Biblia Todo Logo
Biblia ya mtandaoni

- Matangazo -

Ufunuo 22 - New Testament in Swahili (Zanzibar) Revised Edition 1921

1 AKANIONYESHA mto wa maji ya uzima, wenye kungʼaa kama bilauri, ukitoka katika kiti cha enzi cha Mungu, na cha Mwana kondoo.

2 Kati ya njia kuu yake na ule mto, upande huu na upande huu, mti wa uzima, uzaao matunda thenashara, mwenye kutoa matunda yake killa mwezi, na majani ya mti huo ya kuwaponya mataifa.

3 Wala hapatakuwa laana yo yote tena. Na kiti cha enzi cha Mungu na cha Mwana kondoo kitakuwa ndani yake.

4 Na watumishi wake watamtumikia; nao watamwona uso wake, na jina lake katika vipaji vya nyuso zao.

5 Wala hapatakuwa usiku huko; wala hawana haja ya taa wala ya nuru ya jua; kwa kuwa Bwana Mungu awatia nuru, nao watamiliki milele hatta milele.

6 Akaniambia, Haya ni maneno ya uaminifu na ya kweli. Na Bwana Mungu wa manabii watakatifu alimtuma malaika wake kuwaonyesha watumishi wake mambo ambayo hayana buddi kuwa upesi.

7 Tazama, naja upesi; yu kheri yeye ayashikae maneno ya unabii wa kitabu hiki.

8 Na mimi Yohana ndimi niliye mwenye kuona haya na kuyasikia. Na niliposikia na kuyaona nalianguka nisujudu mbele ya miguu ya malaika yule mwenye kunionyesha haya.

9 Akaniambia, Angalia, usifanye hivyo; mimi mjoli wako, na wa ndugu zako manabii na wa wale washikao maneno ya kitabu hiki. Msujuduni Mungu.

10 Akaniambia, Msiyatie muhuri maneno ya unabii wa kitabu hiki, kwa maana wakati huo umekaribia.

11 Mwenye kudhulumu na atende dhuluma tena; na mwenye uchafu na awe mchafu tena, na mwenye haki na afanye haki tena, na mtakatifu na atakaswe tena.

12 Tazama, naja upesi, na ujira wangu u pamoja nami kumlipa killa mtu kama itakavyokuwa kazi yake.

13 Mimi Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho, wa kwanza na wa mwisho.

14 Wa kheri wazifuazo nguo zao, wawe na amri kuuendea mti wa uzima, na kuuingia mji kwa milango yake.

15 Bali nje wako mbwa na wachawi na wazinzi na wauaji nao waabuduo sanamu, na killa mtu apendae uwongo na kuufanya.

16 Mimi Yesu nalimtuma malaika wangu kuwashuhudia ninyi mambo hayo katika makanisa. Mimi ndimi niliye Shina na Mzao wa Daud, ile nyota yenye kungʼaa ya assubuhi.

17 Na Roho na Bibi arusi wasema, Njoo. Nae asikiae aseme, Njoo. Nae aliye na kiu, na aje: na apendae ayatwae maji ya uzima burre.

18 Namshuhudia killa mtu ayasikiae maneno ya unabii wa kitabu hiki, Mtu aliye yote akiyaongeza, Mungu atamwongezea mapigo yaliyoandikwa katika kitabu hiki.

19 Na mtu aliye yote akiondoa baadhi ya maaeno ya unabii wa kitabu hiki, Mungu atamwondolea sehemu yake katika kile kitabu cha uzima, na katika ule mji mtakatifu, ambao khabari zake zimeandikwa katika kitabu hiki.

20 Yeye mwenye kuyashuhudia haya asema, Naam; Naja upesi. Amin: na uje Bwana Yesu.

21 Neema ya Bwana Yesu Kristo na iwe pamoja nanyi nyote. Amin.

Swahili New Testament © Bible Society of Tanzania, 1921.

Bible Society of Tanzania
Tufuate:



Matangazo