Yakobo 2 - New Testament in Swahili (Zanzibar) Revised Edition 19211 NDUGU zangu, msiwe na imani ya Bwana wetu Yesu Kristo, Bwana mwenye utukufu, kwa kupendelea watu. 2 Maana akiingia katika sunagogi lenu mtu mwenye pete ya dhahabu na mavazi mazuri, na akiingia na maskini, mwenye mavazi mabovu; 3 nanyi mkimstahi yule aliyevaa mavazi mazuri, na kumwambia, Keti wewe hapa mahali pazuri, na kumwambia yule maskini, Simama wewe pale, au keti miguuni pangu, 4 je! hamkufanya ihtilafu mioyoni mwenu mkawa waamuzi wenye mawazo mabovu? 5 Sikihzeni, ndugu niwapendao, Mungu hakuwachagua maskini wa dunia wawe matajiri wa imani na warithi wa ufalme aliowaahidia wampendao? 6 Bali ninyi mmemvunjia heshima maskini. Je! matajiri hawawaonei ninyi na kuwavuta mbele ya viti vya hukumu? 7 Hawalitukani jina lile zuri mliloitwa? 8 Illakini mkiitimiza sharia ya kifalme kama ilivyoandikwa. Mpende jirani yako kama nafsi yako, mwatenda vyema. 9 Bali mkiwapendelea watu, mwafanya dhambi na kuhukumiwa na sharia kama wakosaji. 10 Maana mtu awae yote atakaeishika sharia yote, na pamoja na hayo, akijikwaa katika neno moja, amekosa juu ya yote. 11 Kwa maana yeye aliyesema, Usizini, alisema, Usiue, pia. Bassi ijapokuwa hukuzini, lakini umeua, umekuwa mvunja sharia. 12 Semeni ninyi, katendeni kama watu watakaohukumiwa kwa sharia ya uhuru. 13 Maana hukumu haina huruma kwake yeye asiyeona huruma. Na huruma hujitukuza juu ya hukumu. 14 Yafaa nini, ndugu zangu, mtu akisema ana imani, nae hana matendo? Je! ile imani yaweza kumwokoa? 15 Ikiwa ndugu mwanamume au ndugu mwanamke yu uchi na kupungukiwa riziki, 16 mtu wa kwenu akawaambia, Enendeni zenu kwa amani, mkaote moto na kushiba, illakini asiwape mahitaji ya mwili, yafaa nini? 17 Vivyo hivyo na imani, isipokuwa na matendo, imekufa nafsini mwake. 18 Lakini mtu atasema, Wewe una imani, nami nina matendo. Nionyeshe imani yako pasipo matendo yako, nami nitakuonyesha imani yangu kwa matendo yangu. 19 Wewe waamini ya kuwa Mungu ni mmoja; watenda vyema. Mashetani nao waamini na kutetemeka. 20 Lakini wataka kujua, wewe mwana Adamu usiye kitu, kwamba imani pasipo matendo haizai? 21 Je! baba yetu Ibrahimu hakuhesabiwa kuwa ana haki kwa matendo, hapo alipomtoa Isaak mwanawe juu ya madhbahu? 22 Waona kwamba imani ilitenda kazi pamoja na matendo yake, na imani ile ilikamilishwa kwa matendo yale. 23 Maandiko yale yakatimizwa yaliyonena, Ibrahimu alimwamini Mungu ikahesabiwa kwake kuwa ni haki: nae aliitwa raliki wa Mungu. 24 Mwaona kwamba mwana Adamu ahesabiwa kuwa ana haki kwa matendo yake; si kwa iinaui peke yake. 25 Na Rahab, yule kahaba nae, je! hakuhesabiwa kuwa ana haki kwa matendo, alipowakaribisha wajumbe, akawatoa nje kwa njia nyingine? 26 Maana kama vile mwili pasipo roho umekufa, vivyo hivyo na imani pasipo matendo imekufa. |
Swahili New Testament © Bible Society of Tanzania, 1921.
Bible Society of Tanzania