Ufunuo 8 - New Testament in Swahili (Zanzibar) Revised Edition 19211 HATTA alipofungua muhuri ya saba kukawa kimya mbinguni kama muda wa nussu ya saa. 2 Nikawaona malaika saba wasimamao mbele za Mungu, wakapewa baragumu saba. 3 Na malaika mwingine akaja akasimama mbele ya madhbahu, mwenye cheteso cha dhahabu, akapewa manukato mengi illi ayatie pamoja na sala za watakatifu juu ya madhbahu ya dhahabu iliyo mbele ya kiti cha enzi. 4 Na moshi wa yale manukato ukapanda pamoja na sala za watakatifu, katika mkono wa malaika, mbele za Mungu. 5 Malaika akakitwaa cheteso akakijaza moto wa madhbahu, akautupa juu ya inchi, kukawa sauti na radi na umeme na tetemeko la inchi. 6 Na wale malaika saba wenye baragumu saba wakajifanya tayari illi wazipige. 7 Malaika wa kwanza akapiga baragumu, kukawa mvua ya mawe na moto vilivyotangamana na damu, vikatupwa juu ya inchi: thuluth ya miti ikateketea, majani mabichi yote yakateketea. 8 Malaika wa pili akapiga baragumu, na kitu, mfano wa mlima mkubwa uwakao moto, kikatupwa katika bahari, thuluth ya bahari ikawa damu. 9 Wakafa thuluth ya viumbe vilivyo katika bahari, vyenye uhayi: thuluth ya merikebu zikaharibiwa. 10 Malaika wa tatu akapiga baragumu, nyota kubwa ikaanguka kutoka mbinguni, iliyokuwa ikiwaka kama taa, ikaanguka juu ya thuluth ya mito, na juu ya chemchemi za maji. 11 Na jina lake, ile nyota yaitwa Absintho, thuluth ya maji ikawa absintho, na wana Adamu wengi wakafa kwa maji hayo kwa kuwa yalitiwa uchungu. 12 Malaika wa nne akapiga baragumu, thuluth ya jua ikapigwa, na thuluth ya mwezi, na thuluth ya nyota, illi ile thuluth itiwe giza, mchana usiangaze thuluth yake wala usiku vivyo hivyo. 13 Nikaona, nikasikia tai akiruka kati kati ya mbingu, akisema kwa sauti kuu, Ole, ole, ole wao wakaao juu ya inchi, kwa sababu ya sauti zisaliazo za baragumu ya malaika watatu, walio tayari kupiga. |
Swahili New Testament © Bible Society of Tanzania, 1921.
Bible Society of Tanzania