Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni

- Matangazo -

Waroma 8 - New Testament in Swahili (Zanzibar) Revised Edition 1921

1 SASA, bassi, hapana hukumu juu yao walio katika Kristo Yesu, wasioenenda kwa kufuata mambo ya mwili bali mambo ya roho.

2 Kwa sababu sharia ya Roho ya uzima ule ulio katika Yesu Kristo imeniacha huru, nikawa mbali ya sharia ya dhambi na mauti.

3 Maana yale yasiyowezekana kwa sharia, kwa kuwa dhaifu kwa sababu ya mwili, Mungu, kwa kumtuma Mwana wake mwenyewe katika mfano wa mwili ulio wa dhambi, na kwa ajili ya dhambi, aliihukumu dhambi katika mwili:

4 illi wema uagizwao na torati utimizwe ndani yetu, tusioenenda kwa kufuata mambo ya mwili, bali mambo ya roho.

5 Kwa maana wale wafuatao mambo ya mwili huyafikiri mambo ya mwili, bali wale wafuatao mambo ya roho hufikiri mambo ya roho.

6 Kwa kuwa nia ya mwili ni mauti, bali nia ya roho ni uzima na amani.

7 Kwa kuwa ile nia ya mwili ni uadui juu ya Mungu, kwa maana haitii sharia ya Mungu wala haiwezi.

8 Wafuatao mambo ya mwili hawawezi kumpendeza Mungu.

9 Lakini ikiwa Roho ya Mungu anakaa ndani yenu, ninyi hamfuati mambo ya mwili, bali mambo ya roho. Lakini mtu aliye yote asipokuwa na Roho ya Kristo, huyo si mtu wake.

10 Na Kristo akiwa ndani yenu, mwili wenu u katika hali ya kufa kwa sababu ya dhambi, bali roho yenu i katika hali ya uzima, kwa sababu ya haki.

11 Lakini, ikiwa Roho yake yeye aliyemfufua Yesu anakaa ndani yenu, yeye aliyemfufua Yesu ataihuisha na miili yemi iliyo katika hali ya kufa, kwa Roho yake anayekaa ndani yenu.

12 Bassi, ndugu, tu wadeni, si wa mwili tuishi kwa kufuata mambo ya mwili,

13 kwa maana kama mkiishi kwa kufuata mambo ya mwili, mwataka kufa: bali kama mkiyafisha matendo ya mwili kwa Roho, mtaishi.

14 Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho ya Mungu, hao ndio wana wa Mungu.

15 Kwa kuwa hamkupokea roho ya utumwa uletao khofu, hali mlipokea roho ya kufanywa waua, kwa hiyo twalia, Abba, Baba.

16 Roho yenyewe hushuhudu pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu;

17 kama tu watoto, bassi, tu warithi; warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo; naam, tukiteswa pamoja nae illi tutukuzwe pamoja nae.

18 Kwa maana nayahasibu mateso ya wakati wa sasa kuwa si kitu kama utukufu ule utakaofunuliwa kwetu.

19 Kwa maana viumbe vyote pia vinatazamia kwa shauku nyingi siku ile watakayofunuliwa wanawa Mungu.

20 Kwa maana viumbe vyote pia vilitiishwa chini ya ubatili, si kwa khiari yake, illa kwa sababu yake aliyevitiisha,

21 katika tumaini: kwa kuwa viumbe vyenyewe navyo vitawekwa huru na kutolewa katika utumwa wa uharibifu viingie uhuru wa utukufu wa watoto wa Mungu.

22 Kwa maana twajua ya kuwa viumbe vyote pia vinaugua pamoja, na vina utungu pamoja mpaka sasa.

23 Wala si hivyo tu, illa na sisi wenyewe tulio na malimbuko ya Roho tunaugua katika nafsi zetu, tukitazamia kufanywa wana, ukombozi wa mwili wetu.

24 Kwa maana tuliokolewa kwa kutumaini; lakini kitu kilichotumainiwa kikionekana hakuna kutumaini tena. Kwa maana kile akionacho mtu, ya nini kukitumaini?

25 Bali tukikitumaini kitu tusichokiona, twakingojea kwa uvumilivu.

26 Na kadhalika Roho nae hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho mwenyewe hutuomhea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa.

27 Na yeye aichunguzae mioyo aijua nia ya Roho, ya kuwa huwaombea watakatifu kama apendavyo Mungu.

28 Na twajua ya kuwa mambo yote hushiriki kazi moja, ndio kuwapatia mema wale wampendao Mungu, yaani wale walioitwa kwa kusudi lake.

29 Maana wale aliowajua tangu asili, aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana wake, illi awe mzaliwa wa kwanza katika ndugu wengi.

30 Na wale aliowachagua tangu asili, hao akawaita; na wale aliowaita, hao akawahesabia haki; na wale aliowahesabia haki, hawa akawatukuza.

31 Bassi, na tuseme nini baada ya hayo? Mungu akiwa upande wetu, nani aliye juu yetu?

32 Yeye asiyemwachilia Mwana wake yeye, bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote, atakosaje kutukarimia na vitu vyote pamoja nae?

33 Ni nani atakaewashitaki wateule wa Mungu? Mungu ndiye awahesabiae haki.

34 Ni nani atakaewahukumu? Kristo ndiye aliyekufa, naam, na zaidi ya haya, amefufuka, nae yuko mkono wa kuume wa Mungu, tena ndiye anaetuombea.

35 Ni nani atakaetutenga na upendo wa Kristo, Je! ni shidda, au dhiiki, au adha, au njaa, au uchi, au khatari, au upanga?

36 Kama ilivyoandikwa, ya kama, Kwa ajili yako tunauawa mchana kuchwa, Tumehesabiwa kuwa kama kondoo wa kuchinjwa.

37 Lakini katika mambo haya yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda.

38 Kwa maana tumekwisha kujua hakika ya kuwa hatta mauti haiwezi kututenga, wala nzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala wenye uwezo, wala yaliyopo, wala yatakayokuwa,

39 wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe cho chote kinginecho hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Yesu Kristo Bwana wetu.

Swahili New Testament © Bible Society of Tanzania, 1921.

Bible Society of Tanzania
Tufuate:



Matangazo