwambia, U nani? tuwape majibu waliotupeleka. Wajinenaje? 23 Akasema, Mimi ni sauti ya mtu apaazae sauti jangwani, Inyosheni njia ya Bwana! kama alivyonena nabii Isaya. 24 Nao waliotumwa walitoka kwa Mafarisayo. 25 Wakamwuliza, wakimwambia, Mbona bassi wabatiza, kama wewe si Kristo, wala Eliya, wala nabii yule? 26 Yohana akawajibu akanena, Mimi nabatiza kwa maji: kati mwenu amesimama msiyemjua ninyi. 27 Ndiye ajae nyuma yangu, aliyekuwa mbele yangu, wala mimi sistahili niilegeze gidam ya kiatu chake. 28 Haya yalifanyika Bethania ngʼambu ya Yardani, alikokuwako Yohana akibatiza. 29 Siku ya pili yake Yohana amwona Yesu anakuja kwake, akanena, Tazama, Mwana Kondoo wa Mungu, aichukuae dhambi ya ulimwengu! 30 Huyu ndiye niliyemnena khabari zake, Yuaja mtu nyuma yangu, aliyekuwa mbele yangu, kwa maana alikuwa kabla yangu. 31 Nami sikumjua: lakini kusudi adhibirishwe kwa Israeli ndio maana nalikuja nikibatiza kwa maji. 32 Yohana akashuhudu, akasema, Nimemwona Roho akishuka, kama hua, kutoka mbinguni; akakaa juu yake. 33 Nami sikumjua, lakini yeye aliyenipeleka kubatiza kwa maji, huyu aliniambia, Yeye ambae utakaemwona Roho akishuka na kukaa juu yake, huyu ndiye abatizae kwa Roho Mtakatifu. 34 Nami nimeona, tena nimeshuhudia ya kuwa huyu ni Mwana wa Mungu. 35 Tena siku ya pili yake Yohana alikuwa amesimama na wawili katika wanafunzi wake. 36 Akamtazama Yesu, akitembea, akasema, Tazama, Mwana Kondoo wa Mungu! 37 Wale wanafunzi wawili wakamsikia akinena, wakamfuata Yesu. Yesu akageuka, akawaona wakifuata: akawaambia, Mnatafuta nini? 38 Wakamwambia, Rabbi (tafsiri yake, Mwalimu), unakaa wapi? Akawaambia, Njoni muone. 39 Wakaenda, wakaona akaapo, wakakaa kwake siku ile. Ilikuwa karibu na saa kumi. 40 Andrea, ndugu ya Simon Petro, alikuwa mmoja wa wale wawili waliomsikia Yohana na kumfuata. 41 Huyu akamwona kwanza Simon, ndugu yake mwenyewe, akamwambia, Tumemwona Masihi, (tafsiri yake Kristo). 42 Akampeleka kwa Yesu. Yesu akamtazama, akasema, Wewe Simon, mwana wa Yona, utakwitwa Kefa (tafsiri yake, Petro). 43 Siku ya pili yake Yesu akataka kuondoka kwenda Galilaya, akamwona Filipo, akamwambia, Nifuate. 44 Nae Filipo alikuwa mtu wa Bethsaida, mtu wa mji wa Andrea na Petro. 45 Filipo akamwona Nathanaeli, akamwambia, Tumemwona yeye aliyeandikiwa na Musa katika torati, na na manabii, Yesu, mwana wa Yusuf, mtu wa Nazareti 46 Nathanaeli akamwambia, Chaweza kitu chema kutoka Nazareti? Filipo akamwambia, Njoo uone. 47 Yesu akamwona Nathanaeli akija kwake, akamtaja khabari zake, Tazama, huyu ni Mwisraeli kweli kweli, hamna hila ndani yake. 48 Nathanaeli akamwambia, Umepataje kunijua? Yesu akajibu, akamwambia, Kabla Filipo hajakuita, ulipokuwa chini ya mtini, nalikuona. 49 Nathanaeli akajibu, akamwambia, Rabbi, wewe u Mwana wa Mungu, ndiwe mfalme wa Israeli. 50 Yesu akajibu, akamwambia, Kwa sababu nalikuambla, Nalikuona chini ya mtini, waamini? Utaona mambo makubwa kuliko haya. 51 Akamwambia, Amin, amin, nakuambieni, Tangu sasa mtaziona mbingu zimefunguka, na malaika wa Mungu wakipanda, wakishuka juu ya Mwana wa Adamu. |
Swahili New Testament © Bible Society of Tanzania, 1921.
Bible Society of Tanzania